Bintu na Bintutu
Tom Nyambeka
Imarisha Lugha
Bintu na Bintutu
Kimechapishwa na Queenex Publishers Ltd.
S.L.P 56049-00200, Nairobi, Kenya.
Simu: 0727 794 498, 0715 808 200
Barua pepe: info@queenexpublishers.co.ke
queenexbooks@gmail.com,
Tovu: www.queenexpublishers.co.ke
Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kuiga, kunakili,
kupigisha chapa kutafsiri au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi
yoyote ile bila idhini, kwa maandishi ya Queenex Publishers
Limited.
Chapa ya kwanza 2018
Chapa ya pili 2021
ISBN: 978-9966-075-09-3
1
Sura ya Kwanza
Hapo zamani za kale, iliishi familia moja. Familia
hiyo ilikuwa ya Bwana Bintu na mke wake Bintutu.
Bintu na Bintutu walikuwa wameishi pamoja kwa miaka
ishirini. Bwana Bintu alikuwa na miaka hamsini. Bintutu
naye alikuwa na miaka arubaini na mitano. Wawili hao
walipendana sana. Walipendana sawa na mlango na
kufuli.
Bintu na Bintutu walijaliwa watoto watatu. Wasichana
wawili na mvulana mmoja. Mtoto wa kwanza aliitwa
Faida. Huyu alikuwa msichana. Mtoto wa pili aliitwa
Matu. Huyu alikuwa mvulana. Kitindamimba aliitwa
Bahati naye alikuwa msichana pia. Bwana Bintu na
Bintutu waliwapenda watoto wao kama mboni za
macho. Waliwapatia kila hitaji la kimsingi walilofaa
kupewa.
2
Familia hii iliishi katika kijiji kilichoitwa Bintuke. Kijiji
hicho kilikuwa kimezungukwa na msitu mkubwa ajabu!
Msitu huo uliitwa Bintudamu. Msitu wa Bintudamu
ulikuwa umeenea na kusambaa kotekote na hata kufika
kwenye vijiji vingine vilivyopakana na Bintuke. Kwenye
msitu huo miti ilikuwa imeshikana na kushikamana
karibukaribu. Miti hii ilikuwa ikisababisha giza kubwa
kwenye maeneo yaliyokuwa karibu, hata mchana. Upo
wakati majitu yaliufanya msitu wa Bintudamu kuwa
makao yao. Majitu hayo yaliwasumbua wanakijiji kwa
muda mrefu.
...waliwapenda watoto wao kama mboni za macho...
3
Majitu yangaliwaua mifugo usiku na mchana kisha
yakatoroka na kujificha kwenye msitu wa Bintudamu.
Hayo yalikuwa makazi yao. Wakati mwingine majitu
hayo yangaliwajeruhi au hata kuwaua wanakijiji na
kuzinywa damu zao. Ilikuwa rahisi kwa majitu hayo
kuwakamata watoto, ajuza na mashaibu kwa sababu
wasingeweza kukimbia kwa kasi kuyashinda. Kwa hivyo
majitu hayo yaliwakamata kwa haraka na kwa urahisi.
Wakazi wengi wa Bintuke walikuwa walemavu
kutokana na majeraha waliyoachiwa na majitu hayo.
Ulikuwa ulemavu ambao hawakuumbwa wala kuzaliwa
nao! Wapo waliokatwa miguu, mikono na wengine
kujeruhiwa vibaya kwenye sehemu nyingine kadhaa
milini mwao.
Malalamishi ya Wanabintuke yalipowafikia walinzi
wa misitu na wanyamapori, askari walitumwa kuyasaka
na kuyatafuta majitu hayo. Askari hao walifanya kila
jitihada kuyasaka kwenye msitu wa Bintudamu ili
wayaue lakini wapi? Hawakufua dafu. Majitu hayo
yalikuwa yamegundua kuwa yalikuwa yakisakwa. Kabla
ya kufika kwa kikosi cha askaripori, yangalionekana
yakizurura hapa na pale katika kijiji. Lakini askaripori
walipofika hayakuonekana kwa urahisi. Nguvu za kikosi
hicho ziliambulia patupu. Hawakufaulu kuyapata
majitu hayo.
4
Licha ya jitihada za kikosi hicho cha askaripori
kuyawinda majitu hayo, jambo lililowashangaza wengi
ni kuwa kila kulipokucha, ngombe, mbuzi na kondoo
wao wengi walikuwa wameuliwa. Damu na mifupa
ya mifugo wao ilitapakaa kote kijijini! Kila asubuhi
wanakijiji waliamkia maombolezo. Maombolezo ya
kuwapoteza mifugo na kuwaachia hasara nyingi.
Majitu haya yalitumia mbinu gani? Yalijificha wapi?
Yaliua vipi mifugo yasije yakapatikana na kikosi kile
cha askaripori? Hayo yalikuwa baadhi ya maswali
waliyojiuliza Wanabintuke wasiweze kupata majibu!
Kwa kweli, majitu hayo yalikuwa yameota meno!
Bwana Bintu aliheshimika sana kule kijijini Bintuke.
Katika umri wake wa ujana aliwahi kuwa kamanda
wa vikosi vyote vya polisi katika taifa zima kikiwemo
kikosi cha kuilinda misitu na wanyamapori. Lakini sasa
alikuwa amestaafu. Alikuwa katika awamu yake ya
mwisho ya kujirambia chumvi yake ya kiinuamgongo.
Zama hizo akiwa barobaro, aliviongoza vikosi vyote
kuleta usalama kwenye mataifa yaliyokuwa na matatizo
ya usalama. Uongozini mwake, alifaulu pakubwa na
kusababishia mataifa mengi kupata usalama. Aliweza
kutuzwa zawadi nyingi za ushindi huo akiwa kamanda
mkuu. Hakusifika tu na wanakijiji bali pia alisifika katika
taifa zima. Kutokana na sifa hizo za Bwana Bintu, kikosi
kile cha askaripori kiliamua kumshirikisha kuwasaidia
5
katika shughuli ya kuyasaka majitu yale.
Waliamini kuwa koti la mzee halikosi chawa.
Ushauri wake ungaliwafaa hapa na pale na vilevile kinga
na kinga ndipo moto uwakapo. Licha ya hilo, Bwana
Bintu walijuana kuanzia kokwa hadi ngozi na kiongozi
wa askari hao wa kuilinda misitu na wanyamapori.
Walikuwa wamefanya kazi naye na kwa pamoja hapo
awali. Kwa hivyo, walimwamini na kumsadiki kwa njia
zote. Walimthamini sawa na mboni za macho yao.
6
Sura ya Pili
Bwana Bintu na kikosi cha askaripori waliendelea
kujitahidi kwa jino na ukucha kuyasaka majitu hayo
siku baada ya siku. Kwa sasa ripoti kuhusu mauaji ya
wanyama zilikuwa zimepungua. Wanakijiji walikuwa
washarejelewa na utulivu wa akili kwa kiasi fulani.
Uhalifu wa majitu yale ulikuwa umeanza kupungua.
Ushauri wa kuwatahadharisha wanakijiji hasa watoto,
ajuza na mashaibu wasitoke nje ovyoovyo ulitolewa.
Maafa na mejeraha kwa Wanabintuke yalikuwa
yamepungua kwa kiwango kikubwa. Kwa sasa wanakijiji
wengi hasa watu wazima na wenye nguvu walikuwa
wameshirikishwa kwenye shughuli zote za kuyasaka
majitu. Hakuna aliyejali mbinu ambazo zingalitumiwa
almradi tu majitu hayo yauliwe. Ziwe mbinu za kisasa
au za kale. La muhimu lilikuwa kuhakikisha kuwa majitu
7
hayo yameangamizwa kabisa kutoka katika kijiji cha
Bintuke.
Mzee wa kijiji cha Bintuke, Bwana Chatu alikuwa
ameshirikishwa kwenye mpango huo wa kusaidia
kutoa maoni. Baadhi ya wanakijiji walikuwa wametoa
maoni kuwa majitu yaliyowasumbua yalikuwa matatu.
Maoni hayo yangalisaidia kuyanasa majitu yale. Msako
wa kuyasaka majitu yale uliendelezwa kwa jari moja
na kikosi kile cha askaripori pamoja na wanakijiji
kadhaa walioteuliwa. Mbinu zote zilitumiwa na ulinzi
mkali kuwekwa dhidi ya majitu yale na kikosi kile cha
askaripori pamoja na wanakijiji wa Bintuke. Walisadiki
kuwa mchumia juani hulia kivulini.
Majitu yale matatu hayakuonekana kabisa sasa.
Yaliadimika mfano wa seserumbe baharini! Msako
mkali uliendelezwa kwenye kila sehemu ya msitu.
Waliyasaka juu ya miti, mapangoni na kila sehemu
waliyoishuku. Hawakuyapata ngo!
Wakati mmoja Bwana Chatu alikiomba kikosi
kile cha askaripori kuwaita wanakijiji wote kwenye
mkutano. Nijuavyo tukiwahusisha wanakijiji wote
tunaweza kupata ushauri na mwelekeo utakaotufaa
zaidi. Ninaamini kuwa umoja ni nguvu na utengano
ni udhaifu, Bwana Chatu alishauri.
Naam, ninamuunga mkono Bwana Chatu. Hayo
ni maoni mazuri. Tutafanya hivyo bila shaka, kiongozi
8
wa askaripori aliitikia. Walikubaliana kuitisha mkutano
kwa wanakijiji siku mbili baadaye.
Mbiu ya mgambo ililizwa kwa haraka na kila
mwanakijiji akaombwa kufika kwenye boma la Bwana
Bintu. Hapo ndipo mkutano huo ungalifanyika. Mkutano
huo uliwahusisha wakubwa kwa wadogo. Awe mtoto
awe mtu mzima. Haukuwa mkutano wa kubagua. Maoni
yote yalihitajika bila kuzingatia umri, kimo wala nafasi
ya mtu. Baada ya muda mfupi, ujumbe kuhusu kikao
hicho ulikuwa umemfikia kila mwanakijiji cha Bintuke.
Hivyo basi siku ya mkutano ilipofika, Wanabintuke
walifika kwenye boma la Bwana Bintu bila kuchelewa.
Kila mwanakijiji alifahamu fika kuwa chelewa chelewa
utamkuta mwana si wako. Mkuu wa kikosi cha
askaripori alikuwa wa kwanza kuzungumza.
Wanakijiji wa Bintuke, kwanza kabisa
ninawakaribisha kwa heshima na taadhima kwenye
mkutano huu. Pili, pole sana kwa matatizo na hasara
kubwa ambazo zimesababishwa kwenu na majitu.
Ninajua yamewarudisha nyuma sana kimaendeleo.
Mnavyohisi ndivyo tunavyohisi pia. Kilio chetu ni kimoja,
maanake shida zenu ni sawa na zetu. Ndio maana
tumekuwa hapa kwa muda kushirikiana nanyi ili kupata
suluhu ya tatizo hili la majitu.
9
Tumekuwa hapa kwa muda huu wote ili kuhakikisha
kuwa hamtaendelea kupata hasara kutokana na majitu.
Kwa niaba ya serikali, ninawapokeza pole kwa hasara
mlizosababishiwa na majitu haya. Nina uhakika kuwa
suluhu ya kudumu itapatikana hatimaye kwani hakuna
refu lisilokuwa na mwisho wake. Kwa sasa sitakuwa
na mengi ya kusema ila nitaomba moja kwa moja
tuwapatieni nafasi ya kutoa maoni na ushauri wenu
kuhusu mbinu mbalimbali ambazo tunaweza kutumia
kuyaangamiza na kuyaua majitu haya, kiongozi yule
alimaliza.
...walifika kwenye boma la Bwana Bintu bila kuchelewa...
10
Wanabintuke waliinua mikono yao mmoja baada ya
mwingine huku wakitoa maoni yao mbalimbali kuhusu
mbinu ambazo zingalitumiwa dhidi ya majitu hayo.
Yalikuwa maoni yaliyojaa ufasaha na hekima isiyo
mithali. Yalikuwa maoni mazuri ambayo yangalisaidia
kuyanasa majitu yale na kuyasafirisha makaburini bila
nauli wala matwana! Baada ya michango kadhaa kutoka
kwa Wanabintuke, zamu yake mzee wa kijiji Bwana
Chatu kutoa maoni na ushauri wake ilifika. Alijikohoza
mara moja mbili kisha akaanza kuzungumza.
Naam wanakijiji wenzangu, ninakumbuka hapo
zama za zama nilipokuwa mtoto, visa vya majitu
vilisikika na kuenea sana. Vilisikika kwenye kijiji cha
Bantu. Ninajua kila mmoja ashakisikia kijiji hicho hata
kama kiko mbali kiasi kutoka humu kijijini mwetu.
Majitu hayo yalikuwa yakijibadilishabadilisha
kimaumbile na kuchukua maumbo tofautitofauti. Mara
yangalijigeuza na kuchukua maumbo ya ngombe, mara
mbuzi, mara binadamu wa kawaida, mara binadamu
wenye jicho moja. Mara kwa mara yangalijigeuza
yakawa watu na kuingia kwenye nyumba zao. Maumbo
hayo ya kibinadamu yangaliwadanganya watu na
hivyo wangaliyakaribisha nyumbani mwao. Baada ya
muda yangewageukia na kuwala! Ninakumbuka siku
moja kabla ya kifo cha baba yangu, aliniambia kwamba
11
wakati mmoja kijiji cha Bantu kilivamiwa na majitu mengi
sana.
Wanakijiji cha Bantu walitafuta mbinu na kuyaua
yote. Majitu hutembea kwa pamoja. Hawaliachi jitu
hata moja nyuma, Baba aliniambia. Hiyo ndiyo sifa
ya kipekee kuyahusu majitu aliyoiniachia baba yangu.
Nina matumaini kuwa tukitumia maelezo haya kuhusu
sifa hizo hii ya kipekee aliyonipatia baba yangu, bila
shaka tutafaulu kuyaangamiza majitu haya.
Ninaomba tumchague mtu mmoja miongoni mwetu
hapa ili afunge safari hadi kwenye kijiji cha Bantu kwa ajili
ya wazee wa kijiji hicho kumpa siri zaidi walizozitumia
hadi wakayaangamiza majitu yaliyowasumbua watu
wao enzi zile. Ninawaomba tusaidiane kumchagua
mwakilishi mmoja ili kuwa mjumbe wetu katika kijiji cha
Bantu, Mzee Chatu alisita kidogo. Alisitisha hotuba
yake ghafla na kushauriana na kikosi kile cha askaripori
kwa sauti ya chini.
Kila mmoja alionekana akikitikisa kichwa chake juu
na chini ishara ya kukubaliana na maoni ya Mzee Chatu.
Kila mwanakijiji aliyeuinua mkono wake alimchagua
Bwana Bintu. Baadaye na kwa pamoja, wanakijiji wote
walikubaliana kwa kauli moja kwamba Bwana Bintu
awe mjumbe wa wanakijiji wa Bintuke huko Bantu.
12
Sifa na tajriba zake za awali, za kuwa katika
kitengo cha usalama kwa muda mrefu zilichangia
pakubwa kuteuliwa kwake Bwana Bintu. Wanakijiji
walishangilia kwa shangwe na nderemo kuchaguliwa
kwake Bintu. Kijiji cha Bantu kilikuwa umbali wa kilomita
themanini hivi kutoka pale kijijini Bintuke. Bwana Bintu
angalitembea kwa miguu hadi kwenye kijiji cha Bantu.
Ilikuwa safari ndefu sana. Safari hiyo ingalimchukua
siku tatu njiani. Siku moja na nusu kwenda na siku moja
na nusu kurudi.
Zamani zile hakukuwa na magari. Gari lingalionekana
kijijini ama mara moja au mbili. Yalikuwa nadra kama
barafu ya kukaangwa. Vilevile, barabara zilikuwa
chache na zilizoharibika kabisa. Zilikuwa za udongo na
zenye mashimo mengi!
Bintutu, mke wake Bwana Bintu na wanawe Faida,
Matu na Bahati pia walikuwa kwenye mkutano huo.
Walishuhudia Bwana Bintu akiteuliwa kuwa mjumbe
wa Wanabintuke. Walifurahia ndani kwa ndani kama
vitoto vya shule ya chekechea vilivyofuzu kujiunga
na darasa la kwanza. Hata hivyo, kwa asilimia fulani
walimhurumia Bwana Bintu hasa kutokana na urefu wa
safari hiyo. Kwa kweli, ilikuwa safari ya kitalifa kirefu.
Hata hivyo, Bwana Bintu angalifanyaje? Ilimbidi kwani
lisilo na budi hutendwa. Idadi ya majitu kwenye
msitu wa Bintudamu ilikuwa tatu. Idadi hii ilijulikana
13
mwanzomwanzo kabla ya askaripori kutumwa kijijini
humo. Wakati huo majitu hayo yalitembea hata
mchana huku wanakijiji wakijifungia nyumbani ili wasije
wakajipata wakiwa maiti ghafla kutokana na kuvamiwa
na majitu hayo. Wanakijiji waliyashuhudia mchana
peupe yakifuatana unyo kwa unyo.
Mkuu wa askaripori aliendelea, Shukrani
Wanabintuke kwa kutoa maoni yenu mazuri. Maoni
yenu yote tumeyachukulia kwa uzito sana. Yamekuwa
maoni mazuri ambayo ninajua yakiunganishwa
yatatupatia mbinu za kuyashika na kuyaua majitu haya.
Nina furaha pia na ninawapongeza kwa kukubaliana
na ushauri wake mzee wa kijiji Bwana Chatu. Kama
walivyosema wazee wetu, wengi wape.
Basi ninamwomba Bwana Bintu kuyaheshimu maoni
ya wanakijiji na kuwa mjumbe wao. Ninajua Bwana Bintu
ana uwezo wa kufanya hivyo. Ninamwamini kwa dhati
ya moyo wangu. Mimi na kikosi changu askaripori,
tutaondoka na kuisubiri ripoti yake Bintu akirejea.
Atakaporudi, tutarejea papa hapa kuisikiliza na kuitumia
kwa pamoja. Muwe waangalifu na wenye tahadhari
kubwa kwenye shughuli zenu hadi atakaporudi,
alihitimisha.
14
Sura ya Tatu
Umati ulifumukana na kila mmoja akaelekea
nyumbani kwake. Kila mmoja alionyesha ishara ya
subira kwani subira huvuta heri. Bintu na familia yake
walibaki nyumbani mwao baada ya umati kuondoka.
Wote waliingia sebuleni mwa nyumba yao. Kila mmoja
aliketi na kulitega sikio lake na kumsikiliza Bintu kwa
makini. Aliwashauri jinsi ya kuishi kwa usalama hadi
siku ya kurudi kwake. Bintu aliipenda na kuithamini
familia yake sana. Alijali usalama wa familia yake.
Kutokana na upendo huo wa Bwana Bintu, hakukosa la
kuwashauri nalo;
Mke na watoto wangu, mnavyojua ninaondoka
kuelekea kijijini Bantu. Nina matumaini kuwa nitarudi
nikiwa mzima kama kigongo na mwenye buheri wa
afya.
15
Kwa sababu hiyo, ni muhimu mke wangu Bintutu
kuhakikisha kuwa wewe na watoto wetu wako salama
hadi nitakaporudi. Mke wangu, ninakuomba uzitumie
hela nitakazokuachia kwa uangalifu ili kuyafikia mahitaji
yenu nyote. Mahitaji ya vyakula na mavazi.
Wanangu, mtiini mama yenu kwa kila namna.
Akiwatuma mtumike. Muwe wenye maadili kwa kila
mtu maanake hewala haigombi na mtoto akibebwa
hutazama kisogo cha mama yake. Msaidieni mama
yenu kufanya kazi nyepesi nyepesi kama vile kufagia
na kuosha vyombo hapa nyumbani. Mnajua kuwa
ninawapenda sana wanangu. Ninakupenda sana pia
Kila mmoja aliketi na kulitega sikio lake na kumsikiliza ...
16
mke wangu. Ninawaamini na kuwathamini kwa dhati.
Kwaheri mke wangu! Kwaherini wanangu, Bintu
aliwashauri.
Mume wangu, nimekuelewa kwa umakinifu mwingi!
Nitaufuata ushauri wako kwa karibu hadi utakaporudi
majaaliwa. Ninamwomba Mwenyezi Mungu akuongoze
kwa kila njia. Akuongoze unapoanza safari hadi pale
utakapofika. Akuongoze ili ufike salama. Ninakuombea
safari yako iwe yenye heri mume wangu. Kwaheri ya
kuonana! Bintutu alimtakia heri mume wake.
Bintutu alipokuwa akizungumza na mume wake,
watoto wao walisikiliza kwa makini pia. Walikuwa watoto
watiifu, wenye heshima na watulivu. Walielewa umuhimu
wa kusikiliza. Walielewa bayana kwamba kusikiliza
humwezesha mtu kuupata ujumbe unaotolewa.
Asante baba. Asante kwa ushauri wako kwetu!
Kuutii ushauri wako ni kwa manufaa yetu sisi sote.
Tumeelewa na tutautii! Safari yako iwe ya heri na
ya mafanikio baba, watoto wake walimwambia kwa
pamoja.
Bwana Bintu aliingia chumbani mwake haraka
haraka kama umeme. Alipotoka nje alikuwa amejihami
kwa uta, mishale ndani ya podo, mkuki na ngao. Pia,
alijibebea angaa chakula na maji ya kutulizia njaa na
kiu akiwa safarini.
17
Angalitembea mchana kutwa na usiku kucha.
Angalitembea hadi afike kwenye kijiji cha Bantu.
Asingaliogopa chochote kwa sababu alikuwa
amejihami kwa jino na ukucha. Angaliipanda milima
na kuyashuka mabonde. Apite kwenye misitu na nyika.
Ilikuwa safari ya pandashuka!
Nyumbani kwa Bwana Bintu maisha yaliendelea
salama salmini tangu alipoondoka. Maisha yalikuwa
shwari bila shari kwa mke na watoto wake. Mke wake
na wanawe waliishi kulingana na ushauri wa Bwana
Bintu. Waliishi kulingana na mapenzi ya Mungu.
...alikuwa amejihami kwa uta, mishale ndani ya podo...
18
Faida alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili, Matu
miaka kumi naye Bahati alikuwa na miaka minane.
Wasingeondoka nje ya nyumba yao kwenda kucheza
bila ruhusa ya mama yao. Vilevile, wasingewevichukua
vitu vya wengine bila idhini. Hawakuwa wenye mikono
mirefu. Pia, hawakutia ujeuri wafanyavyo baadhi ya
watoto hasa walio na umri kama wao. Walipotumwa
walitumika na walipokanywa walikanyika. Baadhi ya
watoto wanapofikisha umri kama huo huwa hawatumiki!
Licha ya kuwa baba yao alikuwa ashaondoka, walimtii
mama yao kikamilifu. Walikuwa vielelezo na mifano
mizuri kwa marika wao na hata waliowazidi umri kijijini
Bintuke.
Matu alikuwa ashakipitia kisu cha ngariba kule
jandoni. Makungwi walikuwa wamefanya kazi nzuri
ya kumshauri jinsi ya kuishi na watu. Jinsi ya kuwa
jirani mwema kwa wengine. Ujirani wa kusaidiana na
kuwaheshimu wengine. Ujirani wa kujitahidi maishani
na kuuheshimu utamaduni wa wengine.
Faida na Bahati walikuwa na bahati waliyoikosa
baadhi ya wasichana wa rika lao. Wasichana wengi
katika kijiji cha Bintuke walikuwa wamezipitia nyembe
za wakeketaji! Bwana Bintu na mkewe Bintutu
wasingalikubali wasichana wao kuupitia unyama huo.
Walielewa athari za ukeketaji wa mtoto msichana.
Walielewa daima haki za mtoto msichana katika jamii.
19
Vipo visa vingi vya kuogofya vilivyowakumba
wasichana wengi waliopitia ukeketaji katika kijiji cha
Bintuke! Wapo waliovuja damu hadi wakafa, wapo
waliosababishiwa utasa, wapo walioyakuta mauti
wakijifungua walipokuwa wakubwa na kuolewa, wapo
walioambukizwa maradhi hatari kama vile UKIMWI.
Yote haya yalitokana na ukeketaji. Si kwamba ukeketaji
wa watoto ulikuwa umekubaliwa katika kijiji cha Bintuke!
La hasha! Ukeketaji ulikuwa umepigwa marufuku na
kuharamishwa kabisa ila tu wapo waliouendeleza chini
kwa chini. Waliuendeleza ukeketaji kwa kusingizia
kuuendeleza utamaduni.
20
Sura ya Nne
Siku ya tatu ilikuwa imefika. Hii ndiyo iliyokuwa siku
ya kurudi na kurejea kwake Bwana Bintu kutoka kijijini
Bantu. Alisubiriwa kwa hamu na hamumu na kila
mwanakijiji pamoja na kikosi kile cha askari wa kuilinda
misitu na wanyama. Kila mmoja alikuwa na uchu wa
kurejea kwa Bwana Bintu ili kuileta suluhu ya kuyaua
yale majitu. Bintutu alikuwa ameamka mapema kabla
ya jua kuchomoza siku hiyo. Hii ndiyo iliyokuwa siku
yake ya kuzifua nguo na kuufanya usafi wa ndani kwa
ndani katika nyumba yake. Aliamka saa kumi na mbili
za alfajiri hivi.
Alikuwa akiyafua marobota na maburungutu ya
nguo ya familia yake. Hata hivyo ilimbidi awe macho
asije akavamiwa na majitu ghafla bila ya kutarajia
kwake. Aliithamini kauli kuwa jihadhari kabla ya
21
hatari. Hakusahau kuwa msitu wa Bintudamu ulikuwa
makazi ya majitu. Ilimbidi aharakishe kisha aingie
nyumbani kabla ya majitu yale kuamka. Baada ya
muda wa saa moja hivi, Bintutu alikuwa amemaliza
kufua. Alipomaliza, aliingia chumbani. Kufikia saa
tano, wanakijiji wote walikuwa wamefika bomani mwa
Bwana Bintu. Walijazana na kushonana kama nyota
angani. Wallahi mvua ingalinyesha, hata tone moja
lisingaliuramba mchanga.
Mkuu wa kikosi cha askaripori alikuwa amefika.
Wakati huu hakuja na kikosi kizima. Alitaka kuupata
ujumbe wa Bwana Bintu mwanzo kisha aufikishe kwa
kikosi chake. Vilevile, asingeandamana nao kwa sababu
huenda walikuwa na majukumu ya kuwahudumia
wananchi kwingine.
Kila mmoja alitamani Bwana Bintu afike. Afike akiwa
na ripoti ambayo ingalileta suluhu ya kuyaua majitu
yale. Ghafla tu wakiendelea kumsubiri Bwana Bintu,
wimbo ulisikika kwa umbali. Ulisikika kwa kufifiafifia
tu. Maneno ya wimbo wenyewe yalizidi kusikika vizuri
kadiri waimbaji hao walivyozidi kulikaribia boma la
Bwana Bintu. Sauti zilizosikika zilikuwa nzito. Zilikuwa
sauti za kiume. Hao ndio waliokuwa wakiuimba wimbo
huo. Midundo ya dududu! dududu! Ilisikika. Ilikuwa
midundo ya magoma.
22
Wanaume zaidi ya mia moja waliokuwa na silaha
kali waliingia kwenye boma la Bwana Bintu. Hili ndilo
kundi lililokuwa limechaguliwa mapema na Mzee Chatu
kumlaki Bwana Bintu punde tu atakapofika kijijini.
Waliimba na kurukaruka. Walikuwa wamemvisha
Bwana Bintu mizizi na majani ya miti kwenye shingo
yake. Zilikuwa nyimbo maalum za kumkaribisha na
kumpokea Bwana Bintu. Alirejea nyumbani baada ya
siku tatu walivyokubaliana na wanakijiji pamoja na
kikosi kile cha askaripori. Naam, ahadi ni deni na dawa
ya deni ni kulipa.
Bwana Bintu alipokelewa kama shujaa. Alikuwa na
ujumbe muhimu moyoni mwake kwa wanakijiji wenzake.
Wanaume watano wakiongozwa na kundi lile la
wanaume zaidi ya mia moja, walimbeba hobelahobela
hadi walipokuwa wamesimama mzee wa kijiji Bwana
Chatu na mkuu wa kikosi cha askaripori.
Ninamwomba kila mmoja wetu kutulia tafadhali,
Mzee wa kijiji, Bwana Chatu aliuomba umati ule.
Kila mmoja alinyamaza kama maziwa kitomani.
Wanabintuke walikuwa watu watiifu kwa Mzee Chatu.
Alipoongea walimtii. Walielewa dhahiri kuwa heshima
si utumwa wala hainunuliwi.
23
Mnavyoona, Bwana Bintu ameshafika. Nina imani
kwamba ametuletea ujumbe muhimu kwetu. Bwana
Bintu, ninajua hujapumzika lakini ninakuomba kuvumilia
na kujikaza kwa muda mfupi tu ili utueleze ujumbe huu.
Ama vipi Bwana Bintu? Bwana Chatu alimgeukia na
kumuuliza.
Kwa kutabasamu Bwana Bintu alijibu, Suluhu
nimeipata na ninayo hapa. Umati wote ulimshangilia
kwa makofi na vigelegele. Shujaa wao alikuwa amefika.
Walitaka kumsikiliza kwa makini kuwapa suluhu ya
kuangamiza majitu.
...Bwana Bintu alipokelewa kama shujaa...
24
Kabla ya kumpatia Bintu nafasi ya kutufafanulia
suluhu, ninaomba mkuu wa kikosi cha ulinzi wa misitu
na wanyamapori kusema nasi. Karibu ndugu, Mzee
Chatu alimkaribisha mkuu wa kikosi cha askaripori.
Shukrani kwa nafasi wenzangu. Karibuni nyote
kwenye kikao hiki. Karibu sana Bwana Bintu na pole
kwa safari. Ninajua umekuja na ushauri utakaotufaa
sisi sote dhidi ya shida zilizoletwa na majitu kwenye
kijiji cha Bintuke. Mjuavyo mimi na kundi langu tulijaribu
sana ila jitihada zetu hazikufaulu ingawa zilisaidia kwa
kiwango fulani kuyaogofya majitu hayo. Ninajua baada
ya muda yatarejea tena. Yatarejea yatakapogundua
hayafuatiliwi tena. Kwa sasa sina wasiwasi wa mwasi
maanake utatupa suluhu kutoka kwenye kijiji cha Bantu.
Bwana Bintu, naomba kukukaribisha sasa useme nasi.
Karibu sana ndugu yangu, Mkuu wa kikosi alisema.
Mkuu wa kikosi cha walinzi wa misitu na Wanabintuke
hamjambo? Naam, mwanzo ninamshukuru Mungu
kwamba aliniongoza nikafika kwenye kijiji cha Bantu.
Niliwafikia wazee wa kijiji hicho kama mlivyonituma.
Wazee hao ni karimu na wastaarabu sana. Walinipatia
ushauri ambao ninaamini utatufaa sote. Ushauri huu
ni suluhu ya kuyaua kabisa majitu yanayotusumbua.
Hakuna aliyejua kuwa majitu hupenda uji kote kijijini
mwetu hapo awali! Yupo? Nina uhakika hamna! Dawa
ya majitu ni uji. Walinieleza kuwa iwapo majitu yatawahi
25
kutembea nyumbani kwa mwanakijiji yeyote ayaeleze
kuwa atayapikia uji, hayatataka kuondoka hapo.
Yatatulia kabisa. Wazee hao walinieleza kuwa majitu
hupenda uji kuliko chochote kile.
Popote yanaposikia uji huwa yenye upole na
subira. Wanabintuke, tutakapotoka kwenye kikao
hiki tuuzingatie ushauri huu. Majitu hupenda sana uji
wa muhogo. Ninajua wengi huwa wanatumia uji wa
wimbi hapa kijijini hasa ikizingatiwa kuwa tumekuwa
tukipanda wimbi kwa wingi. Kwa kunusa tu harufu ya
uji wa mhogo majitu yatatoka mafichoni ili kuitafuta
nyumba mnamopikwa uji huo. Mnaweza kuyatilia
dawa kali kwenye uji ama mkayamwagia uji moto ili
kuyaangamiza.
Boma langu ndilo lililo karibu na msitu wa
Bintudamu. Kwa hivyo mke wangu atakuwa wa kwanza
kuweka ushauri huu kwenye matumizi. Nina uhakika
tukiuzingatia ushauri wa wazee wa kijiji cha Bantu
tutayamaliza majitu haya. Asanteni kwa kunisikiliza,
Bwana Bintu alimaliza.
Baada ya muda mfupi kila mwanakijiji alijiondokea
akiwa na matumaini moyoni. Mkuu wa kikosi cha
askaripori pia alijiondokea akiwa na la kuwaeleza
wenzake ambao hawakufika kwenye mkutano huo.
26
Sura ya Tano
Siku ya tano kwenye nyumba ya Bwana Bintu
shughuli zilindelea kama kawaida. Faida, Matu na
Bahati walikuwa hawajaamka kutoka vitandani mwao.
Bwana Bintu pia alikuwa usingizini. Bintutu, mke wake
Bintu aliamka mapema. Alikuwa akiupika uji wa muhogo.
Harufu ya uji huo ilikuwa imeenea kote kijijini kama
moto kwenye kichaka kikavu. Muda mfupi baadaye,
Bintutu aliusikia mbisho mlangoni. Ulikuwa mbisho
mzito ulioutikisa mlango kama dhoruba. Ulikuwa
mbisho uliomshtua sana. Haukuwa mbisho wa kawaida.
Ulimtia wasiwasi wa mwasi.
Mbisho huo ulirudiwa kwa mara ya pili na ya tatu.
Mbisho huo uliandamwa na sauti nzito kama radi
elfu moja. Hii ni sauti ya jitu, Bintutu alijiambia.
Binadamu hawezi kuwa mbisho kama huu, Bintutu
alizidi kujisemea.
27
Ewe mwenye boma, utaufungua mlango huu
au tukufunze kilichomnyoa kanga manyoya? Sauti
ilitetemesha. Leo tutakufunza adabu! Sauti iliendelea.
Huku mbisho huo ukiendelea, Bintutu alikuwa
ameipiga hesabu ya jinsi ambavyo angalikabiliana na
majitu hayo. Si neno! Majitu hupenda uji! Uji ninao,
Bintutu alijitia ushujaa. Alipiga hatua mbele kuelekea
mlangoni na kuufungua. Alipoufungua, aliwaona
wanaume watatu.
Majitu yalikuwa yamejigeuza na kuchukua maumbo
ya wanaume. Sifa zao zilikuwa zinajulikana kote kijijini
Bintuke. Yalifika yakiwa wanaume bandia!
Wanaume hao walikuwa watanashati. Walitabasamu
huku meno yao meupe pe yakijitokeza. Walikuwa
wamezivalia suti nyeusi tititi kama makaa. Suti zao
ziliwafaa na kuwachukua kama kitanda kilichopata
mkeka. Nywele zao ziliukamilisha utanashati wao.
Macho yao yalikuwa na ukubwa wa wastani. Hayakuwa
madogo kama chawa wala makubwa kama gololi za
nyati.
28
Karibuni nyumbani mwetu wageni wapendwa.
Mmefika kwa wakati mzuri sana. Uji u karibu kuiva,
Bintutu aliyakaribisha majitu. Yupo kati yenu
asiyeupenda uji? aliuliza Bintutu.
Heri tukakosa vyakula vingine kuliko kuukosa uji,
jitu moja lilisema kwa sauti nzito.
Bila shaka, mengine yaliongeza kwa sauti ya
mtetemeko.
Haya basi, uji utakuwa tayari baada ya muda mfupi.
Uji wa wimbi ni mtamu sana. Nimeupika uji mwingi.
Nyote mtakunywa mpaka mshibe. Raha iliyoje hiyo?
Bintutu aliyaambia majitu.
...Walitabasamu huku meno yao meupe pe yakijitokeza...
29
Majitu hayo yaliposikia hivyo, yalionekana kutia
subira usoni. Yaliamini kuwa subira huvuta heri. Yaliketi
kwenye makochi na kutulia tuli. Kila baada ya dakika
chache yalionekana yakipiga miayo. Yalipanua
vinywa vyao huku yakizibiruabirua pua zao. Yaliketi
kwenye sofa kama wenyeji. Yaliigeuza nyumba ya
Bwana Bintu kuwa yao. Mara jitu moja lingalisimama
na kujiangalia kwenye kioo kilichokuwa ukutani. Mara
liliugeuzageuza na kuuchezeachezea ulimi kinywani.
Wakati mwingine yaliangua kicheko cha radi. Huko
jikoni Bintutu alionekana kuuchochea moto kwa haraka
na kwa bidii. Moto nao ulirindima chini kwa chini huku
uji ukichemka kwa nguvu.
Wakati mwingine majitu yalipiga gumzo kwa lugha
yao. Bintutu hakuielewa katu. Majitu yalipoingia yalikuwa
yakitumia Kiswahili. Bintutu alipotaka kuyazungumzia
majitu, alitumia Kiswahili. Yalizungumza Kiswahili kwa
matamshi mazuri. Hii ndiyo lugha iliyompatanisha Bintutu
na wageni wake! Kila alipoona yameanza kuonyesha
ishara ya uchovu, aliyatuliza kwa kuyaambia, Kidogo
tu! Uji utakuwa mezani hivi punde!
Mama itakubidi uharakishe kama sivyo tukugeuze
kitoweo! jitu moja lilimwambia. Jibu hilo lilimfanya
Bintutu kutokwa na jasho.
30
Mara Bintutu aliwasikia watoto wake wakiongea
kutoka kitandani. Kwa hofu aliwaambia kwa sauti ya
ukali, Wageni wetu hawapendi kelele. Nyamazeni.
Nao walinyamaza kabisa. Walimtii mama yao. Wakati
wote huo, Bwana Bintu hakujua kilichokuwa kikiendelea
nyumbani mwake. Mke wake naye hakutaka kumkatizia
usingizi wake. Alijua kuwa alikuwa na uchovu kutokana
na safari yake kijijini Bantu. Hata hivyo, mbinu za
kuyaangamiza majitu hayo alikuwa nayo. Alikuwa na
dawa yao mkononi. Dawa aliyoivumbua mumewe. Dawa
waliyoitumia wazee wa kijiji cha Bantu kuyaangamiza
majitu. Pia, alikuwa ashapata mbinu ya kuwaondoa
watoto wake kwenye hatari hiyo ya majitu.
Uji umeiva sasa. Wageni wangu tafadhali kuweni
tayari, Bintutu aliyaambia majitu.
Majitu yale yalionekana kuchangamka kuliko hapo
awali. Tulikuwa tayari kitambo, jitu moja lilimwambia
Bintutu.
Yalisonga na kuizingira meza. Kabla ya Bintutu
kukiinjua chungu kile cha uji, aliliona jitu moja likiikazia
macho picha ya watoto wake iliyokuwa imeangikwa
ukutani. Liliitazama kisha likatikisa kichwa. Mama uji
huu utatutosha kweli? jitu hilo liliuliza.
Ninadhani utawatosha, Bintutu alilijibu.
Sawa, usipotutosha tutakuua wewe na watoto wako
tuwale ndio tushibe. Mtakuwa vitoweo vyetu mara
31
moja, jitu hilo lilingaka tena.
Nina uhakika utawatosha. Usipowatosha,
nitawapikia mwingine. Nyumbani humu tunawapenda
wageni, Bintutu alijibu.
Hata ingawa Bintutu alijikaza kuwahudumia wageni
wake, kauli ya jitu lile kuwa lingewaua wanawe iliendelea
kumsumbua akili.
Ninaomba nimtume mtoto mmoja akaniletee
vikombe. Jirani alituomba vikombe vyetu jana akiwa na
wageni na hakuvirudisha, Bintutu aliyaomba majitu.
Faaaida! Faaaida eeeh! Njoo hapa haraka uaniletee
vikombe! Bintutu alimwita Faida kwa sauti.
Kufumba na kufumbua, Faida alifika pale kutoka
kitandani. Bintutu kwa sauti ya chini alimwambia Faida,
Mwanangu, usirudi hapa! Haya ni majitu. Ukirudi
yatakuua! Toroka ujifiche kabisa hadi yatakapoondoka.
Bintutu alihakikisha majitu hayo hayakusikia. Laiti
yangalisikia, angalijipata mashakani!
Faida aliondoka mbiombio. Hakurudi! Watoto wa
siku hizi hawatumiki. Ukiwatuma hawarudi, Bintutu
alisema kwa kujitia hasira.
Kwa sasa subira ilikuwa imeyaisha kabisa majitu.
Mama mtu, zimebaki dakika tano ujijutie, jitu moja
lilitoa kauli.
Maaatu, Baaahati eeeh! Njooni niwatume. Njooni
32
niwatume haraka, Bintutu aliwaita wanawe. Nao
walifika mara moja. Mfuateni Faida mmwambie alete
vikombe haraka. Wageni wetu wamehisi njaa sana,
aliwaamrisha Matu na Bahati. Lakini kwa sauti ya
chini aliwaambia, Wanangu, msirudi hapa! Haya
ni majitu. Mkirudi yatawaua! Torokeni mjifiche hadi
yatakapoondoka!
Bintutu alikuwa mwenye hekima chungu nzima.
Alielewa fika kwamba angaliwaita watoto wake wote
kwa pamoja, yale majitu yangaliutambua ujanja
wake. Vilevile, angaliziamsha tamaa zao hasa
ikizingatiwa kuwa waliipenda nyama ya binadamu.
Kwa upande wake asingeweza kutoka. Majitu yalikuwa
yamemwekea sheria kali. Yalikuwa tayari kummeza
endapo angalijaribu kukaidi amri zao. Alikuwa macho
asije akajipata pabaya.
Upo wakati jitu moja lilimwambia, Mama usijaribu
kutoka nje. Kaa humu hadi pale utakapohakikisha
tumeshiba! Ukijaribu kutoka nje utakiona.
Faida, Matu na Bahati walikuwa hawako tena. Wageni
wangu jamani, naona watoto hawa wamechelewa.
Niwafanyaje wageni wangu jamani? Sina vikombe
vya kuwatilia uji, Bintutu alisema kwa sauti ya upole!
Alikuwa yuajitia hamnazo tu ili majitu yale yasije
yakapoteza subira. Majitu hayakujibu. Yaliendelea tu
kumtazama kwa tamaa.
33
Tutatumia mbinu za haraka almradi uji huu
upate kufika matumboni mwenu. Mmehisi njaa
sana! Hatutaendelea kuwasubiri watoto hawa huku
mkiendelea kuumia kwa njaa. Ninawaomba mviweke
vichwa vyenu pamoja kisha mvifungue vinywa nipate
kuwamwagia uji huu kidogo kidogo ndani ya vinywa
vyenu.
Kwa sababu ya tamaa majitu yalitii! Uji huo ulikuwa
umetokota hadi ukatokoka. Ulikuwa umechemka kabisa.
Bintutu alichukua kitambaa kilichochanikachanika.
Alikikata mara kwa vipande viwili. Alikishikilia chungu
kile kwa nguvu asije akachomeka. Alikiepua. Chungu
hicho kilikuwa na mdomo mkubwa. Aliyaambia majitu.
Wageni wangu wapendwa, ninaomba muwe tayari
sasa.
Yalipanua vinywa vyao. Mate yaliwadondoka huku
yakipiga miayo. Bintutu alikiinua chungu kile juujuu
kwa nguvu. Alihesabu moja mbili tatu kisha akaanza
kuumwaga uji ule kwa mfululizo.
34
Uji ule ulikipata kila kiungo cha majitu yale barabara.
Si macho, si pua si midomo. Hayakutarajia hayo.
Bintutu naye hakusita. Aliendelea kuyamwagia uji hadi
pale alipohakikisha yamechomeka hadi yakaishiwa
na nguvu. Hapo ndipo alipovifunga vichwa vyao kwa
kamba na kuvigongesha kwenye ukuta pa! Yalilia
kwa sauti ya kutetemesha. Kisha aliviingiza vichwa
vyao kwenye chungu moja baada ya jingine. Vichwa
vilichomeka, vikavimba hadi vikapasuka.
Yalipanua vinywa vyao...
35
Sura ya Sita
Mpasuko huo ulimwamsha Bwana Bintu. Aliruka
kutoka kitandani na kukimbilia sebuleni. Aliyapata
majitu yale yakiwa katika hali mahututi. Alichukua rungu
akaanza kuyapondaponda kama mahindi kwenye
gunia. Hakujali iwapo yalikuwa yamekufa au la! Bintu
na Bintutu walianza kuimba na kushangilia.
“Li! Li! Li! Tumeyaua majitu ya msitu wa
Bintudamu!
Tumeyaua ua ua ua jamani, tumeyauaua!
Tumeyauaua mazimwi, tumeyauaua
jamani!
Tumekuwa mashujaa, aiyaiyaiya!
Aiyaiya shujaa, aiyaiyaiya!
Huree! Hure eeeh!
36
Walikuwa wamevunja rekodi pale kijijini Bintuke.
Waliyaua majitu yaliyokuwa yamewatesa wanakijiji
kwa miaka na mikaka. Yalikuwa yamewala watu
wasiohesabika. Yaliwaua mifugo chungu nzima.
Yaliiharibu mimea mingi. Yakasababisha njaa kubwa
kwa wanabintuke. Hiki kilikuwa kitendo cha kihistoria
kutoka kwa Bintu na mkewe.
Mpasuko wa vichwa vya majitu yale na kelele za
nyimbo za Bintu na Bintutu, viliwazindua wanakijiji
wa Bintuke. Kila mmoja alikuja mbio pale nyumbani
kwa Bwana Bintu. Walikuja mbio kujua kilichokuwa
kimetendeka. Boma la Bwana Bintu lilifurika sisisi na
watu. Wapo waliotoka karibu na pia waliotoka mbali.
Kila mtu alikuwa akiushangilia ushindi wa Bintu na
Bintutu. Wanawake walishangilia sana hasa ikizingatiwa
Bintutu alikuwa mwanamke. Alikuwa ameziinua hadhi
za wanawake kijijini. Wanawake hao walimbeba Bintutu
juujuu huku wakimwimbia nyimbo za kuushangilia
ushindi wake. Wanaume kwa upande mwingine pia
hawakuachwa nyuma. Walimshangilia Bwana Bintu
huku wakimbeba juujuu kama makuti ya mnazi.
Nyimbo zilisikika kila mahali bomani mwa Bwana Bintu.
37
Umekuwa ujasiri, kwetu sisi wanawake,
Kila mtu atakiri, si kilema mwanamke,
Yafika hii fahari, kabla mume afike,
Majuto yameyafika, majitu yalotutesa.
Bintutu ni mjasiri, licha yake kuwa mke,
Tungali tunakariri, ushindi hadi tuvuke,
Tutalima maekari, tuvune hapa Bintuke,
Majuto yameyafika, majitu yalotutesa.
Faida, Matu na Bahati walikuwa washarejea
nyumbani kwao. Walikuwa wamezisikia nyimbo
Walimshangilia Bwana Bintu huku wakimbeba juujuu...
38
zilizokuwa zikiimbwa na kuenea kote kijijini. Walifika
kwao nyumbani na kuifutilia sinema hiyo ya kushangiliwa
kwa wazazi wao kwa kuyaua majitu.
Umati mkubwa ulikuwa umefika kwenye boma la
Bwana Bintu. Kila mtu alikuwa amejawa na furaha
riboribo moyoni mwake. Mateso ya majitu yalikuwa
yamewaondokea.
Mzee Bintu alikuwa amemtumia mkuu wa kikosi cha
askaripori ripoti ya kuuliwa kwa majitu yale. Alimwomba
kufika kwenye kikao cha kuitawaza familia ya Bwana
Bintu. Sherehe ya kuwatuza mataji ya kuwaletea
Wanabintuke matumaini katika maisha tena.
Mzee wa kijiji Bwana Chatu na mkuu wa askaripori
walisimama mbele ya umati huo na kuanza kuuhutubia.
Wanabintuke hoyeeeee! Wanabintuke hureeee!
Naam, leo ni siku ya furaha kwa kila mmoja wetu.
Majitu yaliyotusumbua kwa muda mrefu yameuliwa.
Ningependa kuwaelezeni kuwa majitu si sehemu ya
wanyamapori bali ni mashetani. Hii ndiyo sababu ya
kitengo chetu cha ulinzi wa wanyamapori kikakubali
yauliwe. Hakuna mtu anayekubaliwa kuwaua
wanyama wetu kwa kuyasingizia majitu. Wanyamapori
ni kivutio cha watalii na ni sehemu ya uti wa mgongo
wa uchumi wetu. Kwa hayo machache ninawatakia kila
la heri maishani mwenu. Nitamkaribisha Mzee Chatu
39
awazungumzie ninapoondoka mimi. Karibu mzee,
mkuu wa kikosi alimaliza.
Ninawaomba nisiuchukue muda mrefu kuzungumza
maanake wakati ni ukuta, Mzee Chatu alianza.
Mnavyoona jua li karibu kuiaga miti. Jukumu langu
hapa ni kuishukuru familia ya Bwana Bintu na hasa
mke wake Bintutu. Wameyaua majitu ambao yalikuwa
yametusumbua sana.
Wanakijiji wenzangu, mnajua vizuri kuwa majitu
haya hayajakuwa tisho kwa usalama wetu pekee bali
pia mifugo wetu. Miaka mitano iliyopita, kijiji chetu cha
Bintuke kilikuwa chenye utajiri mkubwa. Kilikuwa na
utajiri wa mifugo na mimea. Watalii walikuwa wakitoka
mbali kuja kukitembelea kijiji chetu. Wafanyabiashara
walitoka mataifa mengine kuja kuyanunua matunda na
mazao ya aina mbalimbali katika kijiji kiki hiki. Bintuke
kilikuwa kijiji kilichosifika karibu na mbali. Tazama leo
hii jinsi majitu haya yalivyotusabibishia hasara kubwa.
Mungu ana mpango wa kuturejesha tulikokuwa.
Yameangamiza kabisa mimea iliyojaa mashambani
mwetu. Nina uhakika mazao yetu yataongezeka mara
dufu, Mzee Chatu alikoma kidogo.
Kabla ya kuwavisha Bwana Bintu na Bintutu mataji
ya ushujaa, Chatu aliendelea, litakuwa jambo la
hekima kuichoma miili ya majitu haya. Kulingana na
40
utamaduni, majitu haya yanapaswa kuchomwa kabisa.
Yachomeke kabisa na majivu yao yapelekwe na
kutupwa mtoni. Mili yao ikiendelea kukaa hapa huenda
mikosi yao ikachipuka tena. Nishafahamishwa na
vijana niliowateua kuwasha moto kuwa moto u tayari,
Bwana Chatu aliueleza umati.
Wakati huo vijana wale walikuwa wameiingiza mili ya
majitu kwenye gunia na kuimwagia mafuta fulani. Umati
wote ulielekea kwenye eneo la kuyachomea majitu
yale. Majitu yale yalirushwa motoni yakachomeka hadi
yakabaki majivu pekee. Majivu yao yaliwekwa kwenye
magunia na kutupwa kwenye mto. Wanabintuke
waliamini kwamba mto huo ungeliyasafirisha majivu
hayo na mikosi ya majitu hayo mbali na kijiji chao.
Shughuli ya uchomaji wa majitu zilipokwisha, Bwana
Chatu aliendelea kuzungumza. Wanabintuke hoyeee!
Wanabintuke hoyeee! Mzee Chatu alirejea tena.
Bwana Bintu na Bintutu ninawaomba msonge mbele
tafadhali, Mzee wa kijiji Bwana Chatu aliwaomba.
Nitaituza familia hii vitu vitatu: mikuki, ngao na ngozi
ya simba. Mikuki mitano ni kwa kila mwanafamilia
wakiwamo watoto wao. Zaidi ya hapo nimeitawaza
familia ya Bwana Bintu kuwa familia ya kishujaa.
Mzee Chatu alipomaliza kuwatuza, nyimbo za kishujaa
zilihanikiza. Nyimbo hizo ziliimbwa na umati uliofika
pale.
41
Utuzaji ulipofikia kikomo, hafla na shamrashamra
kubwa ziliandaliwa. Fahali wachache waliobaki kijijini
walichinjwa. Kila mwanakijiji alikula kadri alivyoweza.
Wapo wanakijiji walioondoka baada ya majitu yale
kuchomwa maanake hiyo ndiyo iliyokuwa haja yao
kubwa. Waliondoka na kuenda kusherehekea makwao.
Waliobaki walikula ghaya ya kula. Ilikuwa siku ya
siku. Siku ya ndovu kumla mwanawe kwa wanakijiji
wa Bintuke.
...nyimbo za kishujaa zilihanikiza...
42
Kabla ya wanakjiji kuondoka, Bwana Bintu hakukosa
la kusema. Enyi wanakijiji wenzangu, mke wangu na
wanangu, kwa kweli mke wangu ametuletea ushindi na
baraka nyingi. Yote yamewezekana kutokana na nguvu
zake Mwenyezi Mungu. Imeonyesha wazi kuwa katika
jamii mwanamke ana uwezo, nafasi na maendeleo
sawa na mwanamume. Ninawaombea heri kwenye
shughuli zenu za kila siku. Shukrani! alisema Bintu
huku wanakijiji wakimshangilia.
Wanakijiji waliondoka mmoja baada ya mwingine.
Baada ya majuma mawili hivi kupita, mvua ilianza
kunyesha. Ilikuwa mvua nyingi. Usalama ulikuwa
umerejea kijijini Bintuke. Wanakijiji walifanya shughuli
zao wakati wowote iwe usiku iwe mchana. Hawakuogopa
kuvamiwa na majitu tena. Wanakijiji waliingia
mashambani mwao wakalima na kupanda mimea kwa
wingi. Mimea ilistawi na kushamiri. Mazao na mavuno
yalikuwa yameanza kujaa kwenye maghala.
Wafugaji waliwafuga mifugo kwa wingi. Maziwa
yalikuwa yamejaajaa kote. Wanakijiji walirudiwa na
afya nzuri. Maradhi hayakuwa na nafsi kwenye kijiji
cha wanabintuke. Hawakuogopa mimea na mifugo wao
kushambuliwa na majitu tena. Miti ilipandwa kwa wingi
ili kuzuia mmomonyoko wa udongo. Watoto walienda
shuleni bila woga wala kusindikizwa na wazazi
43
wao. Walisoma hadi vyuo vikuu. Furaha iliyoje kwa
Wanabintuke!
Familia ya Bwana Bintu ilipata heshima ya kudumu
kutoka kwa wanakijiji. Hii ni familia ya kishujaa. Kwa
sasa, kijiji cha Bintuke ni miongoni mwa vijiji vyenye
utajiri mwingi wa kilimo, barabara, umeme, elimu na
usalama. Maendeleo ya kila aina yamerejea huku.
Watalii hutoka mbali kuja kukitalii kijiji hiki.
44
Maneno mapya
ambulia patupu kosa kufaulu
askaripori askari wanaolinda misitu na
wanyama wa mwituni
ghaya kwa wingi; sana
hadhi sifa ya kumfanya mtu aheshimike
jando mahali wanapotahiriwa watoto
wavulana; chari
jasiri mtu asiyeogopa; shujaa
jitihada bidii
jitu (majitu) kiumbe wa kufikirika mwenye umbo
kubwa la kutisha
kifunguamimba mtoto wa kwanza kuzaliwa;
mwanambee
kiinuamgongo malipo ya uzeeni au kustaafu
kikosi kikundi
kitindamimba mtoto wa mwisho kuzaliwa;
kichinjamimba, kifungamimba,
mziwanda
kukaidi kataa kufuata; kosa kutii
ilistawi kua au mea vizuri;
kuwatahadharisha kuwaonya; kuwakanya
kuwatuza kuwapatia zawadi
kuyawinda kuyafukuza
45
makazi mahali wanapoishi viumbe
mara dufu mara mbili
mbisho sauti ya kukigonga kitu kama vile
mlango
ngariba anayetahirisha vijana
ngaka kuongea kwa nguvu
piga miayo fungua mdomo bila hiari na kupitisha
hewa nje sababu ya uchovu, njaa au
usingizi
podo mfuko wa kuhifadhia mishale;
pongono, ziaka, riaka
shamiri sambaa au enea sehemu kubwa
suluhu jibu la shida
teua chagua anayefaa
wakeketaji mtu anayetahiri watoto wasichana
yakizibiruabirua geuza upande
yaungue yachomeke
46
Methali
1. Koti la mzee halikosi chawa - wazee hawakosi
ushauri
2. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu - watu
wanapofanya shughuli kwa kushirikiana hufaulu
3. Hewala haigombi ni vizuri kuwa na heshima kwa
wenzako; heshima si hutumwa
4. Heshima si utumwa wala hainunuliwi - ni vizuri
kuwaheshimu wenzako au wengine
5. Subira huvuta heri ili kufanikiwa ni lazima
uvumilie
6. Wakati ni ukuta huwezi kuzuia muda kuisha;
tumia wakati vizuri
7. Kinga na kinga ndipo moto uwakapo watu
wanaposhirikiana baadaye hufaulu; umoja ni nguvu
utengano ni udhaifu
8. Mchumia juani hulia kivulini anayejitahidi
hufaulu baadaye
9. Chelewa chelewa utamkuta mwana si wako
mtu akichelewa kufanya jambo hatafanikiwa
10. Lisilo na budi hutendwa jambo linalostahili
kutekelezwa ni lazima litekelezwe wakati wake
unapofika
11. Wengi wape watu wengi wanapokubaliana katika
uamuzi ni muhimu kujiunga na uamuzi wao
12. Mtoto akibebwa hutazama kisogo cha mama
yake ni vizuri mtoto kufuata ushauri wa wakubwa
wake
47
13. Jihadhari kabla ya hatari zuia jambo au shida
kabla haijakufika
Tashbihi
1. Waliwapenda watoto wao kama mboni za jicho
Waliwapenda sana
2. Mzima kama kigongo - mwenye afya
3. Alinyamaza kama maziwa kitomani - tulia kabisa
bila kuongea
4. Wasiwasi wa mwasi - wasiwasi mwingi
5. Nzito kama radi elfu moja - sauti kubwa na yenye
ukali
6. Imeenea kote kijijini kama moto kwenye kichaka
kikavu - imemfikia kila mtu kijijini
7. Ulioutikisa mlango kama dhoruba - tikisa kwa
nguvu
8. Nyeusi tititi kama makaa nyeusi kabisa
9. Kuwachukua kama kitanda kilichopata mkeka
kuwafaa kabisa
10. Kicheko cha radi kicheko kikubwa
11. Hayakuwa madogo kama chawa wala makubwa
kama gololi za nyati si madogo wala makubwa
sana
12. Kuyapondaponda kama mahindi kwenye gunia
kuyapiga kwa nguvu na hasira zote
13. Wakimbeba juujuu kama makuti ya mnazi
kumchukua juu kwa juu bila kumwekelea chini;
hobela hobela
48
14. Nadra kama barafu ya kukaangwa kutopatikana
kwa urahisi
15. Walifurahia ndani kwa ndani kama vitoto vya
shule ya chekechea vilivyofuzu kuijiunga na
darasa la kwanza walikuwa na furaha nyingi
16. Haraka haraka kama umeme kufanya jambo
upesi upesi
Semi
1. Hawakufua dafu - hawakufaulu
2. Ziliambulia patupu - hazikufaulu
3. Ninamuunga mkono - ninakubaliana naye
4. Ashakipitia kisu cha ngariba - kutahirishwa;
kupashwa tohara
5. Yalipiga gumzo - kuzungumza ili kupitisha wakati
6. Siku ya siku; siku ya ndovu kumla mwanawe
siku kuu; siku ya sherehe
7. Yameota meno - kuwa na ujeuri kupita kiasi
8. Kokwa hadi ngozi - juana kabisa
9. Mikono mirefu - mwizi/wezi
10. Umepigwa marufuku - umekataliwa/umepuuzwa
Majina ya makundi/nomino jamii
1. Kikosi cha askaripori - kikundi cha askari; askari
wengi
2. Marobota na maburungutu ya nguo - nguo nyingi
kwa pamoja
49
Tanakali za sauti
1. Hawakuyapata ngo! - waliyakosa kabisa
2. Midundo ya dududu! Dududu! - milio ya ngoma
3. Meupe pe - meupe kabisa
4. Lilifurika sisisi - kujaa kwa watu wengi
Takriri
1. Unyo kwa unyo - kwa mfuatano; nyuma kwa nyuma
2. Mchana kutwa na usiku kucha - mchana na usiku
wote
3. Amejihami kwa jino na ukucha - kuwa na silaha
kali kali
4. Salama salmini - bila shida
5. Hamu na hamumu - kutamani sana
6. Hobelahobela - juu juu; haine haine
7. Kufumba na kufumbua - kwa muda mfupi; punde
si punde
8. Jino na ukucha kujitahidi kwa njia zote
Tabaini
1. Si macho si pua si midomo - kwenye macho,
pua na midomo; sehemu zote zilizotajwa
2. Mvua ingalinyesha, hata tone moja
lisingaliuramba mchanga watu walikuwa wengi
sana
50
Maswali
1. Kijiji cha Bintuke kilikuwa kimevamiwa na nini au
nani?
2. Majitu yaliishi kwenye msitu gani?
3. Familia ya Bwana Bintu ilikuwa na jumla ya watu
wangapi? Wataje kwa majina.
4. Kwa nini wanao Bintu na Bintutu hawakukeketwa?
5. Ni hasara zipi walizozipata wanabintuke kutoka kwa
majitu?
6. Mzee wa kijiji cha Bintuke aliitwa nani?
7. Siri ya kuyaua majitu ilipatikana kutoka kwenye kijiji
gani?
8. Ni nani aliyeyaua majitu?
9. Kwa nini kila mwanakijiji alifurahia maafa ya majitu
hayo?
10. Hadithi hii inatufunza nini?