
65
rinda, sweta, blauzi, viatu, soksi, tai na mengineyo. Mwalimu anaweza kutumia mavazi
halisi yanayovaliwa na wanawake na wanaume au awaonyeshe wanafunzi picha au
michoro ya mavazi ya wanafunzi (sare).
Mwalimu awagawe wanafunzi katika vikundi kulingana na idadi na mahitaji yao.
Awaongoze wanafunzi kushiriki katika shughuli ya pili. Wanafunzi wajadili michoro
waliyopewa kitabuni mwao na kuandika majina ya michoro hiyo. Wajadili mavazi
hayo huvaliwa na akina nani kisha watumie majina ya mavazi hayo kutunga sentensi
sahihi. Shughuli hii itasaidia kujenga na kukuza ushirikiano baina ya wanafunzi katika
vikundi.
Wanafunzi wasio na uwezo wa kuona wanaweza kupewa mavazi halisi wakayatambua.
Majina ya michoro: surupwenye/bwelasuti, koa, kanzu, kizibao, kanchiri na tai.
• Surupwenye ni vazi lenye suruali na shati zilizoshikana na huvaliwa na wanawake
na wanaume wakati wa kufanya kazi ili kuzuia mavazi mengine kuchafuka.
• Koa ni aina ya vazi linalovaliwa kichwani na wanawake na wanaume.
• Kanzu ni vazi refu kama gauni linalovaliwa na wanaume hasa wa kiislamu.
• Kizibao ni vazi aina ya koti lililo fupi na lisilo na mikono.
• Kanchiri ni vazi la kike linalovaliwa kifuani kushikilia maziwa.
• Tai ni vazi ambalo ni jembamba na aghalabu refu linalovaliwa shingoni chini ya
ukosi wa shati au blauzi na kufungwa fundo shingoni.
Mwalimu awaelekeze wanafunzi wasome kifungu kilicho katika shughuli ya tatu
ili kufahamu ujumbe wake. Mwalimu anaweza kumteua mwanafunzi mmoja asome
kifungu hicho kisha wengine wasome baada yake. Awasaidie wanafunzi kutamka
maneno ambayo yanawatatiza katika kifungu. Baadaye, mwalimu awaongoze
wanafunzi kujibu maswali ya ufahamu kwa usahihi pamoja na kila mwanafunzi
kuandika muhtasari wa kifungu husika.
Majibu tarajiwa ya ufahamu:
1. Ili asije akavalia kinyume na maadili na kujikosea heshima.
2. Kusitiri uchi, kujikinga dhidi ya baridi, kujikinga dhidi ya jua kali n.k.
3. Umri, mazingira, jinsia, majira, hali iliyoko.
4. Sweta/fulana, kabuti, chepeo, viatu, soksi, tai, kaptura, suruali n.k.
5. Mwalimu atathmini majibu ya mwanafunzi.
6. Mwalimu atathmini muhtasari wa kifungu atakaoandika mwanafunzi ili
kudhihirisha uelewa wake wa kifungu alichosoma.
Mwalimu ahitimishe somo kwa kumpa mwanafunzi kazi ya ziada itakayomshirikisha
mlezi au mzazi wake. Mlezi au mzazi amtajie mwanafunzi baadhi ya mavazi ambayo
wanawake na wanaume huvalia katika jamii yao. Pia, mwanafunzi anaweza kutumia
mtandao. Awaeleze wenzake darasani katika kipindi kijacho.