Pauline Kea
Chakula cha Biko
na Hadithi Nyingine
Gredi 1
Chakula cha Biko na Hadithi Nyingine
Kimechapishwa 2020 na Queenex Publishers Limited
S.L.P. 56049-00200, Nairobi.
Rununu: 0715 808 200, 0727 794 498
Baruapepe: info@queenexpublishers.co.ke,
queenexbooks@gmail.com
Tovuti: www.queenexpublishers.co.ke
© Pauline Kea, 2020
Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kuiga, kunakili,
kupigisha chapa, kutafsiri au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi
yoyote ile bila idhini kwa maandishi, ya Queenex Publishers
Limited.
ISBN: 978-9966-141-13-2
Chapa hii 2023
iii
Yaliyomo
1. Yaliyomo ................................................. iii
2. Zawadi ya Usafi ........................................ 1
3. Chakula cha Biko .................................... 11
4. Biko na Beki Sokoni ................................. 19
5. Mbona Fisi Huchechemea? ...................... 25
1
Zawadi ya Usafi
2
Jina langu ni Biko. Niko Gredi ya Kwanza.
Dada yangu anaitwa Beki. Tulizaliwa siku
moja.
3
Jina langu ni Beki. Niko Gredi ya Kwanza.
Biko ni kaka yangu. Sisi ni pacha.
4
Biko na Beki wanaangika kibuyu cha maji.
Watayatumia maji kunawa mikono baada
ya kutoka chooni. Watayatumia maji pia
kunawa mikono kabla ya kula chakula.
5
Watoto wametoka chooni. Watoto
wananawa mikono kwa maji ya Beki na
Biko. Wanataka kurudi darasani.
6
Watoto wananawa mikono, wametoka
kucheza uwanjani. Kima anawaona akiwa
juu ya mti mkubwa. Kima anataka kunywa
maji.
7
Kima anakunywa maji ya Beki na Biko.
Ananawa uso pia.
8
Watoto wanaangika vibuyu zaidi vya maji
mitini.
Wanataka kila mtoto awe safi. Wananawa
mikono, nyuso na wengine wanaosha viatu
vyao.
9
Mwalimu mkuu anawapa Biko na Beki
zawadi ya usafi. Anasema Biko na Beki
wamewafundisha watoto kuangika vibuyu
vya maji.
Watoto wanaimba huku wakipiga makofi.
Hongera, hongera, hongera, hongera,
Hongera, hongera, hongera, hongera.
10
1. Biko na Beki wanaangika nini mtini?
2. Kwa nini watoto wananawa mikono?
3. Kwa nini kima alikunywa maji?
4. Je, mbona wewe hunawa mikono?
5. Unafikiri Beki na Biko walipewa zawadi
gani?
Jibu maswali yafuatayo.
11
Chakula cha Biko
12
Watoto wananawa mikono.
Wanataka kula chakula chao cha mchana.
Kima anaingia darasani.
13
Watoto wamerudi darasani. Kima
amechukua chakula cha Biko. Kima anataka
kula viazi vitamu vya Biko. Biko analia.
14
Watoto wanampa Biko chakula na matunda
ale. Biko anapokea ndizi, chungwa na
muhogo. Anawashukuru watoto wenzake.
15
Biko anaosha matunda aliyopewa na
wenzake.
Kima anamwangalia Biko kutoka mbali.
Anakula viazi vitamu vya Biko.
16
Watoto wanakula vyakula kama vile uyoga,
mayai, muhogo na ndizi. Wengine wanakula
mahindi na maharagwe. Beki amemkatia
Biko muhogo ale.
17
1. Kima alikula chakula kipi?
2. Je, Biko alipewa nini na wenzake ale?
3. Je, kama ungekuwa Biko ungefanya nini?
4. Taja vyakula ambavyo watoto wanakula
darasani.
5. Je, wewe hula chakula kipi?
Jibu maswali yafuatayo.
18
Biko na Beki Sokoni
19
Biko, Beki na mama yao wanaenda sokoni
kununua chakula. Mama anabeba kikapu
kikubwa. Beki na Biko wana vikapu vidogo.
20
Biko, Beki na mama wanafika sokoni.
Wananunua mbaazi, pojo, mchele, karoti,
nyanya na dania. Mama anachagua na
muuzaji anamsaidia.
21
Biko na Beki wanataka barafu. Mama
anasema kuwa daktari alisema wasile
barafu. Mama anasema barafu inaweza
kuharibu meno.
22
Biko na Beki wanapewa tende. Tende ni tamu
kuliko barafu. Wanakula na kufurahi.
23
Biko, Beki na mama wanarudi nyumbani.
Wamenunua chakula kingi. Pia wamenunua
tende. Wanaimba wimbo wa chakula.
Ndizi na tende, tamu, tamu kabisa, tamu, tamu.
Karoti, njugu, tamu, tamu kabisa, tamu, tamu.
24
1. Biko, Beki na mama walienda sokoni
kununua nini?
2. Biko na Beki walililia nini?
3. Kwa nini mama alikataa kununua barafu?
4. Je, Biko na Beki walikula nini badala ya
barafu?
5. Je, wewe unapenda vyakula vitamu?
Jibu maswali yafuatayo.
25
Mbona Fisi Huchechemea?
26
Hapo zamani za kale, wanyama waliishi kwa
amani. Hakuna mnyama aliyekula mwingine.
Wanyama wote walipendana.
27
Siku moja, chura aliandaa karamu ya siku ya
kuzaliwa kwake. Alitayarisha viazi choma,
mahindi na ndizi za kupika. Alipika pia supu
ya mboga na karoti kwenye chungu.
28
Fisi alifika kwenye karamu. Alicheka na
kutoa mate akisema ana njaa. Aliambiwa
chakula bado kilikuwa kinapikwa.
29
Fisi alichungulia ndani ya chungu cha supu.
Chungu kilikuwa na harufu nzuri. Fisi alitoa
mate na kucheka.
30
Fisi aliteleza na kuingia ndani ya chungu
cha supu. Ndovu alimtoa haraka kwa mwiro
wake. Fisi alilia kwa uchungu.
31
Fisi alichomeka na kupata alama kwenye
ngozi yake. Fisi pia aliumia miguu yake ya
nyuma ikawa mifupi. Fisi alitembea vibaya.
32
1. Je, chura alipika nini?
2. Fisi aliingia vipi chunguni?
3. Je, wewe unapenda supu ya nini?
4. Kama wewe ungekuwa fisi ungefanya
nini?
5. Msimulie mwenzako hadithi hii.
Jibu maswali yafuatayo.