
24
“Mbona huniogopi?Wataka nikubadilishe kitoweo
sasa? Nimewala wanyama wengi. Ni wewe
umebaki na leo nitakuua na kula nyama zako,”
fisi alimtisha sungura.
“Hakika fisi, sikuogopi. Nimekuwa nikikutafuta
kwa kuwa ninajua una nguvu. Pia wewe unapenda
kula nyama tamu.Je,una habari kuwa paa wanane
wamekamatwa na mwindaji?” sungura aliuliza.
“Sina habari hata! Paa wanane! Walikamatwa
lini?Wako wapi unipeleke nikawale?Wajua kati ya
wanyama wote niliokula nyama zao, ninaipenda
sana nyama ya paa. Ni tamu kupindukia,” fisi
alisema huku mate yakimdondoka.
“Mwindaji aliwakamata pangoni. Amewafungia
katika mtego ng’ambo ya mto.Nimetoka huko leo
asubuhi. Ndiyo maana ninatembea nikikutafuta.
Je, utakubali kufuatana nami?” sungura aliuliza.
“Twende basi. Twende tukale nyama. Pongezi
sungura.Wewe ni rafiki unayenijali. Ikiwa ni kweli,
hakika sitakuua lakini ikiwa ni uongo, lazima leo
nikuue,” fisi alisema kwa uchangamfu.
“Sawa, lakini ujue kila kitu kina sheria zake.
Mwindaji akikuona atakutambua mara moja. Ni
lazima ufanane na paa ili mwindaji akuruhusu
uingie katika mtego,” sungura alimwambia fisi.