
63
Maadili
Ewe mtoto Adili, karibu keti kitini,
Nakufunza maadili, yanakili akilini,
Nawe usiwe bahili, yatie mtandaoni,
Ewe mtoto Adili, karibu keti kitini.
Kwanza nasema heshima, si utumwa nakwambia,
Heshimu baba na mama, baraka utapokea,
Mwalimu akikutuma, usichelewe kimbia,
Kwanza nasema heshima, si utumwa nakwambia.
Watendee watu haki, kisha dhuluma epuka,
Kumbuka mpanda haki, huvuna haki hakika,
Haizami kamwe haki, mwisho wake huibuka,
Watendee watu haki, kisha dhuluma epuka.
Usiwabague watu, kwa rangi wala jinsia,
Hata kilema ni mtu, kumbuka hakuchagua,
Chuki isikite kwetu, ukabila nakemea,
Usiwabague watu, kwa rangi wala jinsia,
Siku zote wajibika, bidii kazini tia,
Nyumbani unapofika, upende kusaidia,
Huvuta heri hakika, jitihada ukitia,
Siku zote wajibika, bidii kazini tia.
Tamati nimeshafika, mengi mema nimesema,
Rafiki mui epuka, ukitaka usalama,
Embe likiharibika, huoza pakacha zima,
Tamati nimeshafika, mengi mema nimesema.