
10
Kwetu mambi masuala, cha mchela kutishia,
Hata yawe zilizala, tutatuwe kitulia,
Mwewe huyu tofauti, na wengine hafanani.
Miaka mzo mepewa, ya kuishi duniani,
Na uzee kivamiwa, tarudishwa ujanani,
Nazo nguvu tarudiwa, kuliko hata mbeleni,
Nasi sije kuishiwa, nguvu zetu za mwanzoni,
Tusiweze kulemewa, na majojo maishani,
Mwewe huyu tofauti, na wengine hafanani.
Nyamafu yeye haili, windole hutegemea,
Hapo twaona idili, kwa windaji kabobea,
Nyuni wenza kithakili, mizogani kuzengea,
Nasi tunastahili, waja kutotegemea,
Tuvisake vya asili, tuepuke kuzembea,
Mwewe huyu tofauti, na wengine hafanani.
Makindawe huwafunza, wasitegemee mama,
Kwa idili huwatunza, kwani hiyo yake dhima,
Kuruka wajue kwanza, kijifunza na kuchuma,
Walimu nao hufunza, lilo hilo toka zama,
Tusije tukajiponza, ufalani tukazama,
Mwewe huyu tofauti, na wengine hafanani.
Kichagua masahibu, na hekima huongozwa,
Na wambi hujitanibu, uzembeni ‘toingizwa,
Na wenye nia harabu, asije akapumbazwa,
Upwekewe wa kuhibu, humwepusha na kutwezwa,
Yakini yake adabu, huwa njema kuigizwa,
Mwewe huyu tofauti, na wengine hafanani.
(Mtunzi: Ken Bogonko, Malenga wa Milimani)