
17
Kengele ilipolia, wanafunzi wote walikimbia kwenye
gwaride. Sofia, Helena, Mambo na Lemayan tayari walikuwa
washafika. Walitangulia ili kuitayarisha bendera. Wakati wa
kupandisha bendera ulipowadia, kikosi hiki cha wanaskauti
kilisimama mbele ya mlingoti. Sofia ndiye aliyeibeba bendera.
Mambo, Helena na Lemayan walisimama tisti nyuma yake.
“Eeh Mungu nguvu yetu,” Lemayan alianzisha wimbo wa
taifa kwa sauti. Wanafunzi wote walimwitikia Lemayan
kwa sauti.
“Ilete baraka kwetu…”
Waliimba wimbo wa taifa huku Mambo akiipandisha bendera.
Kisha, mwalimu aliyeshika zamu alitangaza kwa sauti,
“Wanaskauti wetu watatuimbia wimbo wa kuisifu bendera
yetu. Sikilizeni kwa makini ili muimbe nao tena baada ya
wao kumaliza.”
Sofia, Helena, Mambo, na Lemayan waliimba wimbo wa
kuisifu bendera kwa sauti.
Bendera yetu ya Kenya yapendeza,
Bendera yetu ina rangi nzuri,
Nyeupe, nyeusi, nyekundu, kijani,
Hizo ndizo rangi za bendera yetu.
Rangi nyeupe yatangaza amani,
Rangi nyeusi ni ya ngozi zetu,
Rangi nyekundu ni damu ya ukombozi,
Rangi ya kijani ni mashamba yetu.
Wanafunzi wote waliimba wimbo huu pamoja na kikosi hicho
cha wanaskauti. Watu walipofumukana ili kwenda darasani,
baadhi ya wanafunzi waliendelea kuimba wimbo huo kwa
sauti za chini. Wengine waliuimba vizuri na wengine vibaya.