
108
Sungura akamwambia mwenzake, “Basi panda juu.” Panya buku akafanya hivyo na Sungura naye
akamfuatia. Walikuwa na mienge ya moto waliyoitumia kuwachomea nyuki waliojazana mzingani.
Baada ya kufanya hivyo wakaanza kuila asali iliyokuwako.
Mara akatokea Simba chini ya ule mbuyu uliokuwa na mzinga wa nyuki. Yule Simba aliyatupa
macho yake juu na kuona watu wanakula, akawauliza, “Ninyi ni nani?” Sungura akamwambia
buku, “Nyamaza, ana wazimu mzee yule!” Simba akauliza tena, “Nani ninyi, hamsemi?” Panya
buku akaogopa baada ya kuisikia ile sauti ya mngurumo wa Simba akajibu, “Sisi hapa!” Sungura
akamwambia buku, “Nitwae mimi, unitie ndani ya mwenge, umwambie mzee Simba, jitenge
niutupe mwenge, nami ninakuja.” Buku akafanya kama alivyoshauriwa na Sungura. Alipomtajia
Simba akajitenga na buku akautupa mwenge chini. Ulipoanguka chini, Sungura akafyatuka kama
mshale, huyoo akakimbia akaenda zake.
Baada ya muda Simba akamwambia buku, “shuka basi”. Buku akashuka kwa hofu na wasiwasi
mkubwa. Alipoka chini tu, Simba akamkamata. Akamwuliza, “Ulikuwa wewe na nani huko
juu?” Alimwambia, “mimi na Sungura. Je, hukumwona hapa nilipomtupa?’ Simba akamwambia,
“sikumwona.” Akamshika buku na kumla papo hapo. Baadaye akatoka kwenda kumtafuta Sungura
asimwone. Akaapa kuwa atamtafuta kote hadi ampate.
Kila aliyekutana naye anamwuliza, “nyumba ya Sungura i wapi?” Aliowauliza wakamwambia,
“hatuijui.” Kumbe Sungura amekwisha kumwambia mkewe, ‘tuhame nyumba hii.” Wakahama.
Simba akaenda kuuliza, wakamwambia watu, “nyumba yake ile pale juu ya mlima.” Akaenda
Simba, hata akaka lakini hakuwako Sungura. Simba akasema, “nitajicha ndani ya nyumba,
hata Sungura akija na mkewe, nitawala wote wawili.”
Sungura akaja, yeye na mkewe, hana habari lakini njiani akaona nyayo za Simba, akamwambia
mkewe, “rudi wewe, Simba amepita hapa ananitafuta mimi.” Akamwambia, “Sirudi, nitakufuata
mume wangu.” Sungura akamwambia, “Wewe mtoto wa watu, rudi.” Akarudi. Sungura akaenda,
akafuata nyayo za miguu, akaona zimeingia ndani ya nyumba yake. Akasema, “Loo! Simba yumo
ndani.” Basi akarudi taratibu, akaenda akasimama mbali, akatoa salamu, akasema, “Salaam
nyumba! Salaamu nyumba! Salaam nyumba!” Akasikia kimya. Akanena Sungura, “Jinsi gani
kila siku nikipita hapa, nikitoa salaamu, nyumba hunijibu, labda leo mna mtu humo ndani.” Yule
Simba akadanganyika, akaitikia “Salaamu!”
Akamwambia, “Loo! Simba umo ndani, wataka kunila mimi, ukasikia wapi nyumba kusema?”
Simba akamwambia, “Uningoje basi.” Sungura akatimua mbio, wakafukuzana hata Simba
akachoka. Akawaambia watu, “Sungura amenishinda basi, simtaki
tena.” Akarudi zake.
Maswali
1. Je, sungura alitumia ujanja gani?
2. Kwa nini simba alitaka kumshika sungura?
3. Je, hekaya hii ina mafunzo gani?
CH. Saru na matumizi ya lugha
Vihusishi (H)
Vihusishi ni maneno yanayoonyesha uhusiano kati ya maneno. Kwa mfano:
(a) Sungura analala kando ya mti.
(b) Salma anatembea karibu na barabara.
Chemchemi SB1 rvsd FIN.indb 108 12/11/2019 09:44