Dua ya Faraja
Sophy Onura
Msururu wa Mbayuwayu
Dua ya faraja
Sophy Onura
Imarisha Lugha
Dua ya Faraja
Kimechapishwa na:
Queenex Publishers Ltd.
S.L.P 56049-00200, Nairobi, Kenya.
Simu: 0727 794 498, 0715 808 200
Barua pepe: info@queenexpublishers.co.ke
queenexbooks@gmail.com
Tovu: www.queenexpublishers.co.ke
Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kuiga, kunakili,
kupigisha chapa kutafsiri au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi
yoyote ile bila idhini, kwa maandishi ya Queenex Publishers
Limited.
Chapa ya kwanza 2018
ISBN: 978-9966-115-11-9
1
Sura ya kwanza
Tik! Tak! Akrabu za saa zilitoa sauti kwa mfululizo.
Sauti hiyo ilimwudhi sana Gambo aliyekuwa akiufurahia
usingizi mwanana asubuhi ile mbichi. Kwa usaidizi wa
vidole vya shahada, aliyaziba masikio yake ili aepuke
alichokiita kelele na kisirani tukutu za saa.
2
Papo hapo, alianza awamu ya pili ya usingizi
huku akikoroma kwa sauti ya kutisha ungedhani alikuwa
katika mashindano na vyura wakorotao kidimbwini.
Ilikuwa dhahiri kuwa Gambo alikuwa akifurahia uhondo
wa usingizi wa kipekee pale kitandani. Kwa siku nyingi
usingizi kama huo ulikuwa umeadimika kwake mfano wa
wali wa daku.
Awali hakuwahi kupata mwanga kuhusu utulivu
wa mawazo wala kivuli cha kujisetiri kutokana na ukali
wa matatizo. Daima hakuelewa maana ya neno raha.
Kwake lilikuwa neno tu labda msamiati wa wasomi
uliotiwa kwenye kamusi kimakosa. Aliishi maisha ya
bahati nasibu. Kufanikiwa kwake katika jambo lolote hasa
kupata mahitaji ya kimsingi, kulitegemea kuangukiwa na
nyota ya jaha.
Mbali na Gambo mwenyewe, hakuna mwingine
aliyejua namna alivyojipata katika utumwa ule. Kwa
sababu ya mazingira alimoishi, aghalabu Gambo alijikuta
akiwa mwele wa ndwele si haba kama vile utapiamlo,
homa ya matumbo na mafua. Hakuwa na budi kukubali
maisha na mawimbi yake yalivyomvamia.
Kadri mawimbi hayo ya maisha yalivyompeperusha
kama ukuti wa mnazi, ndivyo alivyolazimika kuufuata
mkondo wake. Hakuufuata kwa kupenda. Kichwani alijawa
na maswali mpururu yaliyomfanya ashibe kwa uchungu
na majuto. Hata hivyo, si walisema wahenga lisilo budi
hubidi? Alisadiki usemi mkongwe kuwa dunia ni tambara
bovu. Alijiuliza mara kwa mara kwa nini katika umri huo
mdogo alilazimika kubeba mzigo mzito wa maisha?
Gambo alizidi kulala na kukoroma. Sasa alikuwa
3
maskini asiye na mbele wala nyuma. Katika ile hali ya
uchochole, Gambo alijipata yu miongoni mwa kundi la
vijana ambao walirandaranda ovyo mijini wakitafuta riziki
kwenye majaa ya taka. Vilevile, katika siku takatifu
alivyoiita Gambo, angekimbia kwenye mkahawa na
kununua kopo la uji katika mkahawa wa Makangati.
Hiyo ni siku ambayo angepata msamaria mwema ampe
angalau shilingi tano. Makangati, mkahawa maarufu
katika mtaa wa Rabeki, ulisifika sana hasa kwa mapishi
yake mazuri na vyakula ainati kama hawhaw yaani
dagaa wa kukaanga, ugali macho yaani ugali kwa mayai
na uji moto. Licha ya vyakula vingi kuwepo, vyakula
hivyo viliuzwa kwa bei nafuu sana. Hilo ndilo lililofanya
Makangati kuwameza wateja sufufu pasi na kuwatema
hadi pale walipomaliza kuhudumiwa.
Kitaka, mwanamume aliyekuwa kidurango, mnene
kwa kimo na mwenye pua iliyochongoka, alikuwa mmoja
kati ya wahudumu katika mkahawa ule ulioitwa Makangati.
Aliifanya kazi yake kwa dhati na imani kuliko wahudumu
wengine. Utendakazi wake uliongeza nguvu sumaku ya
kuwavutia wateja katika mkahawa ule.
Kila wakati Gambo alipoangukiwa na nyota ya
jaha na kupata hela, alimkuta kisadfa yule Kitaka akiwa
mhudumu wa zamu. Hivyo basi ikawa ni bahati maradufu
kwake Gambo. Kwanza Kitaka angemtilia uji mwingi zaidi
ya kipimo cha kawaida. Pia, angempa masalia ya chakula
walichokuwa wamekila wateja na kusaza.
Wawili hao wakawa wanakuza uhusiano wa karibu
uliokua na kuwa urafiki wa kupigiwa mfano. Urafiki
wa Kitaka na Gambo mtu mzima na mtoto! Ajabu.
4
Walipokutana walikuwa kama mtu na nduguye hasa.
Kwa mara ya kwanza Gambo aliweza kutabasamu
na kuwa na sababu ya kutabasamu kila alipopata fursa
ya kuutembelea mkahawa wa Makangati. Alipaona hapo
mkahawani mfano wa nyumbani penye mapenzi, malezi
na furaha. Alipokuwa pale kwa dakika chache tu aliweza
kuufungia nje ulimwengu wake wa shida na matatizo.
Aliweza kucheka tena. Alijihisi akiwa mtoto kabisa.
5
Kila kulipokucha, Gambo alituma dua kwa Muumba
wake ampe sababu ya kufika pale mkahawani. Hii ikawa
sala ya kila siku. Akawa anaishi tu kwa ile ile bahati
nasibu ya kila siku, pasipo na kujali mavazi wala makazi
ila tumbo tu.
Tumbo lilo hilo ndilo lililomsukuma Gambo
kupevuka zaidi na kila kulipokucha alisuka mikakati
mipya ya kupata chakula. Alizurura mitaani na hata
kujipata kwenye mitaa mipya iliyokuwa mbali sana na
mtaa wake wa awali yaani Rabeki. Kila alipojaliwa kupata
masalia ya vyakula kwenye majaa ya taka, kwake yeye
angesherehekea. Angesherehekea na kumshukuru
Mola kumjalia riziki. Baadhi ya wapitanjia waliingiwa na
kichefuchefu wakatema mate. Kwake hakujali kitu, ilikuwa
mfano wa karamu tosha. Waama, ganda la muwa la jana,
chungu kaona kivuno.
Baada ya kuzurura kutwa kucha kwenye mitaa
ya mbali, angerudi mtaani Rabeki kwenye makazi yake
pamoja na ndugu zake kwani alijua fika kuwa mbacha
hauachwi kwa msala upitao. Kijana Gambo ndiye
aliyekuwa mdogo kati ya ndugu zake wote. Kwa hivyo
ili kuendelea kuwa mmoja kati ya wote kwenye kundi lile,
alilazimika kutia bidii zaidi ili kupata chakula cha kuwatosha
wote. Wenzake waliona kuwa watu walimsikitikia katika
udogo wake kwa hivyo wangemsaidia upesi kuliko wao.
6
Hata haikuwa kazi rahisi kwake. Isitoshe, wale
wenzake wangempa kichapo cha mbwa iwapo angerudi
bila chakula cha kuwapa. Maskini Gambo! Alipatwa na
shinikizo la kimawazo. Badala ya kuwategemea wakubwa
wake ni wao waliokuwa wakimtegemea!
Kwanza alipoikumbuka siku aliyopokea kichapo
kilichomsababisha kupoteza fahamu, alitokwa na machozi
yaliyomwacha na machungu ndani ya moyo wake. Kovu
moja kipajini pake lilikuwa kumbukumbu tosha ya kipigo
hicho.
Machungu aliyohisi moyoni na mwilini, yalikuwa
kama kutia msumari moto juu ya kidonda na kuunda
donda ndugu lisilosikia dawa wala kafara. Uchungu wa
7
mwilini angeweza kuustahimili, wa moyoni angeufanyaje?
Angeupoza na nini? Hivyo basi, ili kuepuka yaliyojiri
wakati huo kujirudia, alijikaza na kupekuapekua ndani ya
yale majaa. Ombi lake likiwa moja tu, kupata chakula.
Alijipata mara nyingi akililaumu tumbo. Ilimdhihirikia kuwa
matatizo yake mengi yalisababishwa na tumbo. Kichapo
alichokipata kilisababishwa na tumbo lilo hilo. Hakika
aliapa ndani kwa ndani kuwa laiti angalikuwa na uwezo
angaliliondoa tumbo lake na kuwatupia mbwakoko.
Nyakati ngumu alizokuwa akipitia Gambo, ndizo
zilizomfanya siku zote kukosa furaha.Yaliyokuwa moyoni
mwake pia yalichangia pakubwa. Ajabu ni kwamba,
hakuna aliyejua siri iliyokuwa moyoni mwake Gambo,
hata wale ndugu zake hawakujua. Kweli moyo wa
binadamu ni msiri; ungefunguka...
Gambo alionekana mnyonge asiye na furaha wala
amani na daima dhaifu. Wakati ule alipokuwa amezama
katika durusu za maisha yake, alihisi mgoto kwenye bega
lake. Hakushtuka bali aliendelea na safari yake. Maisha
mtaani yalikuwa na migongano na misuguano mingi,
hivyo basi mgoto mmoja begani haukuwa ajabu kwake.
Lilikuwa jambo la kawaida tu.
Kabla ya kupiga hatua mbili, aliguswa tena na mara
hii mgoto ukafuatiwa na jina lake.
Gambo! sauti aliyoijua na kuizoea ilisikika. Siku
nyingi umepotea, lakini dunia kaka ndogo. Nkakusaka
kaka kote kote nthaani nisikupate. Leo hii nashukuru
Maulana kakuleta, alisema Kitaka huku amekopoa
tabasamu sadakta iliyodhihirisha mpangilio mufti wa
8
meno kinywani mwake; meno yaliyokuwa meupe pepepe
kwenye ufizi mwekundu. Kweli asiyemzoea angemwona
kiumbe cha kuogofya iwapo ingekuwa mara yake ya
kwanza kukutana naye.
Kitaka, aliyekuwa ameathirika si haba na lafudhi
ya kikwao, alizungumza kwa mahadhi ya kupendeza.
Alikuwa mzaliwa wa Pwani ya Kenya, kwenye kisiwa cha
Wasini.
Sauti yake ya radi iliyokuwa ya kipekee ilimfanya
ajulikane kote mtaani kwa jina la utani la bwana Radi,
ingawa si watu wengi walioelewa asili ya lakabu hiyo.
Isitoshe, mavazi yake yalikuwa ya kipekee pia. Siku
zote alivalia suti ya rangi ya kijivu, suruali iliyopachikwa
milia miembamba ya rangi ya samawati kuanzia kiunoni
hadi miguuni kwenye muundi. Nalo shati lilikuwa fupi
lenye ukosi mkubwa ulioninginia ungedhani ni masikio ya
sungura. Kwa kweli suti ile ilimchukua Kitaka sawasawa
na kudhihirisha tumbo lake vilivyo. Lilitokeza mbele
na lilitikisika kila alipocheka. Hivyo basi, umbo lake
lilionekana waziwazi alivyoumbika huku mavazi yake
yakipigia debe umbilikimo wake.
Kitaka alikuwa na tajriba ya miaka mingi katika upishi
na mapishi yake yalipendwa na kila mja aliyetembelea
mkahawa wa Makangati mtaani Rabeki. Alikuwa mcheshi
na mwingi wa furaha, ambaye hakukosa neno la kuchangia
katika mazungumzo yoyote.
Naam rafiki yangu waelewa hizi shughuli kaka
hizi shughuli kakangu, Gambo alimjibu Kitaka huku
akionekana kushangaa na mwenye hofu kwani hakutaka
kutaja shughuli zile halisi alizozirejelea.
9
Thughuli gani kaka? Thughuli halisi zenyewe ndizo
zanileta kwako. Twende nikakueleze, alimwelekeza
Gambo kwa haraka.
Wakati ule Gambo hakujua aseme au ajibu nini.
Hakupenda kuharakishia kutoa uamuzi wa mara moja,
lakini siku ile alilazimika kupanga na kupangua mawazo
yake ili atoe uamuzi wa haraka.
Wafikiria nini bwana, twende chemba
tukazungumze. Niliyo nayo leo nina uhakika yatakufaa.
Twendee,”… alisema Kitaka.
Gambo akimkata Kalima na kusema, Nafsi yangu
yanitatiza lakini mahitaji yanizidi.
10
Hilo halikuwa jibu lililomlenga Kitaka bali kibwagizo
alichokipenda kukikariri angalau kujipa moyo alipokuwa
katika zile harakati za kutafuta chakula kwenye mapipa
kule mitaani. Wakati mwingi alikariri mashairi yake
aliyokuwa akijitungia endapo angepata fursa.
Ajabu ni kwamba Gambo hakuwa amesoma sana
kwani kikomo chake cha elimu kilikuwa darasa la tatu,
lakini alijua kuandika na kusoma vizuri ingawaje kwa
Kiswahili tu. Mkoba aliokuwa akitumia kwenda shuleni,
bado aliubeba kila alipoenda kule mitaani. Mle ndani
mlikuwa na kalamu na kitabu ingawaje vikuuukuu.
Alimgeukia Kitaka na kumsaili, Lipi la mno? Wataka
usaidizi?Una chakula cha kunipa? Yote hayo yalikuwa
baadhi tu ya maswali yaliyokuwa moyoni mwa Gambo.
Kitaka aliongoza njia naye Gambo akamfuata nyuma
bila kufahamu pale alipoelekea. Alikuwa na matumaini ya
kupata majibu yote ya yale maswali aliyokuwa nayo.
Twende haraka kijana. Niliyo nayo moyoni ni ya
dharura, Kitaka alimhimiza Gambo.
Baada ya kutembea kwa muda mrefu, hatimaye
rafiki hao wawili walifika kwenye kibanda kimoja. Waliketi
kwenye bao na kuanza gumzo. Aliyohadithiwa Gambo
yalimfanya atabasamu kwa furaha na hamu kubwa. Alipiga
darubini na kuona shida alizokuwa nazo zikiondoka na
kutokomea tokomoko. Kupata chakula na mavazi mazuri
lisingekuwa tatizo tena.
Kitaka alikuwa amemuahidi kazi ambayo
ingemwondolea shida zote, alitakiwa pia kuianza siku ile
ile. Basi baada ya kuelewana, waliondoka sehemu ile
11
na kuelekea alikoishi Kitaka. Njiani walitambiana hadithi
huku wakicheka ovyo na kwa furaha.
Baada ya kupewa mavazi rasmi ambayo alielezwa
kuwa ni ya kufanya kazi, Gambo alifurahi sana na
kumshukuru Kitaka. Kisha wakaondoka ili Gambo
aelekezwe mahali na kuelezwa namna ya kufanya kazi.
Gambo alimfuata unyo unyo, kwapani amepachika
ule mkoba wake. Kadri walivyozidi kusonga ndivyo
giza lilivyozidi kubisha hodi na kuifunika ardhi gubigubi.
Gambo alizidisha kasi na kuziambua nyayo zake
kiba akibandika kiba akibandua kuelekea asikokujua.
Kijibaridi kikali kilikuwa kimeanza kuwanyemelea wawili
hao na kumpepeta Gambo na kuvifanya vinywa vyake
kutetemeka huku meno yake yakiumana na kutoa sauti
ya mtataliko kama nyasi kavu.
Ghafla, Kitaka aliyekuwa hatua chache mbele ya
Gambo, alisimama na kwa ishara ya mkono akamwashiria
Gambo akaze mwendo. Gambo alipomfikia, Kitaka
alimshika mkono na pamoja walisonga kando ya kijia
hicho wakaanza kunongonezeana kwa sauti za chini.
Baada ya kushauriana kwa muda mfupi, wawili hao
walifululiza hadi kwenye kisitu kilichokuwa hapo karibu.
Hapo walikutana na kundi fulani la vijana lililokuwa
likiwasubiri. Punde si punde, safari ya kazi ikaanza.
Walingoa nanga kuelekea mjini Rimba, bila shaka kurina
asali kwenye jumba moja la kifahari; kuenda kuvuna
wasichokipanda. Gambo alikuwa amepewa kazi yake ya
kukamilisha. Shughuli yote pale ilimtegemea yeye.
Giza totoro lilitanda na kimya kikatawala
kote. Hakuna sauti ya kiumbe chochote iliyosikika
12
isipokuwa mikoroto ya vyura kutoka kijito Tala. Gambo
alinyapanyapa taratibu hadi dirishani, akiwa amemakinika
sana asije akawaamsha waliolala au kuwatahadharisha
mbwa wakali.Woga ulimvamia akaanza kuwa na wasiwasi
kama mwasi huku akijikaza ili atimize azimio lake.
Polepole alinyatia dirisha lile, akatanguliza kichwa
na mara moja akajisukuma ndani ya nyumba ile. Bila
shaka wenyeji walikuwa wamelala fofofo bila ufahamu
wowote wa yale yaliyojiri.
Bawabu naye pale langoni kwenye chumba chake
alikuwa katika harakati za kujitayarishia malazi baada ya
kuhakikisha kuwa kila kitu kilikuwa shwari bila shari.
13
Wiuwiuwiuwu...!!! Sauti ya kingora ilipasua ukiwa
usiku ule na kufanya kila kiumbe kugutuka kutoka
usingizini. Mbwa walibweka ovyo kwa sauti za juu kwa
majibizano kana kwamba walikuwa katika tamasha za
muziki. Sauti za kike zilisikika zikipiga kamsa, huku watu
wakikimbia bila mwelekeo mahususi.
Gambo alianza kujuta, moyo ukaanza kumpapa na
kudunda dududu ungedhani ulitaka kutalikiana na mwili
wake. Damu ilimganda mishipani na nguvu zikamtenguka
mwilini huku nywele zake zikitimka timtim kichwani.
Aliona kifo kikimkodolea macho. Taa ziliwashwa
ndani ya nyumba ile, huku milio ya risasi ikisikika kule
nje, ishara tosha ya makabiliano kati ya magaidi na bila
shaka polisi.
Mlango ulifunguliwa kwa fujo na mbele yake
Gambo, alisimama mwanamume mwenye misulitinginya.
Alikuwa mrefu pia mnene na kivuli chake alichokitazama
wakati huo wote Gambo kilidhihirisha vyema umbo lile.
Wewe ni nani? Unafanya nini hapa? Nani
alikutuma? alifoka maswali bila kusita.
Gambo alilaani usiku ule. Alimlaani Kitaka pia
kwa kumshawishi ajitumbukize kwenye jehanamu ile
aliyoshuhudia barabara kabisa. Kweli, msiba wa kujitakia
hauna kilio.
Alibebwa juujuu kama unyoya na kutupwa chini pu.
Mbele ya umati wa watu uliokuwa umekusanyika pale
nje.
Kila mmoja aliyemtazama alikitikisa kichwa kwa
14
mshangao. Hakuna aliyejua namna ambavyo Gambo
aliingia mle chumbani. Wakati huo wote Gambo
aliukumbatia ule mkoba wake aliouenzi kama pigo la
moyo wake, jambo ambalo liliwashangaza watu zaidi.
Choma! Moto! Mwizi choma! ndizo sauti
zilizohanikiza hewani ghafla baada ya kile kimya kifupi
cha mshangao.
Gambo alilia kwi kwi kwi huku akiomba msamaha
lakini nani amsikie? Mafuta aina ya petroli yaliletwa na
mara moja akamwagiwa kwenye mwili akaloa.
Mauti yalimnyemelea Gambo. Mauti katili yasiyo
na huruma. Moto ulipowashwa ili ateketezwe,Gambo
alikikumbuka kile kibwagizo alichokipenda kukariri na
kwa sauti ya juu na unyenyekevu alikikariri huku mkono
wake wa kushoto ukiteketea kwenye moto.
Unyama ulioje! Aliukumbatia mkoba wake,
akayafumba macho yake na kunena, Mimi mtoto tu!
Maskini mimi, nafsi yangu yanitatiza, lakini mahitaji
yanizidi, akapoteza fahamu. Watu walishangaa kuyasikia
maneno yale.
15
Sura ya pili
Saa mbili kamili usingizi ulimpaa Gambo. Akaenda
miayo mara kadhaa huku akijinyoosha na kujigaragaza
kitandani, kisha akayapangusa macho yake ya chawa
yaliyojaa matongo na kuanza kuyapepesa kila sehemu
kwenye dari. Hakuwa na haja tena na usingizi wa pono ila
uchovu wa siku za mwambo alizoziita maisha ya ahera.
Alijihisi mwili ukiwa dhaifu huku tumbo likinguruma bila
shaka likidai haki yake. Mara moja akakumbuka hakuwa
amekula chajio wala kisebeho.
Aliazimia kutoka kitandani atafute chakula. Kabla ya
kushuka kutoka kitandani, maneno ya marehemu mama
yake, Bi Nusura, yalijikariri akilini mwake, Mwanangu,
mkumbuke Mungu siku zote, kwenye raha na kwenye
shida, niwepo au nisiwepo. Siku njema na maisha mema
hufanikishwa na Mungu. Yakumbuke maneno haya
wakati wote.
Papo hapo, Gambo aliyafumba macho yake,
akainuka taratibu, akapiga magoti kitandani na kupiga
Bismillahi:
16
Baba yetu Mwumba mbingu na nchi.
Mwenye kuneemesha neema za kila aina
Nihurumie mimi mwanao.
Daima niepushe na maovu.
Mayatima watimizie mahitaji yao.... Amina.
Alijizoazoa kitepetevu kutoka kitandani na kukimbilia
maji yaliyokuwa kwenye buli. Yalikuwa yamekanzwa.
Akayamimina kwenye bilauri, akayatia asali kisha
akayanywa taratibu huku ameketi juu ya kile kitanda.
Baadaye alifuliliza hadi nje ili kubarizi. Jua lililokuwa
limechomoza lilimkaribisha kwa mikono miwili. Liliungwa
mkono na upepo mwanana uliokuwa ukivuma kutoka
ufuoni mwa bahari. Alihisi faraja moyoni na tumaini la
siku njema.
Aliketi juu ya jiwe, akaokota vijiwe vidogo mkononi
na kuanza kulenga ndege wadogo waliopita karibu
naye. Kweli aliyafurahia yale mandhari yaliyopendeza
na kumfanya asahau matatizo aliyokuwa ameyapitia
kwa muda. Alipotazama nyuma, hakusita kutabasamu
alipoliona lile jengo kubwa la kifahari ambalo sasa alijua
ni nyumbani. Asingeteseka tena akilala kwenye vibanda.
Kuna jambo moja hakuwa daima akitamani
kukumbuka, ile siku aliyoletwa hapo hapo katika jengo
hilo akajitoma ndani kupitia dirishani ili awafungulie
wale majambazi marafikize Kitaka. Aliutazama mkono
wake wa kushoto ulivyojaa mabaka na makovu akahisi
17
uchungu moyoni mwake. Alijua fika kuwa hayo yote
yasingekuja kutokea isingekuwa kwa uwepo wa ukatili
na ubinafsi wa binadamu.
Kwa kweli kifo cha wazazi wake kilikuwa pigo kubwa
kwake. Kilimtatizia ndoto zake kwa kumkatizia masomo
yake akiwa angali mdogo. Kila mara alipokumbuka tukio
hilo, alikilaani kile kitendo vikali.
Wakati ule ule alizama kwenye lindi la mawazo.
Aliona bayana jinsi mkasa huo ulivyotokea. Hayawani
wanane waliojihami vilivyo walivyowavamia na kuacha
hadithi ya kutambwa kwa vizazi vya miaka na mikaka.
Yalikuwa mambo yaliyojiandika akilini mwa Gambo kwa
wino ambao kamwe usingefutika.
Kwa kweli aliikumbuka vizuri sana siku hiyo kana
kwamba ilikuwa jana tu. Saa moja asubuhi, Alhamisi
tarehe 27, Disemba 1995. Ilikuwa baada ya staftahi baba
yake alipoufungua mlango wa chumba cha maegesho,
akawasha gari lake na kurudi chumbani kuwaaga Gambo
na mama yake. Wakati huo Gambo alikuwa mwanafunzi
wa darasa la tatu lakini alikuwa kwenye likizo. Baba yake,
bwana Mambo, alikuwa mwajiriwa katika Shirika la Reli
hivyo basi asubuhi hiyo alikuwa angoe nanga kuelekea
kazini.
Ghafla mlango ulifunguliwa kwa kishindo nusura
uvunjike. Bwana Mambo akaangushwa chini pu kama
gunia la viazi. Wavamizi walikuwa wamebana nyuso
zao kwa mabarakoa wasije wakatambuliwa. Mama yake
Gambo alipoona yaliyotokea, alimvuta Gambo upesi na
18
kukimbilia mlango wa jikoni. Aliufungua upesiupesi. Ghafla
alivutwa nyuma na yule mvamizi. Alimwachilia Gambo na
kumhimiza akimbilie nje. Gambo alisikia mifyatuko kutoka
mle nyumbani. Alitaka kurudi mle nyumbani lakini miguu
ilikataa. Alizidi kuchana mbuga bila hata kujua alikokuwa
akienda.
Gambo alipiga milundi kwa hatua si haba asubuhi ile.
Alijua alikotoka lakini alikoenda hakujua.Mara kwa mara
mawazo yalimshika miguu, akajikuta akisitisha mwendo
na kusimama bila sababu mahsusi. Mawazo yalimsonga,
akajumlisha akaondoa lakini yote hayo yakawa bure si
kitu. Machozi yakamtiririka njia nne nne mithili ya ngamia.
Kweli asingeweza kuwaona wazazi wake tena? Aliganda
kama kigaga pale kwenye kile kijia, akivuta taswira ile,
sinema ya ajabu aliyokuwa ameshuhudia asubuhi ile.
Aende wapi? Afanye nini? Ndiyo maswali yaliyoiteka
nyara akili yake wakati ule. Alifuta machozi kwa ukosi wa
shati lake na kuyapangusa makamasi kwa viganja vyake.
Alipotazama nyuma, aliona wingu la moshi uliokuwa
mweusi ti ti ti, likihanikiza hewani na kutanda kote huku
likibadili anga na kuifanya kuwa nyeusi. Alielewa fika
kuwa hapakosi moto popote palipo na moshi. Alijua bila
shaka kuwa kulikuwa na jambo lililoendelea sehemu ile.
Niende au nisiende? alijiuliza Gambo. Ndiyo,
nitakimbia pale nijionee mwenyewe. La, sitaenda.
19
Nafsi ilimtatiza Gambo, akaganda pale pale,
hakujua asonge mbele au arudi nyuma. Alihisi ndege
mbaya alikuwa ametua kijijini pao siku hiyo. Mibweko
ya mbwa ilishika usukani. Mbwa walibweka ovyo, kwa
majibizano kana kwamba walikuwa wakikariri shairi la
ngonjera. Jogoo waliwika kwa hali ambayo haikuwa ya
kawaida. Kuku walikokoneka. Ngombe nao walisikika
wakiroroma ovyo ni kama walikuwa wamenusa harufu ya
20
simba.
Punde tu, sauti za kike zikatanda kote, ukemi ukitokea
kila pembe. Gambo alijipata akitetemeka kama mgonjwa
wa malaria. Alipojitazama aligundua kuwa suruali yake
ilikuwa imeloa chepechepe kutokana na kujiendea haja
ndogo. Woga aliouhisi haukumpa ruhusa atafute chemba
aende haja. Hakuweza kuvistahimili vishindo vya tumbo
lake. Basi pale tu aliposimama pakawa ndio msala wake,
kwa haja kubwa na ndogo. Pumzi zilimwenda mbio,
akatamani ardhi ipasuke na immeze akiwa hai.
Aliona ni kama siku yake ya kiama ilikuwa imewadia.
Taratibu alijipata akianguka ardhini bila kishindo wala
pupa. Aliketi chini akakiinamisha kichwa chake, tayari
kumpokea Izraili. Dakika chache baadaye, alikumbuka
nasaha za mama yake kuhusu maombi. Mara moja
alijinyanyua akapiga magoti akasema sala:
Mungu wewe ni mkubwa
Nipe nguvu za kustahimili haya yote
Ikiwa nitakufa, ilaze roho yangu pahali pema
Lakini Mungu sitaki kufa
Mama yangu aliniambia
wewe unafanikisha maisha mema...
21
Akiwa bado katika ile hali ya kuomba, alisikia
sauti nzito za watu zilizojaa hamaki, wakija upande wake.
Hakuwa na wakati wa kukamilisha sala yake bali alijua
lazima atafute mbinu za kuepuka maafa ambayo aliona
yakimkaribia.
Watu wale walikuwa wakiimba nyimbo, na
ukidhani ni nyimbo za kumsifu Mungu basi utakuwa
umekosea. Gambo alijua asingekimbia popote pa
kijificha, mdogo alivyokuwa alikuwa kama tone moja
22
akilinganishwa na lile kundi lililokuwa likijongea.
Yaloloeee... mmbaa... mmbaa... yaloole...
Akiliimba... mababantuu... yaloloee yaloloee”
“Kilaki ndikuuo... onyekilaakii...
Gambo alisikiliza kwa makini na kwa ndege mzuri,
aliweza kuelewa ujumbe wa lugha iliyotumika kwenye
huo wimbo.
Bila kupoteza wasaa, alisuka mikakati ya
kujinusuru iwapo taabu ingekuja upande wake. Aliamua
kuimba pia ili ajitambulishe, watu wale wamfikiapo wasije
wakamwangamiza.
“Ilaki Gambo... mwana weno Yaloole...
Ilaki Gambo... Wenyomba Medoo...
Nusura ni mamaa...
Kwenye wimbo wake alijitambulisha kuwa yeye
aliitwa Gambo mwana wao, wa nyumba yao. Mama
yake aliitwa Nusura. Kadri walivyozidi kumkaribia ndivyo
alivyozidi kupaza sauti ingawa kwa shida sana kwa
sababu sauti ilikuwa inampwelea baada ya kulia kwingi.
“Ilaki Gambooo... mwana weno Yaloole..
“Ilaki Gambooo. Wenyomba Medoo...
Nusura ni maamaa.
Alijikaza kupaza sauti huku akipukutikwa na
machozi pukupuku. Yakini, Gambo alisononeka. Sauti
yake ikadhoofika hadi hakuweza kuimba tena. Hakujua
wale watu walishapata barabara ujumbe wake.
Nusura avamiwe na usingizi pale alipoketi.
Aligutuka akikabwa mkono ghafla na mtu asiyemjua. Mtu
23
huyo alikuwa amevaa nguo zilizotangaza wazi utamaduni
wake.
Tilitili mwana Nusura, Wenyomba medo,
akayai Gambo tilitili mwana.
Mtu yule alimweleza Gambo alipotaka kupiga
kamsa.
Alikuwa na kusudi la kumhimiza Gambo anyamaze
asilie kwani alikwisha kusikia kuwa Gambo alikuwa wa
nyumba yake yaani mwana wake.
Alijitambulisha kwa sauti nzito yenye mkwaruzo,
Jina langu ni Kombo. Mimi ni ami yako wa kuumeni.
Gambo aliinuka na Kombo akamnyanyua pamoja
wakaungana na kile kikosi kilichokuwa kikiimba. Katika
hali ile, Gambo alijisawazisha kwenye bega la Kombo,
akakiinamisha kichwa na kukilaza juu ya kichwa chake
mwanamume yule mwenye miraba minne. Polepole
usingizi ulimnyemelea na kumsafirisha safari ndefu katika
ulimwengu wa ndoto.
24
Sura ya tatu
Ngo... ngo... ngo..., mlango ulibishwa.
Karibu ndani, Gambo alimkaribisha mgeni,
akiwa katika jumba la kifahari. Kwenye chumba chake
cha kulala palisheheni samani kadhaa na vyombo vya
kielektroniki. Siku hiyo, mwendo wa saa mbili asubuhi,
alimpokea mgeni aliyemletea habari iliyofurahisha mtima
wake. Ilihusu matokeo yake ya mtihani wa shule ya upili.
Alikuwa ameongoza kote nchini na mgeni yule alikuwa
mwanahabari aliyekuja kumhoji Gambo.
Gambo alimtazama kwa sekunde kadhaa.
Kadri alivyomtazama ndipo akili zake zilivyoendelea
kumshawishi kuwa hakuwa mtu aliyemfahamu. Alifumbua
kinywa na kumwuliza, Nikusaidie vipi kaka?
Mgeni yule alisafisha koo na kujitambulisha, Mimi
ni mwanahabari. Mm... mi... mimi ni ripota wa gazeti la
Anga Pevu na jina langu ni Azandea.
Gambo alimnyooshea mkono kwa heshima,
Karibu sana.
Asante sana,Azandea alijibu.
Kuna jambo gani? Gambo aliuliza, wasiwasi
ukianza kumnyemelea moyoni.
Usifanye wasiwasi. Tulipokea habari kuwa
25
wewe ndiwe mwanafunzi bora nchini katika mtihani wa
sekondari, alimtuliza huku akiitayarisha kamera yake.
Gambo alitabasamu, Namshukuru Maulana kwa
kunijalia ushindi huo.
Ungependa kusomea taaluma gani katika chuo
kikuu? Azandea alimwuliza Gambo.
Siku zote nilipokuwa nikisoma nilitaka kuwa
mhandisi. Hata hivyo, uwakili utanifaa, Gambo alijibu
kwa ukakamavu na uchangamfu.
Azendea alisita kidogo huku akimkazia jicho la
upekuzi. Mbona basi unaamua kuwa wakili?
Gambo alicheka kwa sauti kisha akatoa kauli
yake, Wewe wajua kuwa mwana wa mhunzi asiposana
hufukuta?
Alipogutuka, alijipata msituni. Alikuwa peke yake.
Hakukuwa na mtu hata mmoja.
Aliishi kule msituni kwa siku kadhaa, matunda ya
mwituni yakawa ndicho chakula chake. Wanyamapori
wakawa marafiki zake. Kila wakati alipoketi chini,
alifanya kazi ile aliyoipenda sana, ukipenda utasema
ilikuwa talanta yake, yaani kutunga mashairi. Hayakuwa
ya kubuni tu bali maudhui ama ujumbe ulikuwa ukweli
kuhusiana na maisha yake.
Shairi lake la kwanza, lilihusu mkasa ule wa kwanza
kuwahi kutokea maishani mwake, jambo lililomtia donda
ndugu kwenye moyo wake. Nalo ni hili:
Balaa wataka nini, tafadhali nelezeni,
Ukiwa menyemelea, hofu moyoni mejaa.
26
Haishindwi hata kamwe, taaabu kuingilia.
Moyo wangu huna furaha, maisha kanigeuka
Nafsi yanitatiza lakini mahitaji yanizidi.
Malenga huyu mchanga alieleza hisia zake
barabara kupitia shairi la pili. Hakujua mbona yaliyomsibu
yakatokea, alibaki kukisia tu huku akitapatapa kwenye
sababu na vijisababu.
Imani kwangu kanipaa, siamini neno utu,
Katoweka na kupaa, ingawa hewani haipo,
Nani nimwite jirani, ya moyoni nimpashe,
Yalo nichoma Imani, utumwani kunitweka.
Menizimia taa, ilowashwa na waasisi,
manzilini kaniondoa, kiokote nichakure.
Katu siyapendi, nifanyayo aushini
Nafsi yanitatiza, lakini mahitaji yanizidi.
Gambo alikolea kwenye utunzi, ingawa hakuelewa
ulikuwa utunzi. La muhimu kwake lilikuwa kujiliwaza,
kupitisha ujumbe na kupitisha wakati.
Siku moja alipokuwa katika pitapita zake, aliona gari
aina ya lori, lililokuwa la kubeba makaa. Basi alilikaribia,
akawapata wenyewe wamepakia m akaa na walikuwa
katika harakati za kubadilisha mavazi. Mara moja Gambo
alijua fika kuwa chelewa chelewa utakuta mwana si wako.
Basi alichupia lori kama askari wa rais, akajituliza
mara moja huku akiomba kimoyomoyo asije mtu
akamwona. Alikuwa na nia na matumaini kuwa gari
lile lingemfikisha kwenye barabara kuu. Kutoka hapo
27
ambapo angepata dira aweze kurudi kwao.
Saa thenashara kamili, lori lile liliwasili mtaani
Rabeki. Gambo akashukuru Maulana alipoona
m a g u rudumu yamesalimu amri ya dereva na kusimama.
Alishuka taratibu na kuanza kuenda masia kuelekea
kule asikokujua. Huo ukawa ndio mwanzo wa maisha yake
mtaani Rabeki. Ukurasa wa maisha mazuri ukafungwa na
kumfungulia ukurasa wa masaibu kupitia kifo cha wazazi
wake. Kweli, mti mkuu ukigwa wana wa ndege huyumba.
******
Machozi yalimtiririka tiriri, akauangalia mkono wake
tena na akaiangalia ile nyumba kisha akajiambia, Nina
fursa tena, fursa takatifu, fursa ya kuishi kwa raha tena.
Macho yake yalitua kwa mama yake, yaani
yule mama mwenye lile jengo alimoishi Gambo. Ndiye
yule aliyemwokoa kutoka mikononi mwa mauti, usiku
ule ambao angeteketezwa. Kutokana na ule mshororo
alioukariri, yule mama mwokozi aliguswa akawaonya
watu dhidi ya kumwangamiza Gambo.
Alipopoteza fahamu, aliuchukua ule mkoba na ndani
aliyapata mashairi ambayo Gambo alikuwa ameyatunga
pamoja na picha aliyokuwa ameichora ya mama yake
mzazi.
Mashairi yale yalieleza masaibu aliyoyapitia
Gambo baada ya kifo cha mama yake na baba yake.
Hapo ndipo yule mama alipopata maana ya ule mshororo
aliounena Gambo kuwa, Nafsi yangu yanitatiza, lakini
mahitaji yanizidi, kutokana na huruma, aliapa kumchukua
Gambo.
28
Aliyagharamia matibabu yake kisha akamrudisha
shuleni akaendelea na masomo. Gambo alitabasamu,
akainuka upesi, akakimbia na kumkumbatia, huku moyoni
akiwa mwingi wa furaha. Alikuwa amepata fursa ya kuishi
na kutimiza ndoto zake. Fursa takatifu, yaani fursa teule.
29
Sura ya nne
Saa moja kamili ilimpata Gambo kapiga foleni katika
afisi ya kuwasajili wanafunzi wageni shuleni Komboa mjini
Taji. Alikuwa ndiye wa kwanza na wa mwisho kwenye
foleni. Ilikuwa foleni ndefu mno kwani hakusita kutamani
kujiona kwenye dawati; kaketi kitako akimsubiri mwalimu
au hata akiendelea na kipindi cha somo lolote.
Kwa kweli Gambo alikuwa amefika shuleni
mapema, huku akiwatangulia wote; walimu, wanafunzi
wenzake na hata mwalimu mkuu, ambaye kwake Gambo
alikuwa mgeni wake.
Akiwa katika hali ile, Gambo alivuta taswira.
Alikumbuka barabara siku ile aliyoota ndoto iliyomwacha
na matamanio si haba. Alikumbuka mbisho wa
mwanahabari, maamkizi, kisha maswali ya udadisi.
Alikula yamini kuwa lazima maishani mwake angekuwa
wakili, na si wakili tu bali wakili bora, mwanasheria wa
kutajika, hakutaka kujifunga kwenye sehemu mahususi.
Jinsi angetimiza hilo, lilisalia kuwa kitendawili ambacho
ni yeye tu aliyekuwa na jibu lake.
Asalaam aleikum, aligutuliwa kutoka katika
pilikapilika zake za kimawazo.
30
Aleikum salaam mwalimu, alijibu huku
amejiinamia kwa tahayuri na uoga.
Gambo alijua fika kuwa yule aliyemsalimia lazima
ndiye aliyekuwa mwalimu mkuu. Daima alielewa kuwa
yeyote aliyeonekana kwenye afisi ya walimu alikuwa
mwalimu bila shaka.Hakuuinua uso wake kumtazama
yule mtu aliyemsalimu kwani alichelea kuitwa mtovu wa
31
nidhamu. Alitaka kujilimbikizia sifa sufufu kuwa alikuwa
mtoto mzuri mwenye heshima.
Ha ha ha…, Kicheko cha radi kilifuatia.
Kicheko kile kilimshtua Gambo na kumfanya ainue
uso wake upesi kumtazama aliyesimama mbele yake.
Mara moja macho yake yakatua kwenye maandishi ya
kofia aliyoivaa mtu yule.
BMW security alisoma kwa sauti huku akiacha
kinywa achama kiasi cha kukaribisha nzi kufanya makazi
yao humo.
Salaale! Aliyemwita mwalimu hakuwa mwalimu
bali bawabu wa shule aliyekuwa amekuja kufungua afisi
ya mwalimu mkuu, ilivyokuwa desturi yake.
Huku akiwa ameshika kicha cha funguo mkononi,
bawabu yule alimnyooshea mkono Gambo akimtaka
salamu.
Asante mwanangu, karibu, alimsemeza Gambo.
Ulinipandisha madaraka na kuniita mwalimu,
asante. Kwa kweli nilipokuwa mtoto mdogo umri wako,
nilitamani sana kuwa mwalimu pindi nitimiapo umri
mwafaka. Lakini hayo hayakuwezekana. Mwanangu
usome kwa bidii utimize ndoto zako. Shule ni kiwanda
chenye malighafi ya thamani, kinachotengeneza
wanaume na wanawake wenye thamani kutokana na
watoto sampuli yenu. Hivi leo ninaishi.
Ninaomba kujua baba mbona hukutimiza ndoto
yako na kuwa mwalimu, Gambo alidakiza usemi wa
yule bawabu, kwa swali ambalo wakati wote huo alikuwa
akilikariri tamulini mwake.
32
Piip! Piip! Honi ya gari kwenye lango kuu ilisikika.
Hapo bawabu hakuwa na budi kuondoka upesi pasi na
maagano. Kwa hivyo Gambo akabaki bila jibu la swali lile
alilokuwa amemwuliza bawabu. Ilibidi aanze kukisia na
kujijazia dondoo lile lisilokuwa lake la kutafutia jibu.
Lazima mzee huyu kapitia maisha kama yangu.
Huenda amepitia unyama na ukosefu wa utu nilivyopitia
mimi, alijishawishi Gambo.
Haidhuru, yaliyopita si ndwele. Sisi wanasheria
shupavu hatuishi jana, tunaishi leo na kesho, alijisemea
Gambo huku akichanua tabasamu mufti.
Ungalimwona ungalidhani Gambo kavamiwa na
kichaa. Alisimama kutoka pale alipoketi na kuyaruhusu
macho yake kuzuru kila pembe na mandhari ya shule
ile. Aliweza kuwaona wanafunzi waliokuwa wakiwasili
madarasani mmoja mmoja.
Punde si punde, Mwalimu mkuu aliwasili. Gambo
akangamua kuwa wakati aliokuwa ameuongoja kwa
hamu na dukuduku kuu hatimaye uliwadia. Gambo
hakuwa mwanafunzi mgeni tu, bali pia alikuwa mgeni wa
maisha ya shule ya mjini, iliyosheheni wanafunzi kutoka
familia za walalahai pekee.
Hakujua ni vipi angeyamudu maisha ya pale hasa
maisha ya shule ya bweni. Haikuwahi kumjia hata kwa
ndoto tu kuwa siku moja yeye Gambo, angejikuta kwenye
shule ya bweni. Akawa na hisia tatanishi, za uoga na
furaha, zote zilimvamia na kuiteka nyara nafsi yake.
Kwa wakati ule hayo ndiyo yaliyomtatiza Gambo,
hakujua kuwa kuna makuu yaliyomsubiri, yaliyomkodolea
macho ya kejeli ingawa kwa siri.
33
Sura ya tano
Mwanafunzi wa kwanza aingie, mwalimu mkuu
alitoa amri.
Wasiwasi wa aina fulani ulimnyemelea Gambo.
Woga ukamvaa na ghafla akahisi haja ya kwenda pembeni
angalau kwa haja ndogo. Hayo hayangewezekana kwa
wakati ule kwani alikuwa mhitaji mkuu wa hisani ile, hivyo
asingetaka kukosea.
Sisi wanasheria hodari huwa hatuogopi, Gambo
alijisemea kimoyomoyo, akatabasamu kisha akapiga
hatua kuelekea ofisini. Mahojiano machache baina ya
Gambo na mwalimu mkuu yalifuata.
Mwalimu mkuu alimkaribisha na kumwamkia
Gambo huku akiiweka kalamu mezani, Hujambo bwana
mdogo?
Gambo aliitikia kwa unyenyekevu, Sijambo
mwalimu.
Jina lako ni Gambo, sivyo? Mwalimu mkuu aliulza
na kutabasamu kama mzazi kwa mwanawe.
Gambo aliingiwa na mshangao na mshtuko,
Ndivyo mwalimu.
Mwalimu mkuu aliona mshtuko wa Gambo akataka
kumtuliza, Usiogope, nilikuwa nikikusubiri. Ni mimi
34
niliyekutumia mwaliko wa kujiunga na shule hii.
Gambo alishusha pumzi nusura ampigie Mwalimu
mkuu magoti kwa kumshukuru, Asante mwalimu.
Niambie jina lako na majina ya wazazi wako pia,
mwalimu mkuu alimwambia.
Jina langu ni Gambo Mtume, baba ni Mtume na
mama ni Nusura, Gambo alijibu kwa ufasaha.
Mwalimu mkuu aliinua macho na kumtazama
Gambo kwa muda kisha akamwuliza, Nipe majina yote
mawili ya kila mzazi.
35
Gambo alifungua mdomo ukabaki hivyo kwa
muda. Alimeza funda la mate. Hakuna neno lililomtoka.
Machozi yalianza kumlengalenga machoni. Baada ya
kuhangaikahangaika sauti hafifu ilimtoka, Hakika sijui
majina mengine ya wazazi wangu. Wakati huo nilikuwa
mdogo sana.
Ilikuwa ni zamu ya Mwalimu mkuu kupigwa na
butwaa. Alijitahidi kutoonyesha mshangao. Alikuwa
hajawahi kumwona mtoto anayejiunga na shule ilhali
hakuwajua wazazi wake kwa majina yao. Kwa hivyo
alijipata tu akisema, Aa aa... aa, hakuna neno bwana
mdogo.
Usaili ule ulipokamilika, Gambo alisajiliwa katika
darasa la nne. Ingawa hakuwa amekamilisha masomo
ya darasa la tatu, umri wake usingemruhusu kujiunga na
darasa hilo. Hata pale darasa la nne, ilichukua mkondo
wa pasipo budi hubidi.
Bi. Kesi alibisha langoni pa mwalimu mkuu na
kumpokea Gambo ili ampeleke darasani. Njiani Gambo
alitazama huku na kule, hisia mbalimbali ikimwingia
akilini na moyoni. Alihisi ni kana kwamba kila mmoja
katika maeneo yale aliyajua na kuyasoma maisha yake
barabara. Hata hivyo alipiga moyo wake konde na
kuandamana na Bi. Kesi hadi darasani.
Macho ya kila mwanafunzi pale darasani yaliinuliwa
na kutua kwake Gambo. Nyuso zao zilisheheni alama za
mshangao. Gambo hakujua aikabili vipi hali ile. Alijihisi na
kusadiki kuwa kuku mgeni hakosi kamba mguuni. Umbo
lake kubwa kuliko wote darasani, halikumruhusu aketi
kwa starehe kwenye dawati lile dogo. Kimo chake kirefu
36
nacho kiliusaliti uwepo wake pale. Hata ingawa aliketi
nyuma kabisa ya wenzake, kila aliyeingia mle darasani
alimwona wa kwanza.
Gambo aliiona siku hiyo kama siku iliyokuwa ndefu
zaidi maishani mwake. Ilijikokota huku Gambo akiilaani
kila sekunde. Hatimaye alisalimu amri na kujiambia
kuwa katu asingeyaruhusu maumbile kusitisha ari yake
ya masomo bali angezidi kujikakamua. Alimeza mrututu
na kujikumbusha kuwa masomo ndiyo iliyokuwa njia ya
pekee ya kujikomboa maishani.
Maskini Gambo akawa ndiye chanzo cha kila
utani mle darasani. Wengi walimkwepa wala hakuna
aliyemtakia urafiki. Inakuwaje baba kuja kusoma na
watoto wake! alimsikia mwanafunzi mmoja akilalamika
kwa mwenziwe.
Baba yupi? aliulizwa na mwezake.
Yule twiga karefu, alijibiwa.
Karefu ni baba wa watoto? Ana mke? Ana watoto
wangapi?
Mimi sitaki kujua ana watoto wangapi. Ninaenda
kumwambia baba yangu anipeleke katika shule
nyingine...
Hazikupita siku tatu. Gambo hakuwaona watoto
wale tena. Waliobaki walijitenga naye kama mgonjwa
wa ukoma anavyotengwa kwa ajili ya matibabu. Gambo
alibaki wakati wote amejiinamia kama kondoo.
Hata hivyo, alijua kuwa hayo yote yangeisha ikiwa
angeelea kwenye bahari ya masomo kwa kuwapiku wale
wenzake.
37
Baada ya mwezi mmoja mtihani ulifanywa. Gambo
alijipata miongoni mwa wanafunzi watano wa mwisho.
Jambo hili lilimwatua moyo na kumtonesha kidonda
ambacho kamwe hakutaka kutoneshwa. Akahisi kama
askarijeshi aliyeshindwa kudhibiti usalama katika ghasia
za waandamanaji. Aliona kuwa amejisaliti na kumsaliti
mfadhili wake.
38
Sura ya sita
Masaibu ya Gambo hayakufika kikomo pale katika
shule ya msingi. Umri wake ulimfanya kujiona kama
mbwamwitu miongoni mwa wanakondoo pale shuleni.
Jambo hili lilimtia tabasamu kila alipolikumbuka hasa
baada ya kuhitimu masomo ya msingi. Mambo mengine
yalimsubiri katika shule ya sekondari na labda chuo kikuu.
Kitu muhimu kinachobadilisha mengi ni wakati.
Wakati hufanya marafiki kukosana au maadui kupendana.
Wakati hufanya aliyekuwa chini akawa juu na aliyekuwa
juu akawa chini. Wakati huo ulifanya Gambo akajikuta
amehitimu elimu ya shule za msingi. Alikumbuka mambo
yalivyokuwa mwanzo hadi wanafunzi wote walivyokuja
kumpenda na kumtegemea pale shuleni. Aliwashauri
wengi na kuwatia moyo waliotaka kukata tamaa.
Alikumbuka alivyoteuliwa kuwa kiranja wa
ushauri nasaha. Alijua matatizo ya wenzake na namna
ya kuyatatua. Waliokosana aliweza kuwapatanisha.
Aliona nyota yake ya kuwa mwanasheria ikianza kupata
mwanya katika mawingu meusi yaliyokuwa yameifunika
hapo awali. Kwa hivyo, alipotangazwa miongoni mwa
39
wanafunzi wa tano bora walioongoza katika mtihani wa
kitaifa wa shule za msingi, alishangilia sana.
Mdhamini wake alimhakikishia kuwa angeendelea
na masomo katika shule ya upili. Kwa hivyo furaha
isiyokuwa na kifani ilimfurika akipokezwa barua na
mwalimu mkuu. Ilikuwa barua ya kumwalika kujiunga na
shule ya kitaifa Bingwa School.
40
Baada ya masomo katika Shule ya Komboa, Gambo
alijiunga na Bingwa School. Hii ilikuwa shule ya kitengo
cha kitaifa. Hivyo basi kila mwanafunzi aliyesajiliwa
shuleni humo, alikuwa yule gwiji aliyefuzu vyema kutoka
jimbo lake. Jambo hili la kuwakutanisha mabingwa wa
masomo katika shule moja, lilileta ushindani mkali wa
kimasomo. Kila mmoja alijikaza kisabuni ili dau lake la
ushindi lielekee kwake. Lakini ilivyo desturi, kila ushindani
una mshindi na mshinde.
Baada ya siku chache Shuleni Bingwa, kuna jambo
lililombainikia wazi Gambo. Lilimtia jakamoyo na pia
kumtia msururu wa mawazo. Hakujua angelitatua vipi au
mahusiano yake yangekuwa vipi.
Kwani kila sehemu ni balaa, alijiambia. Hata
maisha yote balaa tupu tu? aliendelea kujiuliza.
Alisimama kimya na kutazama nje kupitia lile
dirisha la bwalo. Katika hali ile, aliyapitisha macho yake
kila pembe hasa ngambo ya pale alipokuwa. Mara
yakatua kwenye Milima ya Tutu. Milima miwili iliyoinuka
na kuacha upenyu mwembamba katikati. Hakika milima
ile ilitoa umbo la maziwa ya mama kama yalivyo kifuani.
Gambo alipoipata picha ile, alijipata akiangua
kicheko. Kweli dunia ina vituko, alijisemea. Angalau
kicheko kile kilimtoa, kwa muda, katika ulimwengu
wa mawazo. Aliondoka pale dirishani, akapiga hatua
kinyumenyume. Aliufungua mlango, akavua viatu
akaingia. Aliufunga mlango taratibu. Alipiga magoti juu ya
ule mkeka na kupiga dua.
Ilikuwa ni Ijumaa jioni. Alikuwa akifungua sala au
41
ibada yake. Angeabudu hadi Jumamosi jioni. Mdhamini
wake alikuwa ni Mwaadiventisti. Huo ndio uliokuwa
utaratibu wa ibada yao.
Gambo alikuwa sasa chumbani peke yake. Hakuwa
na mwingine. Hivyo akawa ndiye kasisi, shemasi na
mshiriki kwa wakati mmoja. Jambo hili ndilo lililofanya
kutengwa kwake na wenzake shuleni humo. Naye
alilichukulia kwa uzito huku likimkera sana. Alijipata
akibaguliwa na wenzake na hata baadhi ya walimu.
Walipokuwa katika majadiliano akashikilia msimamo
fulani ilisemekana ni kwa sababu ya dini yake. Eti achana
na huyu mdini. Aliona jambo hili likimnyima nafasi ya
kujinoa makali ya kushindana na wenzake. Je, ndoto
yake ya kuwa mwanasheria shupavu ingekamilika vipi
katika Bingwa School?
Nani bora mbele ya Muumba? Siku zote alijiuliza.
Siku hii aliapa kufika kikomo cha utesi wake. Mara
moja wazo likamjia na akasuka mikakati.
Nimwandikie mama yangu barua nimweleze
yanayonisumbua, alijinenea.
La, nimwombe anitafutie shule tofauti nijiunge
huko, alijirekebisha.
Basi bila kusita alikimbilia darasani, akaichukua
kalamu, kisha karatasi na kuondoka. Alifululiza hadi
maktabani ambapo alijua angeiandika barua ile bila
yeyote kujua.
42
GAMBO MPOLE,
S.L.P 30,
MALENGONI,
3-3-2018.
Kwa mama Saida mpendwa,
Nina furaha riboribo kama kapera aliyeuasi
ukapera kwa kupata fursa hii ili kukuandikia waraka
huu.
Je, u hali gani? Mimi hapa ni mzima kama
ngarange za mvule. Hofu ni kwako mama. Nina Imani
kuwa nawe u salama salmini.
Madhumuni ya kukuandikia waraka huu mama,
ni kuwasilisha ombi langu la kutaka unitafutie shule
nyingine ili nijiunge huko muhula ujao. Uamuzi huu
nimeufikia baada ya kupata wakati mgumu katika
mahusiano yangu humu shuleni hasa kutokana na
suala la ibada.
Nitashukuru sana iwapo utalikubali ombi langu.
Wako mpendwa
Gambo Mpole.
Alitamatisha barua ile na kumpelekea mwalimu
wake wa somo la dini. Alimwomba aiwasilishe baadaye
kwa mama yake mlezi.
43
******
Baada ya kipindi kile cha likizo, Gambo alijiunga
na shule yake ngeni, Shule ya Upili Maua. Alijawa na
bashasha asubuhi ile alipofikishwa shuleni Maua na
mama yake mlezi. Alijihisi kuwa na matumaini mapya na
imani ya kutimiza ndoto zake ikamrudia.
Baada ya kusajiliwa, ilibidi mama mlezi aondoke.
Gambo aliinuka kutoka kitini alipoketi. Aliubeba mkoba
wake, mama yake akamshika mkono wakaondoka ofisini.
Furaha aliyokuwa nayo Gambo ilipisha machozi
yaliyomtiririka kama mtoto mchanga bila ya kuyazuia.
Mama yake aligeuka akamtazama, naye Gambo
akamtazama, wakatazamana, kisha wakakumbatiana
kwa furaha. Kwake Gambo maisha yakapata maana tena
kupitia yule mama aliyemfaa kwa jua na mvua.
Nitakufaa maradufu siku moja. Hiyo siku yaja,
alijiambia kimoyomoyo huku akimpungia mkono hewani
kwa kumuaga mama yake mlezi. Alikuwa tayari kukitegua
kitendawili cha maisha ...
44
Sura ya saba
Kule shuleni Maua, Gambo alijifunga nira
masomoni, akajikaza kisabuni na kuibuka nambari moja
kila muhula. Shuleni mumo humo alikutana na wanafunzi
wa matabaka mbalimbali. Kunao waliozaliwa katika
familia za walalahai, walalaheri na bila shaka walalahoi.
Hakujali hayo bali alishirikiana nao wote bega kwa bega.
Tayari maisha yalikuwa yamemfundisha kuwa
mkakamavu, mwenye subira, shupavu na mvumilivu.
Alikuwa mwadilifu na mnyenyekevu daima dawamu.
Licha ya hayo, bidii za Gambo masomoni na tabia yake
nzuri vilimpa sifa chungu nzima na mapenzi kutoka kwa
walimu na wanafunzi wenzake.
Kwa vile alikuwa mwanafunzi mwenye bidii na
mwaminifu, alitwikwa jukumu la kuwa kiranja mkuu
wa shule. Ilikuwa dhahiri shahiri kuwa chanda chema
huvikwa pete. Gambo aliongeza jitihada zaidi masomoni
akauma uzi kwelikweli. Hakutaka kuwaudhi au pengine
kuwatamausha waliomwamwini wote. Hivyo basi alijikaza
na kufua dafu katika mitihani yoyote aliyoifanya.
Kijana Gambo hakufanikiwa katika masomo tu bali
pia michezoni. Alipenda kushiriki michezo mbali mbali
45
ikiwemo kandanda, mchezo wa pete na vilelvile mpira wa
kikapu. Alishiriki mashindano ya mipira yaliyoandaliwa
kila mwaka ambapo hakukosa kuisaidia timu yake kufika
kilele cha michezo hiyo yaani kitengo cha kitaifa.
Isitoshe, alishiriki pia mashindano ya tamasha za
muziki za shule za upili. Alikuwa mtunzi na mghani stadi
wa mashairi na kila aliyemsikiliza akiyakariri mashairi
alibaki kinywa wazi kwa kustaajabia umahiri wa Gambo.
Kati ya mechi nyingi alizoshiriki Gambo, ile
aliyoshiriki ya mwisho kabla ya kuaga shule ya upili rasmi
ndiyo ilisalia katika kumbukumbu za waja wengi.
Kinyang’iro na patashika ya mchezo wa kandanda
kilikuwa kimeandaliwa baina ya wachezaji kutoka shule
ya Maua na wachezaji kutoka shule ya Lengo katika uga
wa Nyayo. Mashabiki wa timu hizo mbili walifurika furifuri
uwanjani ili kushuhudia mechi na kushabikia timu hizo,
kila mmoja ile aliyoipendelea, waama, kipendacho moyo
dawa.
Saa tatu kamili kipenga kilipulizwa kuwazindua
wachezaji wawe tayari. Wachezaji wa timu ya Maua
walivalia jezi za rangi ya manjano, kaptura nyeusi na soksi
za rangi ya zambarau.Wale wa timu ya Lengo walivalia
jezi za samawati, kaptura nyeupe na soksi nyekundu.
Bila shaka walionekana watanashati mno.
Wachezaji kutoka timu zote mbili walikusanyika
katikati ya uwanja, wakapewa mawaidha na refa kabla
ya mechi yenyewe kungoa nanga. Halafu wachezaji
walisalimiana kama ishara ya kutakiana heri njema.
Kisha kila timu ilijumuika kwenye gwaride dogo na
46
kuongozwa na nahodha wao kutuma dua ya ushindi kwa
Mungu. Punde si punde kila mchezaji aliitwaa nafasi yake
uwanjani.
Baada ya kuhakikisha kutoka kwa washika bendera
na wachezaji kuwa mambo yalikuwa shwari bila shari,
refa alipuliza filimbi. Mechi ilishika kasi. Mashabiki wa
kila upande waliwatia shime wachezaji wao kwa shangwe
na nyimbo za kuwasifu. Ama kweli ilikuwa vuta nikuvute
kutoka pande zote mbili. Mechi ilisisimua kwelikweli huku
kila mshirika akitaka kuonyesha umahiri wake vilivyo.
Gambo, aliyekuwa golikipa wa wa timu ya Maua,
alijitahidi kwa udi na uvumba kuchupa kama nyani hewani
ili kuipangua mikwaju mikali iliyokuwa ikielekea langoni.
Alikaa ange kila wakati bila kuzubaa kwani hakutaka
kuiaibisha timu yake. Bila shaka timu pinzani ilikuwa na
makali zaidi.
Kufikia kipindi cha mapumziko, hakuna timu
iliyokuwa imefanikiwa kuona lango la timu pinzani.
Wachezaji walienda mapumzikoni huku wakihema kama
mbwa walionusurika kumezwa na chatu. Hadi wakati huo
matokeo yalikuwa sare tasa.
Baada ya robo saa ya mapumziko, kipindi cha lala
salama kilianza. Kila timu ilizidisha juhudi zake maradufu
dhidi ya timu nyingine. Chenga zilipigwa na pasi kutolewa.
Wachezaji wa timu ya Lengo walionekana kuwalemea
wale wa timu ya Maua kwani walizidi kujongea lango la
timu Maua na kufanya kambi huko kwa muda mrefu.
Duru, mchezaji matata sasa wa timu ya Lengo
alimchenga mpinzani wake na kutoweka mbio na mpira
47
huku akiuelekeza langoni kwa mianajili ya kufunga bao.
Hata hivyo, Gambo hakuupatia mpira huo nafasi ya
kukaribia wavu.Alipiga mbizi hewani na kuudaka mara
moja.
Mashabiki wa timu ya Maua walirukaruka kwa
furaha, vifijo hoihoi za Gambo... Gambo... Gambo...
Lengo, lenga tena. Lengo, lenga tena, ndizo
sauti zilizotoka kwenye vinywa vya mashabiki wa timu ya
Lengo angalau kuwahimiza wachezaji wao kujikaza na
kujikakamua zaidi.
Kinyanganyiro kikazua mkondo mpya.
Mashambulizi ya mara kwa mara katika kila lango la timu
zote yakawa ndio mtindo. Mashabiki nao hawakuachwa
nyuma bali walizidi kuwahongera na kuwahimiza
wachezaji wao.
Mnamo dakika ya themanini na tisa, hakuna timu
ambayo ilikuwa imebahatika kuona lango la timu pinzani.
Basi baada ya dakika ya mwisho ya tisini na ushei bila
mafanikio, refa hakuwa na cha msalie mtume wala nabii
ila kuamrisha penalti. Ama kweli, lisilo budi hubidi.
Mchezaji wa timu ya Lengo, aliyejulikana kwa
jina Duru, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipiga penalti.
Kila mwanasoka wa timu yake alionekana kumwamini
sana. Lengo alirudi nyuma hatua kumi. Akaweka mikono
kiunoni. Akatazama lango, akautazama mpira, akaja mbio
na kupiga shuti kali kimo cha twigwa, go go go go go go
go go go... Gambo akachupa na kujipinda kama upinde
na kuudaka mpira na kuganda nao kama smaku.
48
Baada ya majaribio matatu ya penalti hakuna timu
ilikuwa imefunga bao huku magolikipa wakishika ama
wachezaji wakipiga nje. Sasa ilisalia tu mikwaju miwili
kwani penalti hupigwa aghalabu mikwaju mitano. Golikipa
wa timu ya Lengo akaamua kupiga penalti ya tano. Naye
kama wenzake wote aliambuliwa patupu kwani Gambo
tena aliudaka mpira ule. Nyoyo za watu zikawa mikononi
huku pumzi zikiwaenda mbio.
Ikawa ni zamu ya Gambo kupiga mpira kwenye
penalti ya tano na mwisho kwenye timu yake. Aliuchukuwa
mpira, akausawazisha kwenye eneo la penalti, akarudi
nyuma hatua moja, akatazama mbele kisha akapiga mpira
na kuutikisa wavu wa timu ya Lengo. Mlindalango alienda
upande mmoja nao mpira ukaenda upande mwingine.
Mabao yakawa moja kwa yao.
Bao hilo lilipokelewa na mashabiki kwa shangwe
na nderemo ambazo ungedhani zingaliwaamsha manabii
na mafarisayo kutoka mavani mwao masahaulifu. Gambo
aliiletea timu yake ushindi uliopelekea timu hiyo kutuzwa
kombe la fahari na shilingi alfu hamsini pesa taslimu.
Ushindi huo ulimfanya Gambo ajulikane na kuheshimiwa
na wengi huku hadithi yake ikibaki kutambwa na waja wa
kila aina.
Hatimaye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne
uliwadia. Kama kawaida, Gambo aliukabili na kuibuka
kifua mbele na kukwangura alama takribani zote. Alama
nzuri alizozipata zilimtwalia nafasi murua aliyoitamani
katika maisha yake.Nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu ili
kutimiza ndoto yake ya kuwa wakili.
49
Basi Gambo alipata mwaliko wa kujiunga na chuo
kikuu cha umma kilichomezewa mate na kila mwanafunzi.
Hivyo basi Gambo alijua kuwa kaangukiwa na nyota ya
jaha na pia Mungu kumfungulia milango ya neema na
rehema.
Mwaka huo ambao Gambo aliufanya mtihani wa
kitaifa shuleni Maua, ndio mwaka ambao shule hiyo
ilifanikiwa kupata ufanisi mkubwa zaidi ikilinganishwa na
miaka mingine ya awali. Kwa hivyo waelekezi waliamua
kuandaa sherehe kubwa ya kutoa shukurani kwa Mungu
kwa matokeo hayo murua yasiyo kifani. Gambo pamoja na
wenzake walialikwa, naye Gambo akaombwa kuhutubia
hadhira ya siku hiyo kwa niaba ya wenzake wote.
Mfawidhi alipolitaja jina lake, shangwe, nderemo
na vifijo vilihinikiza na kutamalaki anga nzima ishara
tosha kuwa Gambo alitambuliwa na kuenziwa na kila
mmoja kwa ushindi wake sio tu katika mitihani bali pia
katika nyanja nyingine kama vile michezoni na kwenye
tamasha za muziki. Ama kweli, jina jema hungaa gizani.
Haya basi tunyamaze sisi sote tumsikilize bingwa
huyu wetu. Asanteni sana, mfawidhi aliituliza hadhira.
Gambo alikabidhiwa kipaza sauti, akasafisha koo
kisha akaanza kutongoa hotuba yake:
Mwalimu mkuu, naibu wa mwalimu mkuu, walimu,
wazazi na wanafunzi wenzangu, hamjambo? Nina furaha
riboribo kupata fursa hii adimu kusema nanyi wakati
huu tunapoiaga shule hii tuliyoienzi kwelikweli. Hakika
ninamshukuru sana mwalimu mkuu kwa kunipa nafasi hii
ya kuhutubu kwa niaba ya wanafunzi wenzangu.
50
Ninawapa mkono wa tahania washikadau wote
wakiwemo walimu, wazazi na wanafunzi wenzangu
kwa ushirikiano mwema uliotusaidia kupata ufanisi huu
tunaosherehekea siku ya leo. Kwa yakini, umoja ni nguvu
na utengano ni udhaifu. Kamwe sitamsahau Maulana
ambaye ametupa uhai, nguvu na uwezo wa kuikwepa
mitego ambayo ingetuzuia kufaulu.
Walimu na wazazi, kuna mengi mliyotutendea
ambayo uzuri wake haumithiliki, wema wenu kwetu
hauna kipimo. Mungu awabariki na mbawazi zake lufufu
na azidi kuwaongoza ili muwasaidie wenzetu waliobaki
mlivyotusaidia sisi.
Kwa watahiniwa wa mwaka huu, hata na wale
wa vidato vya chini, hamna budi ila kujifunga vibwebwe
na kujitoa mhanga maishani na masomoni. Fahamu
kuwa mtaka cha mvunguni sharti ainame. Ninawaomba
mzifuate nyayo zetu, muige mazuri tuliyoyafanya na
bila shaka mtafanikiwa. Dumisha nidhamu,hulka njema
na staha kwa wote miongoni mwenu. Masomoni jifunge
masombe, hakuna wakati wa kupoteza katika uzembe
wala msivimbe vichwa. Anza kazi sasa kama sio sasa
hivi. Kumbuka, safari ya kesho huanza leo.
Ninawasihi mtukumbuke pia katika maombi
tunapoondoka ili kujiunga na vyuo mbalimbali, ili Mungu
atulinde tusije tukapotoka bali tuzidi kuwa wangwana na
kulifaa taifa letu katika siku za usoni.
Ninawashukuru nyote kwa kunisikiliza, heri na
fanaka ziwafuate popote mwendapo, asanteni.
51
Gambo alimaliza hotuba yake, akamkabidhi
mfawidhi kipaza sauti kwa utaratibu na kuondoka jukwaani
kwa unyenyekevu, huku makofi na heko za shukurani
zikimsindikiza.
Alipojiunga na chuo kikuu cha Bidii, Gambo
hakughairi nia na azma yake wala hakubadilika kitabia.
Aliendelea kuwa mkakamavu zaidi na kutia bidii masomoni.
Hatimaye alihitimu baada ya miaka mitano
chuoni, akapata shahada ya kwanza katika taaluma ya
Uanasheria. Hakika alitimiza ndoto yake.
Baada ya mahafali, chuo hicho kiliamua kufadhili
masomo ya Gambo katika kusomea shahada ya pili yaani
shahada ya uzamili nchini Marekani. Hii ni kwa sababu ya
bidii na ukakamavu wake na matokeo mazuri ya mitihani.
Alijiunga na Chuo kikuu cha Leaders nchini
Marekani ambapo alihitimu na kupata shahada yake ya
pili baada ya miaka mitatu.
Alirudi nchini na mara moja akaanza kazi yake.
Alijiunga na shirika la mawakili lililotetea haki za binadamu
na kutoa huduma za bila malipo ama kwa ada ya chini
kwa wanyonge na wasiojiweza kifedha. Daima hakushiriki
ufisadi, njia za mkato, ubinafsi wala unyanyasaji. Alihimiza
uadilifu na haki kwa wote bila kujali vyeo wala madaraka.
52
Sura ya nane
Shangwe na vigelegele vilihinikiza nje ya mahakama
ya jijini Malengoni. Wananchi walikuwa wakishangilia na
kuimba nyimbo za ushindi:
Haki leo haki leo haki leo
Raha leo raha leo raha leo
Ushindi leo ushindi leo ushindi leo...
Milango ya mahakama ilifunguka akatokea
bwana mmoja katika suti nyeupe pe! Aliuinua mkono
wa kulia alioufumba. Wananchi waliongeza shangwe na
vigelegele. Wimbo na kucheza kulipamba moto.
Gambo bingwa Gambo bingwa Gambo bingwa
Gambo simba Gambo simba Gambo simba
Haki leo haki leo haki leo
Raha leo raha leo raha leo
Ushindi leo ushindi leo ushindi leo
Baada ya dakika kumi hivi za kuimba huku
wamemwinua Gambo juujuu aliinua mikono kama ishara
53
ya kuwanyamazisha. Walinyamaza lakini waliombeba
hawakutaka kumtua chini.
Sema nasi simba wetu, walimhimiza.
Sema! Sema! Sema! Gambo sema! Umati ulipaza
sauti.
Gambo alilisafisha koo kisha akaanza, Wazee
wangu shikamoo na wenzangu mabibi na mabwana
hamjambo. Leo ni siku kubwa sana katika maisha yenu.
Kesi hii ilikuwa ngumu, imechukua mwaka mzima lakini
leo imeisha. Kilicho na mwanzo kina mwisho. Nasikitika
kwa zaidi ya miaka kumi mmeishi kama wakimbizi katika
nchi yenu.
Kuanzia wiki ijayo hakuna atakayekuwa katika
kambi tena. Uamuzi wa korti umehakikisha kila mmoja
atanunuliwa kiasi cha ardhi aliyoihama hapo awali. Juu
ya hayo kila mmoja atatunukiwa kiasi cha pesa cha
kumwezesha kujijengea angalau nyumba ya mtomo.
Wizara ya ustawi wa mifugo itaipa kila familia ngombe
mmoja. Wizara ya uchukuzi itapanga usafiri wa kila aina.
Gambo alikumbuka hotuba hiyo akiwa katika ofisi
yake Gambo na Gambo Uzalendo Advocates. Alikuwa
ameketi na mdhamini wake Mama Saida aliyemsaidia
sana kimasomo.
Barabara yake ya masomo ilikuwa imempeleka
chuo kikuu alikosomea shahada katika uanasheria.
Baadaye alikuwa amesafiri nchini Marekani kuongezea
masomo akapata shahada ya uzamili. Kazi yake ilikuwa ni
kushirikiana na makundi ya haki za kibinadamu kuwatetea
wasioweza kugharimia huduma za mawakili. Alikuwa
54
ameanzisha vituo mbalimbali vya kuwaauni randaranda
wa kiume ambao idadi yao ilikuwa imeongezeka sana
mijini. Aliwajengea makao katika vituo hivyo pamoja na
shule na karakana za ufundi.
Wakati Gambo akiwa Marekani akisomea shahada
ya uzamili, jumba la mlezi wake Bi. Saida lilinyakuliwa
na bwanyenye mmoja. Maskini Bi. Saida katika ukongwe
wake sasa hakuwa na uwezo wa kulitetea. Jumba lenyewe
ni lilo hilo walilokuwa wameketi ndani. Gambo aliporudi
alimpepeta bwanyenye huyo mahakamani akakosa la
kusema.
Bi. Saida alirudishiwa jengo hilo naye akamkabidhi
Gambo afanyie kazi yake hiyo muhimu. Kazi ya kuwatetea
wanyonge.
Gambo mwanangu, sijuti moyoni kuwa Mungu
alinimulikia nikufae utotoni. Ningejuaje ungekuja kunifaa
uzeeni. Nakutakia kila la heri nikingojea amri ya Mungu
hapa duniani, Bi. Saida alisema kwa tabasamu ya kizee.
Gambo alijaribu kusema akashindwa. Alisimama
kitini pake akazunguka meza akamkabili Bi. Saida. Ghafla,
alipiga magoti na kukiegemeza kichwa magotini pake.
Kilichofuata ni dakika nyingi za kutiririkwa na machozi.
55
La la la mwanangu. Inuka leo haikuwa siku ya
machozi. Inuka.
Gambo alisinasina huku akipangusa machozi yake.
Ni kweli mama. Si siku ya machozi. Ni siku ya faraja
iliyotimia baada ya kutuma dua kwa Maulana siku zile.
Kwa hivyo, niruhusu tutume dua tena. Naam, Dua ya
faraja.
Walifumba macho huku wameshikana mikono.
Hakika ilikuwa imetimia... Dua ya faraja.
56
Kamusi Yangu
mtima: moyo
izraili: malaika anayeaminika kuchukua roho
za watu
bwakia: hali ya kutia kinywani upesiupesi
kama vile chakula
ajuza: mwanamke mzee sana. pia
huitwa bikizee
msonge: ni nyumba ya mviringo yenye paa
lenye umbo la pia
ari: hali ya kuwa na moyo hima wa
kufanya jambo, yaani hamu
nasaha: maneno ya kumpa mtu mwongozo
mzuri katika jambo. Pia ni ushauri au
mawaidha
jizatiti: hali ya kujikaza kwa jambo, mtu au kitu
howa: neno la kumuongolea mtoto kwa nia
ya kumbembeleza alale au anyamaze
hayawani: ni wanyama; pia mtu aliye na roho ya
unyama, hana utu ama hajali
maisha ya wengine
dari: ni sakafu ya juu ya nyumba
ubao: ni njaa
yakini: hakika
57
Semi
1. Adimika Kama wali wa daku: Kukosekana kabisa.
2. Nyota ya jaha: Bahati nzuri
3. Ingiwa kichefuchefu: Kuwa katika hali ya kutaka
kutapika
4. Kata kalima: Kukatiza mtu anapozungumza
5. Shwari bila shari: Mambo kuwa sawa bila kasoro
6. Msiba wa kujitakia hauna kilio: Shida ya kujitakia
hufai kulalamika inapokupata
7. Anguka Pu!: Anguka kwa kishindo
8. Siku za mwambo: Siku za shida au taabu nyingi
9. Piga bismillahi: Kuomba
10.Ndege mbaya: Bahati mbaya
11.Kulalia mate: Kulala bila kula chakula chochote
12.Mti mkuu ukigwa wana wa ndege huyumba: Mtu
aliyekuwa akitegemewa anapoondoka waliokuwa
wakimtegemea hupata shida
13.Kula yamini: Kutoa kiapo/kuapa
58
Maswali
1. Taja methali tatu zilizotumika kwenye masimulizi
haya.
2. Tik! Tak!...Ni fani ya lugha inayoitwa________
3. Cheka Ni kwa kulia na kutabasamu Ni kwa______
4. Neno utani limetumika,Lina maana gani?
5. Paji Ni sehemu ya mwili.Je,kipaji Ni Nini?
6. Unadhani ndoto ya Gambo ilitimia?Eleza
7. Mtoto asiye na wazazi wote wawili huitwaje?
8. Mtu anayetunga mashairi huitwaje?
9. Mshororo wa mwisho kwenye beti za mashairi
unaorudiwarudiwa huitwaje?
10.Taja mambo mawili muhimu unayojifunza kutokana na
wimbo wa Taifa ambayo yamejitokeza katika hadithi
hii.