Fumbo la Watamu
Ali Attas
Published by
One Planet Publishing & Media Services Limited
PO Box 5649 - 00506, Nairobi, Kenya
Email: info@oneplanetpublishing.com
Website: www.oneplanetpublishing.com
© Ali Attas 2018
The moral rights of the author have been asserted.
First published 2018
All rights reserved. No part of this publication may be reproduced
or transmitted in any form or by any means, electronic or
mechanical, including photocopy, recording or any information
storage and retrieval system, without the prior written
permission of One Planet Publishing & Media Services Limited.
Enquiries concerning reproduction may be sent to the Publishing
Department, One Planet Publishing & Media Services Limited, at
the address above.
ISBN 978 9966 068 80 4
Illustrations by Henry Kirui
Printed by
Printing Services Ltd
PO Box 32197 00600, Nairobi, Kenya
1
1
Sura ya 1
Familia ya Bakari
Kokoiko ya jogoo ilinadi mapambazuko ya ufuo wa
Watamu bila kubadili ratiba. Nusu duara ya jua
la alfajiri ilichungulia upeoni. Miale ya dhahabu
ilichanua na kumwaga vivuli vyenye kumeremeta juu
ya Bahari ya Hindi. Upepo mwanana ulitikisa majani
taratibu na kuyakonyoa yale ambayo yamekauka.
Umande wa alfajiri ulitanda juu ya matita ya nyasi.
Mandhari ya Watamu yaliamka siku hiyo mpya.
Yalikaribisha wakubwa kwa wadogo kujibarizi na
kuzama katika burudani pale ufuoni.
Majahazi matatu yalitia nanga karibu na ukingo wa
bahari. Yalikuwa ya wavuvi ambao walikuwa wamerejea
baada ya kuvua samaki. Jahazi moja lilimilikiwa na
Bakari ambaye alikuwa mmoja wa wavuvi hao. Yeye
alibahatika alfajiri hiyo.
Alivua jodari na papa mmoja mkubwa kupindukia.
Tabasamu ilimjaa usoni. Alijua angemuuza yule papa
kwa bei nono sokoni. Kama kawaida Bakari angerudi
nyumbani na samaki ambao wangekuwa kitoweo
chema kwa chakula cha siku hiyo. Nyumba yake
ilizoea kula samaki waliovuliwa baharini siku hiyo.
2
2
Mara kwa mara, wakati wowote Bakari angetaka
kujivinjari na wanawe, ungemwona pwani akitembea.
3
3
Bakari na mkewe, Bahati, waliishi kwenye
nyumba ya wastani iliyoezekwa paa la makuti. Ilijikita
masafa mafupi kutoka kwenye Ufuo wa Watamu.
Bakari aliinukia katika kizazi cha wavuvi. Uvuvi
kwake ulikuwa kazi tunu sana. Aliyapenda maisha ya
bahari, na vilevile, alikuwa mpiga mbizi stadi. Moja
kati ya vipenzi vyake vya kuburudika ilikuwa kupiga
picha samaki mbalimbali wa baharini. Pia alikusanya
sanaa ambazo ziliundwa kwa kutumia viumbe hao
waliokaushwa. Haikushangaza kwamba nyumba ya
familia yake ilikabiliana na bahari.
Mandhari ya bahari ya Ufuo wa Watamu
yalionekana mtu alipochungulia dirishani. Mtu aliweza
pia kuona majabali matatu ambayo yalichomoza
kutoka baharini.
Jabali moja kubwa na bapa, lilijitandaza kuliani. La
pili kwa ukubwa, lilichongoka juu kidogo kushotoni.
La tatu, ambalo lilikuwa dogo kabisa, lilijipachika
katikati. Sura za majabali hayo zilikuwa kitambulisho
maarufu cha Ufuo wa Watamu.
Mara kwa mara, wakati wowote Bakari angetaka
kujivinjari na wanawe, ungemwona pwani akitembea.
Pembeni mwake watoto wake wangeruka wakifurahia
mandhari ya ufuoni. Vinyama mbalimbali vya baharini
vingekimbilia machoni vikihoa usalama wao.
Bakari na Bahati walibarikiwa kupata watoto
watatu. Kijana Adili alikuwa mkubwa kabisa,
4
4
kifunguamimba, akifuatwa na kaka yake mdogo,
Amana. Dada yao, Almasi, alikuwa kitindamimba.
Walipotembea pamoja, Almasi alijipachika katikati,
akijiona kama malkia.
Bakari na Bahati waliwapa watoto wao majina
yenye heru moja mahususi. Walitazamia kufanya
hivyo kungewachochea masomoni ili kujipatia
matokeo bora mitihanini.
Adili alikuwa katika darasa la sita. Alimzidi kaka
yake mdogo kwa mwaka mmoja na dada yake kwa
miaka miwili.
Pale nyumbani, wakati wa Adili, Amana na Almasi
kwenda shuleni ulikaribia. Waliandaliwa meza na
mama yao akawakaangia mayai. Harufu ya mapishi
ilichomoza dirishani. Ilihanikiza eneo alikopitia
Bakari, akitoka sokoni. Pua yake ilitanuka kidogo,
akielekea mlangoni.
“Mmm, kifunguakinywa kinaandaliwa!” alijiambia
mwenyewe.
Muda si muda, familia ilijumuika mezani na Bakari
akasimulia jinsi alivyobahatika kumvua yule papa.
Wote walimsikiliza kwa makini.
Bahati alimpokeza mumewe kwa upole, “Ilikuwa
bahati kumvua huyo papa kwani leo tulimwahidi Adili
pilau ya papa kama zawadi yake ya siku ya kuzaliwa.”
Adili alitabasamu. Ndugu zake walimtazama na
kutamka kwa sauti ya chini, Happy Birthday Adili.”
5
5
“A-a! Tulieni na mmalize kifunguakinywa chenu,”
mama yao aliwaagiza.
6
6
Adili alitingisha kichwa bila kutamka kitu.
“Baba, likizo yetu inaanza wiki ijayo. Safari hii
mtatupeleka wapi?” Amana aliuliza akitazama wazazi
wake.
“Baba ametuahidi safari ya Mombasa, au siyo?”
Adili alikatiza.
“Naam, ahadi ni deni. Tutamtembelea shangazi
yenu Mombasa mwishoni mwa wiki ijayo,” baba yao
alijibu.
Almasi na Amana walikuwa wamemaliza
kifunguakinywa chao. Waliinuka mezani kwa furaha
nusura kila mmoja adondoshe sahani yake ya chakula.
“A-a! Tulieni na mmalize kifunguakinywa chenu,”
mama yao aliwaagiza.
“Tumemaliza,” Amana na Almasi walijibu kwa
pamoja.
Bakari aliwatazama kina Adili wakiondoka mezani
na sahani na vikombe hadi jikoni. Kisha walianza
kujitayarisha kwenda shuleni. Macho ya Bakari
yaliwalenga Adili na Amana, wakishindilia mabegini
mwao ala za kupiga mbizi pamoja na mavazi maalum.
Kisha yaliinuka yakatua ukutani.
Fremu nne nzuri za picha zilizonakishiwa
vizuri zilitundikwa sambamba ukutani. Zilikuwa
zimetundikwa juu ya makabati mawili. Kabati moja
lilikuwa na rafu iliyojaa vitabu aina aina, saa pamoja
7
7
na gudulia la maua. Juu ya kabati la pili palikuwa na
taa ya totovu aliyekaushwa. Ndani palifungiwa jiko la
makaa la kuchomea nyama. Kando ya taa palikuwa
na kikombe ambacho kilikuwa na taswira ya kaa.
Kikombe hicho kilikuwa zawadi aliyopewa Bakari
shuleni alipokuwa mwanafunzi.
Macho ya Bakari bado yaliangaza pale ukutani,
yakitazama picha moja moja za wale viumbe wa
baharini. Picha hizo alikuwa amezipiga yeye
mwenyewe. Fremu ya kushotoni ilikuwa na picha ya
kamba. Fremu ya pili ilikuwa na picha ya kaa. Macho
ya Bakari yalitua kwenye picha iliyobaki na kuganda.
Sura yake ilisinyaa kidogo, akionekana kama donge
la mawazo limemtua kichwani.
Amana alimwona baba yake akitazama zile picha
mbili za kuliani ukutani.
“Baba, mbona wazitazama sana picha hizo?”
“Ah! Zimenikumbusha mikasa ambayo ilitokea
kwenye bahari ya Watamu nilipokuwa kijana.”
Adili na Almasi walitega masikio.
Bakari akaongezea, “Walitupa masaibu makubwa
baharini.”
“Pole baba,” wote watatu walitamka kwa pamoja.
“Baba yenu amewahi kunisimulia zamani. Ni
bahati tunaye hii leo,” Bahati alitamka.
8
8
“Tusimulie masaibu hayo jioni tukirudi,” Adili
alimwomba baba yao.
“Nitawasimulia.”
Baada ya nukta mbili tatu Bakari akaongezea,
“Jichungeni vyema mkienda kwenye mazoezi yenu ya
kupiga mbizi alasiri.”
Almasi, kabla hajatoka, alitupiwa swali na Bahati,
“Nyie darasa lenu limepanga nini baada ya masomo?”
Almasi alijibu, akimfuata Adili, “Tutasimuliwa
hadithi mpya na mwalimu wetu.”
Bakari alimwambia, “Tusimulie hadithi yenu leo
jioni.”
Adili, Almasi na Amana waliaga, wakafungua
mlango na kuelekea shuleni. Masaibu ya baba yao
yaliwakaa kichwani na kutawala mazungumzo yao.
“Sijui baba alipatikana na masaibu gani?” Amana
aliuliza.
“Alishambuliwa na pweza!” alijibu Almasi.
“Je, yule taa?” Adili alitupa changamoto.
Amana alimuunga mkono Adili, “Kweli, ingekuwa
masaibu kidogo baba asingesema ‘mikasa na
masaibu’”.
Mara majengo ya shule yao yalijitokeza.
“Tumeka shuleni, tusubiri jioni,” alitamka Adili.
“Baba atatufumbulia Fumbo la Watamu!”
9
9
Sura ya 2
Vitendawili vya Shuleni
Shule ya Msingi ya Papa Upanga ilikuwa karibu
na Ufuo wa Watamu. Ilikuwa na sifa ya kunyakua
matokeo bora sana miongoni mwa shule za pwani.
Watoto wa Bakari na Bahati walikuwa
wamebahatika kupata nafasi katika shule hiyo. Wazazi
waliwaonea fahari watoto wao kwa jinsi walivyofanya
bidii kusoma. Pia, walijiunga na vilabu mbalimbali vya
shule kama vile klabu cha muziki, cha kupiga mbizi
na cha masimulizi.
Kengele ya mwisho ilipolia, Adili na Amana
walijiunga na klabu chao cha kupiga mbizi na
kuelekea kwenye Ufuo wa Watamu wakiongozwa na
walimu wao watatu.
Almasi naye alikimbilia darasani walikokusanyika
wanafunzi wenzake. Wote walikuwa wamesisimka
wakimsubiri mwalimu wao.
Almasi aliinuka na kuwakumbusha wenzake,
“Mwalimu alituahidi kutusimulia hadithi ya Jirani
Hasidi leo. Mnakumbuka?”
Wenzake waliitikia kwa kutingisha vichwa vyao.
Mwalimu Zani aliingia kwa wakati darasani.
“Hamjambo?” aliiamkia klabu.
10
10
“Hatujambo mwalimu,” wanafunzi walijibu.
“Mko tayari?” Mwalimu Zani aliuliza.
Klabu kikaitikia, “Ndiyo mwalimu.”
Kimya kilitawala huku kila mwanafunzi akijisogeza
kwenye dawati la mbele. Walikuwa wamesisimka
huku wametega masikio kabisa.
“Kitendawili!”
“Tega!”
“Mvua hema na jua hema,” Mwalimu Zani alitega.
Wanafunzi waliduwazwa na kitendawili hicho.
Walinong’onezana majibu lakini kila mmoja alikataa
kutamka ufumbuzi wake. Almasi alijasiri akainua
mkono juu. Mwalimu Zani alimwashiria aseme
jawabu.
“Mwanariadha!”
Mako yalipigwa.
“Umekosea!”
Mako yalisita na kimya kutawala tena.
“Nipeni mji basi kama mmeshindwa kukifumbua
kitendawili changu.”
Wanafunzi walinong’onezana tena wakakubaliana.
“Mombasa!” darasa lilitamka.
11
11
“Zamani Mombasa iliitwa Mvita. Ni jiji lenye historia
ndefu. Lina vivutio vingi vya watalii …”
12
12
“Zamani, Mombasa iliitwa Mvita. Ni jiji lenye
historia ndefu. Lina vivutio vingi vya watalii. Nitazuru
Ngome ya Fort Jesus nijionee mizinga iliyowekwa na
Wareno walipokuja kulitawala jiji hilo ili kulikinga jiji
hilo dhidi ya maadui. Nitautembelea mtaa wa Mji wa
Kale wenye majengo ya kale. Nitakwenda forodhani
nipande jahazi la kunitembeza kando ya kisiwa cha
Mombasa,” Mwalimu Zani alitua kidogo.
“Hatimaye, nitakwenda kwenye masoko ya
Mwembe Tayari nikanunue maembe dodo. Ni matamu,
nitarudi nayo Watamu.”
Almasi alikatiza, “Utatugawia sisi, mwalimu?”
Darasa liliangua kicheko cha muda mfupi.
“Bila shaka,” Mwalimu Zani alijibu. Kisha alianza
kuisimulia hadithi ya Jirani Hasidi.
13
13
Sura ya 3
Jirani Hasidi
Jirani Hasidi kilikuwa kisa kilichomshukia Bwana na
Bibi mmoja ambao waliishi katika mtaa wa Chaani,
jijini Mombasa. Kwa bahati mbaya, walikuwa hawana
watoto. Waliishia kufuga kobe mmoja mpole ambaye
walimwokota karibu na mto, si mbali na nyumba yao.
Joto la mapenzi yao likaangukia kwa huyo kobe.
Siku moja kobe aliugua maradhi, nusura afe.
Bwana na Bibi wakampeleka kwa mganga. Mganga
alimtibu yule kobe.
Kabla ya Bwana na Bibi kumbeba kobe huyo
nyumbani, mganga aliwausia, “Huyu kobe si kobe
wa kawaida. Zamani alikuwa kasa, akiishi katika
bahari ya Ufuo wa Watamu. Hakuna ajuaye ilikuwaje
hata ikawa hivyo au vipi alikuja huku. Ni Fumbo la
Watamu. Mtunzeni. Siku moja atawafaidi.”
Bwana na Bibi walishangaa. Hata hivyo,
hawakuuliza kitu. Walimbeba kobe wao wakarudi naye
nyumbani. Siku zikapukutika. Usiku mmoja mvua
kubwa ajabu ilinyesha. Mito jirani ilifurika na maji
yakatiririka na kuishia mtaani. Kwa bahati, Bwana na
Bibi pamoja na kobe wao walinusurika wakajiepusha
na janga hilo, lakini nyumba yao ilibomoka na
kuzolewa na mafuriko makubwa ya maji.
14
14
Bwana na Bibi wakajikuta umaskini umewavaa.
Licha ya hali yao, bado walimtunza yule kobe. Kila
walichokula walimgawia. Hatimaye, walipata msaada
kutoka kwa serikali ya mtaa. Walijengewa kibanda
cha kuishi. Kobe naye akatengewa kijumba cha
kukaa mle kibandani.
Siku moja, Bwana na Bibi waliishiwa na
chakula. Walipojitupa kitandani usiku ule, matumbo
yaliwasokota kwa njaa. Kobe naye siku ile alichua
tabia ngeni. Alionekana kama anawashwa na kitu.
Asubuhi na mapema waliamka. Bwana na Bibi
walijiandaa kutafuta chakula. Walimwona kobe
ametoka kijumbani na ameegemea kilango cha
kutokea kibandani.
Walistaajabu lakini walifahamu kuwa yule kobe
alitaka kutoka nje. Walimfungulia mlango na kobe
akatoka. Alitangulia na akatambaa taratibu akielekea
mtoni. Punde si punde, kijishamba kimoja kilijitokeza.
Pale kijishambani palikuwa na kibanda cha kuku.
Yule kobe alitambaa kidogo tu kisha akasimama.
Mbele yake kulikuwa na koo aliyeatamia mayai. Yule
koo alitazamana ana kwa ana na kobe kama kwamba
wanaambizana kitu. Koo aliamka akajitenga kando.
Mayai saba yalijichua.
Kobe aliwageukia Bwana na Bibi akatoa ishara.
Bwana na Bibi walifahamu ile ishara iliyosema,
‘chukueni hayo mayai’. Tabasamu ilikunjuka nyusoni
15
15
Yule koo alitazamana ana kwa ana na kobe kama
kwamba wanaambizana kitu. Koo aliamka akajitenga
kando. Mayai saba yalijichua.
16
16
mwa Bwana na Bibi. Walichutama, wakayabeba
mayai yote taratibu, wakihoa kudonwa na yule koo.
Ajabu ni kuwa yule koo hakuonyesha ishara
yoyote ya kushambulia. Walirudi nyumbani pamoja
na kobe kwa furaha tele.
Walipoka kibandani mwao, Bwana na Bibi
walikuwa wanabanwa na njaa kali. Walichukua mayai
mawili wakayakaanga. Baada ya kumpatia kobe
sehemu, waliyala yale mayai. Matano wakayaweka
mahali pazuri kama akiba.
Usiku uliingia na wote wakalala, wakikorota kwa
kushiba.
Alfajiri, kokoiko ya yule jogoo ilicharuka kulia.
Sauti yake ilikuwa kama inanadi sherehe fulani.
Bwana na Bibi waliamka, wakaenda haraka kuchukua
mayai mengine wayapike. Walipoyatazama yale mayai,
walidhani wanaona kiinimacho. Mayai yote matano
yalikuwa yamegeuka mayai ya dhahabu!
Bwana na Bibi walifurahi kupindukia.
Walikumbuka matamshi ya yule mganga, ‘Mtunzeni.
Siku moja atawafaidi.’
Walimkumbatia yule kobe kwa furaha nyingi. Sasa
walikuwa na kitendawili kikubwa. Yale mayai matano
ya dhahabu wangeyacha wapi?
Kobe aliwaona Bwana na Bibi wakijikuna vichwa.
17
17
Walitoka mabuu pamoja na yale mayai yaliyooza
wakarudi nayo nyumbani. Walijaza yale mabuu ndani
ya yale mayai…
18
18
Aliwajongelea na kwa mara ya kwanza akatamka
kwa sauti, “Msishtuke wala msiniulize kitu.”
Bwana na Bibi waligutuka na kumtazama huku
macho yao yametumbuka kwa mshangao.
“Najua mnasumbuka kuyacha mayai yenu ya
dhahabu. Niacheni nipige bongo. Nitawaambia namna
ya kuyacha,” yule kobe aliwaambia.
Bwana na Bibi waliitikia huku bado wameduwaa.
Kobe alichemsha bongo na muda si muda aliwapa
maarifa.
Bwana na Bibi hawakuchelewa kutekeleza ushauri
wa yule kobe mpole. Walitafuta vyungu viwili, kimoja
wakakipaka rangi ya dhahabu vizuri. Cha pili
walikipaka rangi nyeusi na ya zambarau vibayavibaya.
Kisha walichukua mayai yale ya dhahabu wakayacha
kwenye chungu cheusi na zambarau.
Yai moja walilitenga kando ili lichukuliwe sokoni,
likauzwe.
Walitoka nje wakaenda kule kwenye kibanda cha
kuku. Walitafuta mayai yaliyooza. Halafu walielekea
ukingoni mwa mto. Waliokota mabuu pamoja na yale
mayai yaliyooza wakarudi nayo nyumbani. Walijaza
yale mabuu ndani ya yale mayai, wakayaunganisha
makaka yao. Halafu wakayaweka ndani ya chungu
cha dhahabu.
19
19
Walivifunika vyungu vyote viwili kwa vifuniko
ambavyo vilipakwa rangi sawa na vile vyungu.
Walipomaliza kuyacha yale mayai ya dhahabu,
Bwana alikimbilia sokoni kuliuza lile yai moja la
dhahabu.
Wanunuzi walijitokeza kwa wingi, ikabidi yai
liuzwe kwa njia ya mnada. Mfanyabiashara mmoja
akashinda na kulinunua. Thamani ya lile yai moja
ilipindukia bei ya kununua nyumba ya kawaida!
Pale sokoni, habari za lile yai zilienea kama moto
kwenye msitu mkavu. Zilimkia jirani yao ambaye
alikuwa mmoja wa wale ambao walitaka kulinunua lile
yai la dhahabu. Jirani huyo alikuwa mwingi wa udaku
na wivu. Alimwahi Bwana kabla hajaondoka sokoni
akamwuliza pale alipolipata yai lile. Bwana hakucha
siri. Jirani alimshawishi sana. Bwana alimweleza
jirani kuwa bado alikuwa na mayai mengine.
Hata bila kujua ulimi wake uliteleza, alimwambia
kuwa wameyahifadhi mayai yale kwenye chungu
kimoja.
Bwana alirudi nyumbani na mabunda ya pesa
na chakula kemkem. Njiani, alijiimbia, ‘Umaskini
umetukimbia!”
Kule sokoni, yule jirani alirudi kwa mkewe,
akamweleza zile habari za yai la dhahabu. Wivu
ulitokota rohoni mwao wakapanga mpango.
20
20
Usiku huo, yule jirani alinyemelea kibanda cha
Bibi na Bwana. Alifungua dirisha taratibu. Aliparamia
na kuingia ndani. Alinyata kimyakimya na tochi yake.
Hatimaye aligundua pahali alipodhani pamechwa
kitu. Sura yake ilikunjuka kwa furaha.
“Wajinga ndio waliwao,” alijiambia kimyakimya.
Alijongelea zaidi pale pahali akaona vyungu. “Lo!
Mbona vimekuwa viwili?” alijiuliza yule jirani.
Sasa alikuwa na mtihani.
“Chungu cheusi chenye mabaka ya zambarau
kimezeeka kupita kiasi. Na hata kifuniko chake
kimechakaa, lakini hiki cha dhahabu kinameremeta
kwelikweli. Kinang’aa kwa upya. Hiki ndicho
nitakachokibeba. Sina haja hata ya kukifungua
kifuniko chake.”
Jirani alijitwika haraka haraka kile chungu cha
dhahabu mabegani akakibeba hadi nyumbani kwake.
Alipoka nyumbani kwake, alikitua chungu hicho
chumbani na kumwambia mkewe, “Amini usiamini,
tumepata mayai ya dhahabu na chungu cha dhahabu.
Tutalala maskini, tutaamka matajiri!”
Usiku ulipita taratibu kama mwendo wa kobe.
Kila mmoja aliwaza na kuwazua mali ile ya mayai ya
dhahabu wataitumia vipi.
Alfajiri ilipowadia, wote wawili waliamka sawia.
21
21
Walikikaribia kwa pamoja kile chungu huku
wakitabasamu kwelikweli.
“Akili ni mali!” mkewe alitamka huku akifungua
kile kifuniko kwa hamu kuu.
Lo! Uvundo mkali ajabu uliwapiga puani nusura
wazimie! Ule uvundo ukawapofusha jicho mojamoja
wakawa chongo!
Mwalimu Zani alitua akalitazama darasa zima.
“Je, kisa hiki kimewafundisha nini?”
Wanafunzi walikuwa bado hawajazindukana
vizuri. Hadithi ilikamata masikio yao kwa msisimko.
Almasi alikuwa mwepesi wa kuinua mkono juu.
“Tamaa mbele, mauti nyuma!”
Mwalimu Zani alitabasamu kisha akasema,
Kweli kabisa!”
Wanafunzi walipiga mako.
Mwalimu Zani sasa alikariri kitendawili cha awali
kabla ya kukisimulia kile kisa cha Jirani Hasidi.
“Mvua hema na jua hema.”
Mwanafunzi mwingine alinyanyua mkono juu.
Aliashiriwa kujibu.
“Kobe!”
22
22
Mwalimu Zani alimpokeza, “Kobe! Umepata!”
Mako yaliwaka darasani.
Mwalimu Zani alisema, “Haya basi, tumemaliza
kwa leo. Mnaweza kusimama na kwenda nyumbani.”
Wanafunzi walisimama wakiyasukumiza madawati
yao bila kelele. Almasi alisimama akichungulia dirisha
la darasani. Kwa mbali aliwaona kaka zake wakirejea
kutoka mazoezi yao ya kupiga mbizi baharini.
Almasi alimuaga mwalimu wake pamoja na
wanafunzi wenzake akatimka mbio kuelekea kule
walikokuwa wakitembea kaka zake.
Adili, Almasi na Amana waliungana, wakaondoka
shuleni. Walishika njia ya kuelekea nyumbani. Almasi
kama kawaida yake, akijipachika katikati ya kaka
zake. Njiani, Almasi aliuliza, “Vipi mazoezi yenu ya
kupiga mbizi?”
Adili alimwona Amana amebana maneno
mdomoni. Alimwashiria ajibu.
“Leo tumepiga mbizi na tumepewa mafunzo juu ya
kuepukana na viumbe hatari wa baharini.”
Almasi alibahatisha, “Pweza na taa?”
Adili alimtazama dada yake kwa macho ya
kushangaa. “Ulijuaje?” alimwuliza dada yake.
“Nilikumbuka viumbe walio kwenye picha za
ukutani nyumbani,” alijibu Almasi huku macho
yake yaking’aa.
23
23
Amana alitazamana na Adili bila kupepesa
macho kama kwamba wanamcha dada yao kitu.
“Mbona sura zenu zinaonyesha mnanicha kitu?”
Almasi aliwauliza kaka zake.
Adili alijibu, “Amini usiamini, tumepata raki
mpya ufuoni.”
Almasi alikunja uso akauliza, “Nani tena huyo?
Anasoma shule yetu?”
Amana alicheka kidogo akajibu, “Si binadamu. Ni
kiumbe mwingine wa baharini.”
Adili aliomwna dada yao amekanganyika, “Kasa!”
Almasi alikariri, “Kasa! Huyo ndiye raki mpya?
Mbona mwanidanganya?”
Adili alimjibu dada yake, “La, hatukudanganyi. Ni
tukio la kweli.”
Adili na Amana walitazamana kisha wakakubaliana
kumsimulia dada yao Almasi kwa kupokezana zamu
ya usimulizi.
Adili alianza kusimulia, “Kisa chenyewe ni cha
kustaajabisha. Tulipotembea kutoka mazoezi yetu
ya kupiga mbizi na kurudi shuleni, Amana aliona
alama kama za kwato za mnyama kwenye mchanga
wa ufuoni. Amana alitambua kuwa zile kwato au
nyayo hazikuwa za mnyama wa kawaida. Tuliamua
24
24
Tulimpanda. Alitambaa hadi kwenye Ufuo wa Watamu.
Alitumbukia majini na kuogelea.
25
25
kuzifuata. Zilitukisha ukingoni mwa ufuo. Katika
hali ya kutafutatafuta, tuliona zile alama zimepotelea
kwenye kitita cha nyasi. Tukajasiri kupasua zile
nyasi tukisonga mbele ndani. Mara, mandhari ya
ajabu yalichuka mbele yetu. Tulipotupa macho,
tulimwona kiumbe mwenye miguu juu kichwa chini
ametumbukia kwenye shimo. Miguu yake ilitapatapa
juu akilalia gamba kubwa.”
Adili alimpungia mkono Amana aendelee kusimulia
kisa hicho.
“Tulimtambua yule kiumbe. Alikuwa kiumbe wa
baharini. Ila hakuwa mmoja wa wale walio kwenye
picha za viumbe wa baharini nyumbani. Kiumbe
huyo alikuwa kasa, tena mkubwa ajabu. Mimi na
Adili tulimkaribia tukamgusagusa. Kwa pamoja,
tukamsukuma kwa nguvu zetu zote. Alibingirika na
kutoka mle shimoni. Tulimpindua gamba juu miguu
chini. Macho ya yule kasa yalikaza na kututazama
huku yakionyesha hisia za shukrani,” Amana alitua.
Adili akaendelea na usimulizi. “Ajabu! Mara, yule
kasa alisimama huku akituelekeza tumpande
mgongoni. Tulimpanda. Alitambaa hadi kwenye Ufuo
wa Watamu. Alitumbukia majini na kuogelea. Tulikaza
mikono yetu mgongoni mwake tusije tukateleza na
kutumbukia baharini.
“Kasa huyo alikata maji akazunguka yale majabali
matatu. Tulijisahau huku tukiyafurahia mazingira ya
Ufuo wa Watamu. Baada ya muda, kasa aliturudisha
26
26
ufuoni kwa utaratibu. Tuliteremka kutoka mgongoni
mwake. Tulikuwa tumesisimka sana. Kasa alitutazama
mara ya mwisho akatambaa mchangani hadi akazama
majini. Kisha akatoweka.”
“Kisa cha kustaajabisha kweli. Laiti na mimi
ningetembezwa na huyo raki yenu mpya,” Almasi
alitamka.
Amana alikatiza, “Hivi kaka, tukitaka kusimulia
kisa hiki tutakiitaje?”
“Fumbo la Watamu,” Adili alitamka bila kusita.
Ndugu wote watatu waliangua kicheko.
Muda si muda, walishika njia na kuelekea
nyumbani. Mfukuto wa jua ulikuwa umepoa na jua
lilikuwa linazama upeoni. Anga ya samawati ilibadilika
rangi. Sasa miale ya dhahabu ilikoza na kutangaa juu.
“Leo baba atatusimulia masaibu yaliyomkuta
baharini,” Almasi alitamka.
Adili aliongezea, “Hata wewe una hadithi ya
kutusimulia au siyo?”
Almasi alitabasamu, “Ndiyo. Inaitwa Jirani Hasidi.”
Muda si muda, wote watatu walijikuta wanabisha
hodi nyumbani. Mama yao alifungua mlango haraka
kama ambaye ameotea wakati wa wanawe kuwasili
nyumbani.
27
27
Maakuli ya pilau ya papa yaliandaliwa mezani.
Familia ya Bakari na Bahati ilikula kwa furaha Adili
akitabasamu wakati mwingi.
Baadaye, familia ilimpa Adili zawadi ya siku yake
ya kuzaliwa. Almasi alifungua kiboksi na kumpa
kaka yake kikombe kama cha baba yake. Kilikuwa na
mchoro wa papa. Adili alipokea zawadi kwa furaha
tele.
Kisha, familia ilijumuika kwenye chumba cha
wageni. Bakari kama kawaida yake, alikuwa na
kijimeza mbele yake na buli la chai na kikombe chake
cha chai.
Alijishika kifua kidogo akakohoa kama ambaye
alikuwa anaitakasa sauti yake. Alimimina chai
kikombeni akanywa funda moja na usimulizi wa
masaibu yake ya ujanani yakaanza.
28
28
Sura ya 4
Kisanga cha Watamu
“Ufuo wa Watamu ulikuwa umetulia siku hiyo. Pazia
la mapambazuko lilikaribia kufunguka. Upeoni mwa
bahari, miale ya jua ilikuwa bado haijachomoza.
Sauti za kuagana na usiku taratibu zilijitambulisha
na upepo mwororo ulipuliza.
Katika bahari ya maji makuu, jahazi letu moja
lilikuwa mavuvini. Ndani mlikuwa na wavuvi wawili
wakijitayarisha kumaliza uvuvi.
Mmoja alikuwa Mzee Hamisi. Mimi nilikuwa
wa pili. Siku hiyo hatukuwa na bahati. Uvuvi wetu
uliambulia patupu na tulikuwa tumekata tamaa.
Kwa sauti hafu, Mzee Hamisi ambaye alikuwa
mzoefu kunishinda alieleza hisia zake, “Wiki nzima
tumevua samaki kemkem. Naona leo tutapata aibu.
Hatujavua samaki hata mmoja.”
Mimi nikaongezea kwa unyonge, “Kweli Mzee
Hamisi. Alfajiri nayo ndiyo hiyo yanukia. Labda bahari
ina nuksi.”
Ghaa, tulisikia sauti fulani. Sauti hiyo ilitufanya
tunyamaze kimya. Tulihisi kivuli cha kiumbe
kisichojulikana kinatujongelea omoni mwa jahazi
letu.
29
29
“Mimi nilikuwa nimeondoka upande wangu kusimama
omoni, …karibu na kifundo cha nyavu. Nilikuwa
ninakagua nyavu kuona kama zimekaa barabara…”
30
30
Mzee Hamisi alikuwa upande wa tezini, hakuweza
kuhisi kitu. Mimi nilikuwa ngamani. Niliinua mkono
wangu wa kulia nikakunja vidole juu ya kitanga
cha mkono nikanyoosha kidole cha shahada na
kukigandamiza mbele ya mdomo wangu.
Mzee Hamisi alifahamu ishara yangu. Alijikunyata
kimya. Tulitega masikio yetu na kimya cha kutisha
kilitanda. Sauti uliyosikia ilikuwa ya maji ya bahari
ambayo yalikuwa yanakupwa. Mawimbi hayo
yalikuwa yakilisogeza jahazi letu taratibu karibu na
yale majabali matatu yanayokabiliana na Ufuo wa
Watamu.
Punde si punde, mimi nilijikunjua, “Naona hamna
kitu. Nilihisi tu kuna samaki mkubwa anakata maji
karibu yetu. Labda masikio yangu yameota kutu na
kunihadaa.”
Mzee Hamisi alipiga hatua mbili na kunikaribia,
“Hata mimi katika uzoefu wangu wa uvuvi nilihisi
kuna kitu kinapasua bahari kando yetu.”
Muda si muda, tulianza kulipandisha tanga la
mashua yetu kwa utaratibu na kujiandaa kurejea
kituoni. Mara maandalizi yetu yalikatizwa.
Kivuli kile kile sasa kilikuwa kinajongelea
kwa utaratibu kama mwindaji tezini mwa jahazi
letu. Mzee Hamisi alikuwa upande wa tezini.
Hakuweza kuhisi kitu. Ukungu wa alfajiri pia
ulitatiza kwani ulikuwa bado haujaanuka.
31
31
Mimi nilikuwa nimeondoka upande wangu kusimama
omoni, katikati, karibu na kifundo cha nyavu. Nilikuwa
ninakagua nyavu kuona kama zimekaa barabara au
ndio chanzo cha sisi kutovua samaki hata mmoja.
Nilipotuliza mkono kifundoni, ghaa nyuzi za nyavu
zilianza kuchezacheza na kukazika. Kifundo cha
nyavu kilianza kufunduka. Kani ya nyavu iliongezeka
na nyavu zikatingishika kwa nguvu za ajabu.
Nilimaka kwa msisimko, “Nyavu naona zimetega
samaki mkubwa!”
“Mzee Hamisi alikimbilia pale niliposimama. Sote
wawili tukashika nyavu. Mtingiko wa nyavu sasa
ulikuwa umechacha.
“Inaonekana kweli tumevua samaki mkubwa,”
Mzee Hamisi alisema huku sura yake ikikunjuka kwa
tabasamu.
“Hapana shaka. Hata mashua yetu inanesanesa kwa
nguvu zake,” nilimjibu.
Bila kupoteza muda tulipiga nyoyo konde na
tukaanza kuzivuta nyavu kwa nguvu zetu zote.
“Tumbo la mashua liliyumbayumba kutokana
na papatiko la samaki mkubwa sana aliyekuwa
amenaswa nyavuni.
Umbo lake lilikuwa mviringo hivi. Kichwa chake
kilikuwa kimebonyea na macho yake madogo
32
32
yamechomoza pande mbili. Umbo lake bapa liliishia
nyuma kwa mkia mwembamba mrefu.
“Taa! Taa!” alitamka Mzee Hamisi kwa furaha
kubwa. “Bahati kubwa. Tumevuna mali. Huyu taa
atatuchumia hela chungu mbovu! Bila shaka atakuwa
ametokezea pango moja ambalo lipo chini ya lile jabali
bapa,” aliongezea.
Sote wawili tulikuwa tunahema kwa sababu
ya vuta nikuvute ya yule taa. Lilikuwa pandikizi
la samaki. Lilitupa changamoto kubwa kulivua.
Hatimaye, tulifanikiwa kumvua. Tulipombwaga
boharini, alikuwa anatapatapa na kupapatika.
Mzee Hamisi alimjongelea huku macho yake
yaking’aa kwa ufanisi wetu.
“Tumemvua samaki ambaye ni adimu kumpata,”
nilimwambia.
“Ninasikia sauti ya ngwenje tele pale sokoni.
Zitatumwagikia wakati wa mnada,” Mzee Hamisi
alisema huku sauti yake ikionyesha kuchangamka.
“Hebu tuache kujitia kisirani,” nilimtahadharisha.
Upeoni mwa bahari, maumbile yalifungua pazia la
mapambazuko. Upepo ulivuma na mawingu madogo
meupe yalitapanyika na kupita kwa kasi.
Jicho la jua lilichungulia upeoni na kuchomoza
ndimi za dhahabu.
33
33
“Mandhari ambayo yalijifunua mbele yangu yalinitia
ganzi mwilini. Jichwa kubwa liliibuka kutoka
baharini…”
34
34
Ndani ya jahazi, sisi tulikuwa tumemfunga yule
taa na kumtia nyavuni. Tulikuwa tukiota ndoto ya
mnada wa yule samaki. Bahari ilikuwa shwari na
jahazi likielekea karibu na yale majabali matatu.
Mzee Hamisi alianza kusinzia huku kichwa chake
kikigonga mlingoti wa jahazi. Hatukuwa na fahamu
kwamba muujiza mkubwa ulikuwa junguni.
Mara, masikio yangu yalitegua sauti ngeni
yakasisimka. Ile sauti ngeni ilitokea chini ya jahazi
letu. Ilisikika kama kitu kinapapasa ubavu wa jahazi
letu.
Ilipotokea tena, macho ya Mzee Hamisi yalifumbuka
ghaa. Sura yake ilinya kama ya mtu aliyeona swila
mbele yake akifurisha koo lake kutema mate yake ya
sumu.
Kufumba na kufumbua, jahazi liliinama. Maji
kidogo ya bahari yaliingia ndani, nikahisi kama
kwamba jahazi letu litazama maji. Kwa bahati, lilirudia
wima wake.
Mandhari ambayo yalijifunua mbele yangu
yalinitia ganzi mwilini. Jichwa kubwa liliibuka kutoka
baharini na kono moja pana ajabu likatokezea ghaa.
Lile kono lilipapasa na kutambaa juu ya ubavu wa
jahazi letu.
Kufumba na kufumbua, lile kono la jipweza
lilijizingira shingoni na kumtia tanzi Mzee Hamisi.
35
35
Alinyakuliwa hobelahobela hadi baharini. Mikono na
miguu ya Mzee Hamisi ikirukaruka hewani akajikuta yu
baharini. Alipiga mayowe wakati lile jipweza likianza
kumvuta mbali zaidi baharini.
Akili iliniganda kwa nukta mbili tatu. Kwa bahati,
iliganduka papo hapo ikachemka haraka. Ilinituma
nichukue hatua ya dharura kumwokoa Mzee Hamisi.
Nilijikuta ninapachika seti mbili za ala za kuvuta hewa
baharini pamoja na kamera yangu. Nilikimbilia jisu la
kukatia samaki wakubwa, nikalipachika kibindoni.
Nilivuta na kubana pumzi halafu nikajirusha
baharini. Mikono yangu ilikata maji kwa ustadi
kwani nilizoea kuogelea na kupiga mbizi. Nilifuata
kule alikokuwa akiburutwa Mzee Hamisi. Nilimwona
akijaribu kujisongoa kutoka kwenye kono la jipweza
huku akijiziba pua. Makono mengine ya jipweza
yalingirika hewani.
Mara jichwa la lile jipweza liliibuka kwa kishindo
na kunitazama. Kono moja likanijia kama umeme.
Nami nilifyatua pigo moja la jisu langu. Lile kono
lilikatika. Nikaona jipweza likizamisha jichwa majini
huku likimwachilia Mzee Hamisi.
Nilimwahi nikamrushia ala za kupiga mbizi.
Hakupoteza muda kwani pumzi zilianza
kumwishia. Alizivaa haraka haraka ili apate kupumua
pumzi. Kwa sekunde chache tulilisahau lile jipweza.
36
36
“…lakini nilijijua nikiwahi kutumbua majicho yake
ningeibuka mshindi.”
37
37
Mara, lile jipweza likaibuka na kuturudia.
Likanyong’oa makono yake juu na kutushambulia
tena. Kono lake jingine lilimzingira Mzee Hamisi
tumboni likamvuta kwenye kina cha bahari. Nami
nilipiga mbizi na kuwafuata. Jipweza lilitua chini
kabisa ya mtandazo wa bahari. Lilijitandaza kwenye
vijabali ambavyo vilichongoka kama mikuki.
Nguvu za pweza zilimzidia Mzee Hamisi akawa
hawezi hata kupumua. Macho yake yalitumbuka,
yakatazama bahari ile iliyotifuka juu yake. Yalionekana
kama aliyepigwa na dhoruba ya kimbunga.
Nilipiga mbizi mpaka karibu yao. Niliona mikono
ya pweza ikikaza zaidi.
Mzee Hamisi alipiga mayowe ya kutaka msaada
wa dharura. Alikuwa taabani. Hajiwezi kabisa.
Nilipiga moyo konde. Huku nguo zangu zimetota
kwa maji, nilipambana na lile jipweza. Maarifa ya
kupigana na pweza nilikuwa sina, lakini nilijijua
nikiwahi kutumbua majicho yake ningeibuka
mshindi. Nililiotea wakati lile jipweza likitupa
makono yake mawili kunizingira. Nami nikatumia
hila mpaka nikafanikiwa kulitumbua majicho yake.
Nilimkumbatia Mzee Hamisi, nikaogelea naye hadi
juu ya bahari.
Lile jipweza lilibaki nyuma likizama chini huku
makono yake yakijinyong’oanyong’oa.”
38
38
Hapo, Bakari alitua. Aliwatazama wanawe ambao
walikuwa wametega masikio. Usimulizi wa masaibu
ya baba yao uliwasisimua. Hata Bahati alionekana
amesisimka licha ya kuyasikia yale masaibu ya
mumewe kwa mara nyingine.
“Baba, hali ya Mzee Hamisi ilikuwaje baada ya
kumwokoa?” aliuliza Amana.
“Tulimpeleka hospitalini akatibiwa kwa siku tatu.
Alipona kabisa. Shingoni, hata hivyo, alibaki na kovu
pale alipobanwa na kono la lile jipweza,” Bakari alijibu.
Baada ya nukta mbili tatu hivi aliongezea, “Lakini
siku hiyo Mzee Hamisi aliniambia kitu kimoja
ambacho sitakisahau. Kila niendapo kupiga mbizi ni
muhimu kufutika jisu langu kibindoni.”
“Hata mwalimu wetu wa kupiga mbizi ametuagizia
tufanye hivyo,” Adili alimpokeza baba yake.
“Baba, mimi natamani kuwa stadi wa kupiga
mbizi na kuogelea kama wewe. Nitaweza kuokoa watu
ambao wanakabiliwa na hatari,” alisema Adili.
“Hata mimi,” alipokeza Amana.
“Najua mmefanya mazoezi mengi ya kupiga mbizi
shuleni. Tukirudi kutoka Mombasa wakati wa likizo
yenu, nitawapeleka baharini tukapige mbizi pamoja,”
aliahidi Bakari.
Sura za Adili na Amana zilikunjuka kwa tabasamu.
Sura ya Almasi ilisinyaa kidogo.
39
39
Mama yake alitambua hisia za binti yake.
Alimshika bega, “Usijali binti yangu. Utajifunza
jingine la kusaidia watu kama vile kaka zako.”
Hata ile hadithi yake ya Jirani Hasidi aliibania.
Wiki ilikatika na likizo ikabakiza siku moja.
Walifunga safari ya Mombasa kumtembelea shangazi
yao. Ziara yao ikapita upesi kama kimondo ambacho
hufyatuka angani.
Safari ya kurudi Watamu iliwadia kwa haraka. Adili
na Amana walichangamka sana njiani. Mazungumzo
yao yalitawaliwa na ahadi ya baba yao. Kesho yake
angewapeleka kwenye bahari ya Watamu kupiga
mbizi.
40
40
Sura ya 5
Siri ya Majabali Matatu
Ufuo wa Watamu ulikuwa unashuhudia miale ya
dhahabu ikipasua anga na kulifukuza giza la usiku.
Rasharasha ya mvua ilisababisha kutanda kwa upinde
wa rangi saba. Ulijitandaza angani kama kwamba
ulikaribisha wageni pale ufuoni. Mawimbi ya bahari
yaliyumbayumba na maji kukupwa. Hali ya bahari
ilikuwa nzuri kwa kuogelea na kupiga mbizi.
Harufu ya chumvi na shombo la samaki zilienea
kwingi. Joto lilianza kufukuta jua lilipopanda angani.
Bakari na wanawe wawili wa kiume, Adili na
Amana, tayari walikuwa wamewasili kwenye Ufuo wa
Watamu pindi tu alfajiri ilipopambazuka. Walikuwa
wamevalia mavazi yao ya kupiga mbizi. Walikuwa
wakiogelea karibu na yale majabali matatu kuamsha
viungo vyao. Upepo mwororo ulipapasa nyuso zao
zilizochangamka.
Kando ya yale majabali matatu, majahazi ya wavuvi
yalitia nanga na baadhi ya wavuvi walitembea kwenye
maji madogo wakipishana na Bakari na wanawe.
Walibeba mavuvi yao wakielekea ufuoni na hatimaye
sokoni kuchuuza samaki wao.
Bakari aliwageukia Adili na Amana. Aliwakumbusha
maagizo aliyowapa nyumbani kuhusu kupiga
41
41
Kwenye kina cha bahari bustani ya mimea yenye rangi
za kuvutia ilijifungua.
42
42
mbizi, “Kumbukeni kunifuata ubavuni, nyuma
kidogo. Amana ataogelea katikati yangu na wewe
Adili. Utamchunga mdogo wako endapo patatokea
tukio tusilotazamia.”
Adili aliitikia huku Amana akijipachika katikati
yao wakijiandaa kupiga mbizi.
Bakari alipiga mbizi, Amana akamfuatia ubavuni
na Adili akajiweka kushotoni mwa Amana.
Chini yao bahari ilifungua pazia la kusisimua.
Waliona mwamba ukifunikwa na marijani na
matumbawe yenye mchanganyiko wa rangi nyekundu
na ya machungwa. Walizama chini zaidi taratibu huku
baba yao akigeuka kuwatazama wanawe mara kwa
mara.
Kwenye kina cha bahari bustani ya mimea yenye
rangi za kuvutia ilijifungua. Uhai ulipwita kwa mvuto
usio na kifani. Mazingira hayo ya chini ya bahari
yalikuwa kivutio kikuu cha watalii kupiga mbizi
kwenye bahari ya Ufuo wa Watamu.
Bakari na wanawe walipiga mbizi na kuizunguka
ile miamba ya yale majabali matatu. Walipishana na
samaki wa kila sampuli.
Bahari ilikuwa shwari na upigaji mbizi uliendelea
huku Adili na Amana wakimfuata baba yao ambaye
alipasua maji kama samaki.
43
43
Dakika zilipita na sura za Adili na Amana zilikuwa
zimejaa msisimko na furaha. Hatimaye, walikuwa
wamepata nafasi ya kupiga mbizi na baba yao.
Walikuwa wamepiga mbizi na kukaribia mwamba
wa lile jabali bapa kuliani mwa Ufuo wa Watamu.
Kwa mbali, waliona kitu kama tundu hivi. Baba yao
aliwaashiria Adili na Amana wamfuate. Walipokaribia,
waliona tundu kubwa ambalo limefunikwa na giza
tupu.
Kutoka kiunoni Bakari alichopoa tochi akamlika
mdomo wa lile tundu. Sasa tundu lilijitambulisha
kinagaubaga. Lilikuwa pango kubwa. Bakari katika
upigaji mbizi wake wote wa bahari ya Watamu, alikuwa
hajawahi kupiga mbizi ndani ya pango. Kwa kuwa
hakuwa peke yake alijasiri kujisogeza na kuingia ndani
ya lile pango. Adili na Amana walimfuata baba yao
bila kunung’unika. Walijua kuwa baba yao alikuwa
stadi wa kupiga mbizi. Hawakuwa na chembe ya la
wasiwasi.
Adili na Amana pia walikuwa na tochi zao. Sasa
walizifutua kutoka vibindoni mwao wakaongeza
mwanga mle ndani ya pango.
Baba yao alipunguza kasi ya kupiga mbizi. Alianza
kupapatisha miguu yake nyuma taratibu. Wanawe nao
vilevile walipunguza kasi ya kuogelea wakihakikisha
wako ubavuni, nyuma kidogo ya baba yao kama
walivyoagizwa awali.
44
44
Hamu ya kupiga mbizi pangoni ilimfanya kusahau
hatari zinazojitokeza mapangoni ingawa Mzee Hamisi
aliwahi kumtajia kuwepo kwa pango hilo zamani.
Hakukumbuka ushauri wake ambao ulimtanabahisha
juu ya hatari za kuogelea pangoni. Sasa alikuwa siyo
tu anajihatarisha bali vilevile anawaingiza wanawe
katika mkabala wa hatari.
Tochi zao zilipasua kiza cha pangoni. Bakari na
wanawe walizidi kusonga ndani ya lile pango. Ghaa,
wimbi dogo la samaki lilitimka kutoka ndani. Wimbi
hilo liliwakumba na kuwagutusha Bakari, Adili na
Amana.
Kufumba na kufumbua, jichwa la dubwana la
kutisha lilitokea kwa mbali. Sura yake ilikuwa kama
ya nusu mamba na nusu mburukenge. Mijicho yake
ya magololi iliwaka kama kurunzi na kuangazia kule
walikokuwa Bakari na wanawe.
Amana alikuwa wa kwanza kuliona. Alitingisha
mkono wake na kuelekeza kidole pangoni. Bakari
alizindukana. Alifutua kamera yake. Kama ilivyo kuwa
desturi yake akafyatua. Miale ya mwangaza ilitua juu
ya sura ya jichwa la dubwana hilo. Ile miale ilikuwa
kama imelichokoza dubwana hilo. Mara, lilijawa na
mori na kuanza kuwajia kwa kasi.
Bakari alijipindua haraka na kutahadhari,
akiashiria wanawe wabadilishe mkondo na kurudi
walikoingilia.
45
45
Nyuma yao walihisi mwendo wa lile dubwana
likiendelea kuwakaribia.
46
46
Punde si punde, walijikuta wanakimbizwa mle
pangoni na lile dubwana lenye hasira za mkizi.
Dakika zilionekana kama miaka na mdomo wa
pango haukujitokeza. Dubwana liliwakaribia huku
likikenua domo lake lenye safu ya mijino iliyojikita
jinywani kama meno ya msumeno aina ya jambeni.
Adili alianza kuitingisha tochi yake. Walipomtazama,
waliona mwanga wa tochi yake ulikuwa unaa.
Bakari na Amana walitazama tochi zao. Mianga ya
tochi zao pia ilianza kua.
Nyuma yao walihisi mwendo wa za lile dubwana
likiendelea kuwakaribia. Mzizimo uliwakumba wote
watatu.
Matamshi ya Mzee Hamisi yalimgonga Bakari
kama jicho la sunami. Alianza kujuta na kujilaumu
kwa kuwatia wanawe katika jungu la hatari kubwa.
Bakari alijua sasa walikuwa hawana la kufanya
ila kupambana na lile dubwana. Alikumbuka jisu
alilolifutika kibindoni kabla hawajaanza kupiga mbizi.
Alilifutua huku akipapasa kuona kama wanawe
walikuwa ubavuni. Alifaulu kuwaashiria kila mmoja
aogelee ubavuni mwake.
Muda si muda, dubwana liliwavamia.
Uzoefu wa pambano lake na lile jipweza alipokuwa
akimwokoa Mzee Hamisi ulimsaidia. Bakari alijua
mijikono ya lile dubwana isingeweza kukatika hata
47
47
kwa pigo kubwa la jisu lake. Alijikakamua na kubaki
kimya kama mamba anayewinda mnyama. Aliliotea
mijicho yake.
Adili na kaka yake walikumbuka mazoezi yao ya
kupiga mbizi shuleni. Mwalimu wao daima aliwashauri
wabebe bisibisi ya kujitetea. Walichopoa bisibisi zao
wakisimama imara ubavuni mwa baba yao.
Dubwana lilipoinua jichwa na kuwashambulia,
Bakari alipigwa shavuni na kono la lile dubwana.
Chumvi ya bahari iliingia jerahani na kumtia uchungu
mkali kupindukia. Bakari na wanawe, hata hivyo,
waliwahi shabaha yao, wakalidunga jijicho moja.
Dubwana lilirudi nyuma kwa maumivu. Sura yake
ilizidi kuchusha kwani sasa lilipandwa na mori ya
kulipiza kisasi.
Mara, tochi zao zilizimika kabisa na giza
likawafunika gubigubi.
Kutokana na wasiwasi na hofu, dira ya kuelekea
mdomoni mwa lile pango iliwapotelea. Wala hawakujua
lile dubwana lingeshambulia kutoka upande gani.
Bakari alijua kuendelea kujuta kusingemsaidia
katika mkabala ule wa hatari kubwa. Alijikakamua
tena huku ameshika jisu lake akibana pumzi ili aweze
kuhisi dubwana lingeshambulia kutoka upande gani.
48
48
Kwa mbali, waliona duara ya mwanga. Kisha
wakaona umbo likiziba ile duara. Upesi Bakari
aliwashika wanawe na kuwavuta waogelee kule
walikoona ile duara ya mwanga. Nyuma yao walisikia
pumzi kali za lile dubwana likiwakaribia.
Bakari na wanawe waliogelea kwa kasi ya uwezo
wao, lakini dubwana tayari lilikuwa jirani yao.
Lilikenua domo lake tayari kuwashambulia tena.
Mara, mbele yao palizuka shani. Waliona kasa
mkubwa ajabu akiwajia. Amana alimtambua yule
kasa. Alikuwa yule raki yao! Nyuma yao lile dubwana
lilinyong’onyea lilipomwona yule kasa. Lilipinduka na
kurudi pangoni.
Kasa aliwakaribia kisha akapinduka na kuogelea
kuelekea kule kulikochomoza duara ya mwanga.
Punde si punde, walijikuta wanafuatana na yule kasa
hadi kwenye mdomo wa lile pango.
Hatimaye, Bakari, Adili, Amana na yule kasa
walitokezea baharini. Walikabili Ufuo wa Watamu.
Mara, kasa alipasua maji akapiga mbizi na kutoweka.
Bakari, Adili na Amana wakabaki wameduwaa. Walijua
kuwa wameshuhudia mkasa ambao watausimulia
miaka na mikaka.
Njaa ilifukuta matumboni mwao kwani saa nyingi
zilipita tangu waingie baharini kupiga mbizi. Miili
yao pia ilikuwa michovu kutokana na yale masaibu
ambayo yalitokea pangoni. Walirudi nyumbani.
49
49
Aliiweka ile picha kwenye fremu mpya, kisha
akaitundika ukutani kando ya ile fremu yenye picha
ya pweza.
50
50
Waliingia nyumbani kimyakimya. Walikuta chakula
cha adhuhuri kipo mezani. Walikula na kujitupa
vitandani kwa mapumziko.
Jioni walipoamka, familia ilikusanyika kwenye
chumba cha wageni. Bakari na wanawe wakawasimulia
Bahati na binti yake, Almasi, masaibu yaliyowapata
baharini.
Bakari alikwenda dukani kesho yake kusafisha
picha alizokuwa amezipiga walipokuwa wakipiga
mbizi pangoni. Baada ya kusashwa, alirudi na
picha za lile dubwana ambalo liliwashambulia
pangoni. Aliiweka ile picha kwenye fremu mpya, kisha
akaitundika ukutani kando ya ile fremu yenye picha
ya pweza.
Almasi alimkaribia baba yake akamwuliza swali
changamoto, “Baba, mbona lile dubwana lilinywea na
kurudi pangoni lilipomwona yule kasa?”
Bakari alitafakari kidogo kisha akamjibu binti
yake, “Mmmh! Kweli hata sisi tukio hilo kidogo
lilitukanganya. Labda tuliite Fumbo la Watamu.”
Mwisho