Bahati ya Kezo
na Hadithi Nyingine
Yahya Mutuku
Bahati ya Kezo na Hadithi Nyingine
Kimechapishwa na Queenex Publishers Limited
S.L.P 56049-00200, Nairobi, Kenya.
Simu: 0727 794 498, 0715 808 200
Baruapepe: info@queenexpublishers.co.ke
queenexbooks@gmail.com
Tovuti: www.queenexpublishers.co.ke
© Yahya Mutuku, 2022
Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kuiga, kunakili, kupigisha
chapa, kutafsiri au kutoa kitabu hiki kwa jinsi yoyote ile bila
idhini kwa maandishi ya Queenex Publishers Limited.
ISBN:
Chapa ya kwanza 2022
1
Kito na Zawadi ya Ajabu
2
Miaka mingi iliyopita, paliondokea familia moja iliyoishi karibu
na msitu ulioitwa Makongoni. Kiongozi wa familia hiyo aliitwa
Mzee Mwema. Mke wake naye aliitwa Bi.Amina. Mzee Mwema
na Amina walijaaliwa watoto wengi. Walikuwa watoto wenye
sura nzuri sana. Katika nchi nzima ya Nyota, hakukupatikana
watoto wenye sura nzuri kama wale. Mzee Mwema na mkewe
walikuwa maskini hohehahe wasio na mbele wala nyuma. Mzee
Mwema alifanya kazi ya kushona kamba auze apate riziki naye
mkewe alitegemea kulima mashamba ya wanakijiji ili apate pesa
za kununua chakula.
Nyumba waliyoishi ilikuwa mbovu sana. Ilikuwa nyumba ndogo
iliyojengwa kwa fito na tope. Paa la nyumba hiyo liliezekwa
mabati mabovu. Nyakati za msimu wa mvua, nyumba hiyo ilivuja
sana. Shida zilikuwa nyingi katika familia hiyo. Kuna siku wazazi
walikosa pesa na wakalazimika kulala njaa. Wanawe Mzee
Mwema walikosa mavazi mazuri na kuvalia mararu, yaani nguo
mbovu zilizoraruka na kujaa viraka. Ilikuwa vigumu kwa watoto
hao kupata wazee wa kuwafundisha kwa kuwa baba na mama
hawakuwa na pesa za kulipa wapate mafunzo kutoka kwa wazee.
Siku moja, Mzee Mwema aliota ndoto. Katika ndoto hiyo, aliona
mwanawe mmoja akimfanya tajiri mkuu duniani.Ajabu ni kuwa
hakuuona uso wa mtoto aliyetokeza na kusimama mbele yake.
Ndoto hiyo ilimshtua sana. Hakuiamini.Alizinduka akitokwa na
jasho jingi kila sehemu ya mwili.
“Mke wangu, nimeota ndoto ambayo sijawahi kuota tangu
nizaliwe, alimwelezea mkewe ndoto hiyo.
Bi. Amina alipoisikiliza ndoto hiyo, aliangua kicheko, akacheka
hadi machozi yakamtoka.
3
“Mke wangu, nimeota ndoto ambayo sijawahi kuota...
4
“Mume wangu, leo hakika umenichekesha sana. Zipo ndoto
za kuotwa lakini nyingine zina uongo mwingi sana. Ati uliona
mmoja wa wana wetu akitufanya matajiri wakuu duniani! Hiyo
ni ajabu kubwa. Mimi mkeo nishaamini kuwa maisha yetu ya
umaskini yalishapangwa na Mwenyezi Mungu. Siamini kuwa kuna
uwezekano kwamba siku moja tutakosa kuwa na shida.Tumeishi
na matatizo mengi hadi yamekuwa sehemu ya maisha yetu, Bi.
Amina alielezea.
“Si neno mke wangu. Si neno hata usiponiamini, Mzee Mwema
alisema.
“Najua ndoto ya kawaida na ndoto isiyo ya kawaida. Nina
imani kuwa ipo siku ukweli wa ndoto hiyo utajitokeza waziwazi.
Wahenga walisema, Mungu si Athumani. Hatuwezi kuishi katika
hali hii ya umaskini maisha yetu yote hapa duniani, Mzee Mwema
alimjibu mkewe aliyeendelea kuumia mbavu zake kwa kucheka
sana.
Siku moja, Mzee Mwema alirejea nyumbani kutoka mbali kutafuta
riziki.Alikuwa amechoka sana.Alimpata mkewe akipika wali wa
nazi. Wanawe wengi walikuwa wamekaa kuizunguka sufuria
yenye wali iliyokuwa ikichemka jikoni.Walikuwa na njaa sana.
Tangu asubuhi siku hiyo, hawakunywa kiamshakinywa na wala
hawakula chakula cha adhuhuri.Waliomba wali huo uive haraka
ili waweze kula na kuifukuza njaa iliyokuwa ikiwatesa kwelikweli.
Mzee Mwema ilivyokuwa desturi aliwakumbatia wanawe na
baada ya kujuliana hali na mkewe, akaingia bafuni na kuoga.
Alioga na kuondoa uchafu na uchovu uliokuwa mwilini. Mara
nyingi alipooga, alipenda kuketi barazani kupigwa na upepo.
Akiwa pale barazani, Mzee Mwema alisikia sauti kama ya farasi
akija upande wa nyumba yake. Sauti ya hatua za mwendo wa
5
farasi zilikaribia hadi kwenye lango. Baada ya muda usio mrefu,
alisikia mtu akibisha mlango.Alisimama na kwenda kumfungulia
aliyebisha.Alipata alikuwa na mgeni kutoka nchi za mbali. Mgeni
huyo alikuwa mwanamume aliyekonda kupindukia.Alivalia mavazi
machafu yenye vumbi na yaliyorarukararuka.Alionekana mwenye
shida nyingi mno. Alishindwa kutembea ikabidi Mzee Mwema
kumsaidia kutembea.
“Naomba…Naomba maji na cha..chakula. Na..naomba ma..maji
na cha..chakula, mgeni alisema kwa maumivu.
Mzee Mwema alimsaidia kwa kumtembeza polepole hadi akafika
katika nyumba. Alimchukulia kiti kisha akamwamuru mkewe
kupasha maji moto. Kila mmoja katika familia hiyo alishangazwa
na mgeni huyo. Maji yalipokuwa tayari, Mzee Mwema alimsaidia
mgeni kwa kumpelekea maji bafuni. Mgeni alioga hadi akawa safi
kabisa. Mzee Mwema aliyaweka mbali mavazi mabovu ya mgeni
kisha akachukua suruali yake nzuri akampa avalie.
“Shukrani ndugu yangu. Hakika wema unaonitendea sitawahi
kuusahau maishani, mgeni alimwambia.
Wakati huo, Mzee Mwema aliingia katika chumba cha ndani na
kupitia mlango wa nyuma. Dakika kumi na tano baadaye alirudi
akiwa mwingi wa furaha.
Bi.Amina aliwapakulia chakula kidogo wanawe jioni hiyo.Alichukua
sinia na kuijaza wali kisha akamkaribisha mgeni. Mgeni aliyekuwa
na njaa ya siku nyingi, alikula hadi akashiba.Alipewa maji akakata
kiu na kushusha pumzi.
Mzee Mwema hakusahau kumtafutia farasi maji na chakula.
6
“Nyinyi ni watu wema na Mwenyezi Mungu atawazidishia baraka
zake. Nilikuwa nusura kupoteza maisha yangu kutokana na njaa
lakini mmenionesha wema, mgeni alishukuru.
“Ni sisi tunaofaa kukushukuru. Ni furaha yetu kukupokea na
kukutendea wema, Mzee Mwema alisema.
“Jina langu ni Saidi Ulenge kutoka nchi ya Nyikani. Nyikani ni mbali
sana na hapa. Ni safari ya siku zaidi ya kumi na tano kwa farasi.
Niliamua kusafiri kwa kuwa nilioneshwa na Mwenyezi Mungu
katika ndoto kuwa kuna mtoto katika familia hii atakayewafanya
matajiri. Mungu alinituma ili nije kumwona, mgeni alieleza.
Maneno ya mgeni yalimshtua sana Mzee Mwema.Aliikumbuka
vyema ndoto aliyoiota ambayo ilipuuziliwa mbali na mkewe. Ni
ndoto iliyomfanya kucheka hadi akaumwa na mbavu kwa wiki
nzima. Mkewe aliposikia ujumbe wa mgeni, naye alishtuka na
kupanua midomo kwa mastaajabu.
“Yaani una hakika yupo mwana wetu atakayetufanya matajiri?
Sijawahi kuamini, Bi.Amina alimwambia mgeni.
“Hiyo haikuwa ndoto ya kawaida. Niliiamini na ndipo nikafunga
safari, Saidi alisema.
Mzee Mwema alianza kuuona ukweli wa ndoto hiyo.Alimtazama
mkewe kwa macho ya kumwambia kuwa alijaribu kumwelezea
asikubali hata! Lilikuwa ni jambo la aibu kwa mkewe kuyasikia
maneno hayo kutoka kwa mgeni na bado hakuwa tayari
kuyakubali.
“Mzee Mwema, najua wanao wameenda kulala. Naomba
uwaamshe sasa hivi. Nataka kujua ni zawadi zipi wangeomba
nikawatafutie, Saidi alisema.
7
“Haiwezekani ukalala na kupumzika kisha asubuhi nikawaita
mbele yako wakasema zawadi wazitakazo?” Bi.Amina aliuliza.
“Haiwezekani hata kidogo. Naomba ombi langu litimizwe haraka
iwezekanavyo, Saidi aliwashauri.
Mzee Mwema aliwaamsha wanawe waliokuwa usingizini.Walimtii
mara moja.Walitoka walikolala kwenye matandiko sakafuni na
kusimama mbele ya mgeni. Walionekana wachovu sana huku
wakijikuna na kwenda miayo.
“Nawaomba mnitajie ni zawadi zipi mngetamani niwaletee.
Naondoka kesho alfajiri na mapema na baada ya mwezi mmoja
nitarejea hapa tena, Saidi aliwaahidi.
Watoto walikuwa na furaha isiyo kifani. Usingizi waliokuwa nao
uliisha na wakaonesha uchangamfu mwingi. Ule uzuri wa sura
zao ulikuwa dhahiri kwa Saidi.
“Naomba uniletee nguo za kifalme, wa kwanza alisema.
“Mimi natamani uniletee mkufu wa dhahabu, wa pili alisema.
“Ningetamani uniletee viatu vizuri ambavyo nikivivalia, kila mtu
kijijini ataajabia, wa tatu aliomba.
“Nami naomba niletewe bangili za dhahabu, wa nne naye alisema.
“Zawadi niiombayo ni mbawa za ajabu zitakazoniwezesha kuruka
kama ndege, wa tano naye alisema kwa furaha.
Watoto waliendelea kuomba zawadi zao mbalimbali. Saidi naye
aliendelea kuandika zawadi hizo kwenye kitabu kidogo alichobeba.
8
“Je, watoto wote wako hapa?” aliwauliza Mzee Mwema na Bi.
Amina.
Swali hilo liliwashangaza watoto na hata wazazi wao.
“Nauliza tena, je, hawa ndio watoto wako wote?” Saidi alimgeukia
Mzee Mwema.
“La hasha! Yupo mwingine mmoja, Mzee Mwema alisema kwa
wasiwasi.
“Yuko wapi? Mbona hujamleta hapa pamoja na ndugu zake?”
Saidi aliuliza.
“Mzee Mwema hakutaka kulijibu swali hilo. Alizidi kubabaika
na kutokwa na kijasho usoni pake.
“Nauliza kwa mara nyingine. Mwanao ambaye hayuko hapa yu
wapi?” Saidi alisisitiza.
Baada ya kimya kirefu, Mzee Mwema aliamua kusema ukweli.
Moyo ulikuwa ukimdundadunda kama ngoma.
“Basi mgeni wangu, sitaki kukuficha chochote. Daima mimi
hupenda kuusema ukweli. Ninaye mwanangu mwingine kwa
jina Kito. Hayuko hapa na ndugu zake. Ulipoingia hapa kwangu,
sikutaka umwone. Ni mvulana mlemavu. Nilienda kumficha nje
ya nyumba yangu. Naomba unisamehe, Mzee Mwema alisema.
“Si vyema kuwaficha watoto hata wakiwa na ulemavu wa
aina gani. Maumbile yote ni ya Mwenyezi Mungu.Wanao wote
wameomba zawadi zao zinazowapendeza isipokuwa Kito.
Natamani kumwona hapa mbele yangu, Saidi alisema.
9
Mzee Mwema hakuwa na pingamizi tena.Alitoka katika nyumba
na baada ya dakika chache akarejea akiwa na mwanawe Kito.
Alivyosema, Kito alikuwa mvulana mlemavu. Hakuwa na uwezo
wa kuona. Alikuwa ni kipofu na alitembea akipapasapapasa ili
kufika mahali alipotaka kwenda. Kito alipofika karibu na mgeni,
alifanya jambo ambalo ndugu zake hawakulifanya.
“Shikamoo, mgeni?” alimjulia hali.
“Marahaba, Kito. Naitwa Saidi. Hujambo?” alimwamkia.
“Sijambo, Saidi. Baba ameniarifu kuwa tumepata mgeni. Jihisi
nyumbani Saidi, Kito alimkaribisha.
“Nakuona mvulana mwema sana mwenye adabu ya kupigiwa
mfano. Nimeshapata maombi ya zawadi kutoka kwa ndugu zako.
Naondoka na huenda nikarejea hapa baada ya muda mrefu. Je,
ungependa nikakuletee nini?” Saidi alimuuliza Kito.
Kito aliposikia kuhusu zawadi, aliwaza na kuwazua. Hakumjibu Saidi
haraka. Baada ya muda ndipo alipomtazama Saidi akitabasamu.
“Naomba ukaniletee fimbo ya kunisaidia kutembea. Iwe ni fimbo
ya mti mmoja unaopatikana katika kisiwa cha Mawemeusi. Fimbo
hii imo katika nyumba ya maskini mmoja aliyefariki zamani.
Kila mmoja alishangazwa na zawadi ya Kito.
“Mwanangu, mbona waomba zawadi kama hiyo? Hapa petu
pana fimbo nzuri za kukusaidia kutembea. Mbona unamchosha
mgeni kwenda kisiwa cha Mawemeusi kukuletea fimbo tu?” Mzee
Mwema alimuuliza mwanawe, Kito.
10
“Naomba ukaniletee mbo ya kunisaidia kutembea...
11
“Kipendacho moyo ni dawa mwenyeji wangu. Mwanao ameomba
zawadi nami nafunga safari kwenda kuwatafutia wote zawadi
zao. Inshaallah Mungu akinijaalia nitarejea salama, Saidi alisema.
Saidi alisafiri usiku ule ule kuelekea sehemu za Kaskazini. Kwa
muda wa siku sita alikuwa safarini. Alikuwa amebeba chakula
cha kutosha.Alipitia miji mingi kuwanunulia wale watoto zawadi
zao naye akabahatika kuzipata kwa urahisi. Hata hivyo, zawadi
ya Kito ilikuwa vigumu kuipata. Alipoulizia kuhusu kisiwa cha
Mawemeusi aliambiwa kuwa kilipatikana mbali mno na chombo
kilichokaribia kisiwa hicho kilizama. Habari hizo zilimfanya Saidi
kuvunjika moyo.
“Usife moyo mwenzangu. Yupo mganga mmoja hapa mjini
anayeweza kukusaidia.Amka kesho alfajiri uende na bila shaka
utafanikiwa, mzee mmoja alimshauri.
Siku iliyofuata Saidi alifika kwa mpiga ramli ambaye
alimtengenezea dawa maalumu ya kumwezesha kufika kisiwa
cha Mawemeusi.Alikodi jahazi na kuanza safari akiwa amejiandaa
kabisa. Ilimchukua miezi miwili kufika kwenye kisiwa hicho
kisichokuwa na watu. Alipoiona ile nyumba iliyotajwa na Kito,
aliingia ndani na kuiona ile fimbo na bila kuharibu wakati
akaichukua. Alikuwa na furaha nyingi kuona kuwa zawadi
iliyomtaabisha kwa siku nyingi alikuwa ameipata.
Kito alikuwa na furaha nyingi kuzidi ndugu zake. Baba na mama
walishangazwa na furaha aliyokuwa nayo, hasa walipoitazama
fimbo aliyoshika. Haikuwa na chochote cha ajabu. Ilikuwa sawa
na fimbo yoyote ile. Hata hivyo, Kito aliikumbatia kana kwamba
fimbo hiyo ilikuwa ni dhahabu. Saidi aliiaga familia ya Mzee
Mwema na kuondoka.
12
“Kito, kesho amka nitakuongoza hadi kwenye chumba cha hazina
kilicho kule mlimani, fimbo ilimwambia Kito usiku mmoja.
Ilipofika asubuhi, Kito alitoka bila yeyote kujua. Fimbo ilimwelekeza
hadi mlimani kwenye pango moja la siri. Lilikuwa ni pango lisilo
na mahali wazi pa kuingilia.
“Nikamate sawasawa na uupige mwamba huu mara tatu. Mwamba
utapasuka na kutoa uwazi ambao utakuwezesha kuingia, fimbo
ilimshauri.
Kito alitii.Aliingia mle ndani na kushauriwa na fimbo achukue jiwe
moja la dhahabu.Aliporejea nyumbani, kila mmoja alishangaa.
“Mwanangu, umeiba wapi jiwe hili la dhahabu?” Mzee Mwema
aliuliza kwa hofu.
“Mwanao hajaiba kwa kuwa ni kijana mwenye nidhamu. Mimi
zawadi yake ndimi niliyemwongoza kulipata jiwe hilo. Lichukue,
ewe Mzee Mwema, ukaliuze kwa baniani. Atakupatia pesa
nyingi sana. Kila wiki Kito atakuwa akikupatia jiwe la kwenda
kuuza. Hakuna mtu atakayekushinda kwa utajiri. Utajiri wako
utamshangaza kila mmoja. Mtii mwanao Kito, fimbo ilishauri.
Mzee Mwema alifanya alivyoshauriwa. Baniani alishangazwa na
uzito wa jiwe lile.Alijua mara moja ilikuwa dhahabu safi.Alimlipa
Mzee Mwema pesa nyingi mno. Ilibidi Mzee Mwema amtafute
punda wa kubeba pesa zile alizozitia katika gunia. Kila wiki,
alikuwa akimuuzia baniani dhahabu.Wafanyabiashara wengine
wengi walifika kununua dhahabu. Familia ya Mzee Mwema ilipata
utajiri wa ghafla. Maisha yao yalibadilika wakawa na mali nyingi
mno. Walijenga nyumba maridadi iliyofanana na ya mfalme.
Kando ya nyumba hiyo, walitengeneza bustani iliyowavutia
wageni wa karibu na mbali.
13
“Mke wangu, umeamini ndoto yangu? Nilipokusimulia kwamba...
14
“Mke wangu, umeamini ndoto yangu? Nilipokusimulia kwamba
mmoja wa wanangu angetufanya matajiri, ulicheka nusura uvunjike
mbavu. Je, umeamini?”
“Kweli, mume wangu. Naomba radhi zako kwa kudharau kile
kilichopangwa na Mungu. Ama kweli, apangalo Mungu, huwa,
Bi.Amina alisema kwa furaha.
Familia ya Mzee Mwema iliishi maisha mema yenye amani na
furaha kwa msaada wa fimbo kupitia mkono wa Kito.
15
Kamusi Yangu
baniani neno lenye maana sawa na Mhindi
barazani sehemu inayojengwa ya kukaa na
kuzungumzia
bustani sehemu yenye miti na mitunda mizuri
hohehahe maskini asiye na chochote ila
kuombaomba
ilivuja iliwezesha maji kupita
kiamshakinywa chakula cha kwanza cha asubuhi
kubabaika kukosa umakini au utulivu
kupiga ramli kitendo cha mganga cha kumwagua
mteja wake
kupigiwa mfano tajwa kuwa mfano bora kwa wengine
kuvunjika moyo kukosa matumaini
mararu mavazi yaliyochakaa
paa sehemu ya juu ya nyumba
16
Maswali
1. Elezea kazi walizofanya wazazi wa Kito Mzee Mwema na Bi.
Amina
2. Eleza ndoto aliyoota Mzee Mwema.
3. Ni jambo gani lililotukia Mzee Mwema alipokuwa ameketi
barazani
4. Kwa nini Mzee Mwema alikuwa amemficha mwanawe Kito?
5. Eleza ni zawadi zipi walizoomba wanawe Mzee Mwema?
6. Zawadi maalum aliyoomba Kito ilikuwa gani na ingepatikana
wapi?
7. Ni matatizo gani aliyopata Saidi kabla ya kufika kisiwani
Mawemeusi?
8. Fimbo ilimwelekeza Kito wapi ili aupate utajiri?
9. Utajiri wa Mzee Mwema na familia yake ulitokana na uuzaji
wa nini?
10. Hadithi hii ina funzo gani kuhusu walemavu?
17
Bahati ya Kezo
18
Paliondokea kijana mmoja aliyeitwa Kezo. Baba yake Kezo, Mzee
Huzuni, alikuwa mtemakuni na mama yake, Bi. Mpole, alikuwa
mfinyanzi. Kila siku, Mzee Huzuni na Bi. Mpole waliamka alfajiri
na mapema kwenda kutafuta riziki. Kazi ya ukataji kuni ilikuwa
ngumu na ilimletea Mzee Huzuni pesa kidogo. Vilevile, kazi ya
kufinyanga vyungu haikuwa rahisi na mara nyingi Bi. Mpole
alirejea nyumbani mkono mtupu wakati alipokosa wateja wa
kununua vyungu vyake.
Kezo alilelewa katika familia maskini mno. Nyumba yao ilikuwa ni
kibanda kilichojengwa kwa fito na udongo. Paa lilikuwa la mabati
makuukuu. Nyakati za msimu wa mvua, paa la nyumba yao
lilivuja na kuwalazimu kuhamisha malazi kutoka upande mmoja
hadi mwingine.Vijana wengi wa kijiji cha Ngomeni alikoishi Kezo
na wazazi wake walimdharau kutokana na umaskini wao.
“Usivunjike moyo, mwanangu. Ipo siku itafika hao wanaokucheka,
watakuheshimu. Mungu hamtupi mja wake, Mzee Huzuni
alimwambia mwanawe Kezo.
“Ni kweli Kezo anayoyasema baba yako.Twaishi kwa majaaliwa
na hakuna ajuaye kesho itakuwa vipi. Nitazame kwa mfano. Hii
mikono yangu imekuwa migumu kutokana na kushika udongo
kila siku. Mikono ya baba yako nayo ni migumu sana kwa kuwa
yeye hutumia nguvu nyingi kukata miti apate kuni za kuuza. Sisi
wazazi wako tunafanya juhudi kwa uwezo tulio nao. Siku moja
Mungu atatujaalia, Bi. Mpole alimtia Kezo matumaini.
19
...Sisi wazazi wako tunafanya juhudi kwa uwezo tulio nao...
20
Haukupita muda mrefu, Mzee Huzuni aliugua. Ugonjwa wake
ulikuwa wa ajabu.Alianza kulalamika kuumwa mgongo.Aliacha
kwenda kukata kuni kabisa kwa kuwa kila alipoinama, mgongo
uliuma sana. Baadaye maumivu yalianza kichwani. Aliumwa
kichwa kila siku.Alianza kupoteza uwezo wa kuona na hatimaye
akawa kipofu. Uchungu ulifika miguuni akashindwa kutembea.
Bi. Mpole alihangaika sana kumtafutia mumewe matibabu.Alitumia
pesa nyingi kwa matibabu. Aliuza shamba lao dogo akiwa na
matumaini mumewe angepona lakini ugonjwa huo haukusikia
dawa zozote zile. Mzee huzuni alifariki na wanakijiji cha Ngomeni
wakamwomboleza kwa muda wa siku nyingi. Bi. Mpole na Kezo
walilia kwa siku nyingi lakini kilio chao kisingeweza kumrejesha
Mzee Huzuni.
Bi. Mpole alibaki na mwanawe, Kezo. Maisha yaliendelea kuwa
magumu.Walirarukiwa wakatembea wakivalia nguo zenye viraka.
Nyumba yao mbovu ilianguka mara kadhaa ikabidi wasamaria
wema kuwasaidia. Mara kwa mara walikosa chakula na kulala
njaa. Kila mmoja katika kijiji cha Ngomeni aliwajua kutokana
na shida nyingi zilizowakabili. Baadhi ya watu wasio na huruma
waliwaita Kezo na mama yake machokoraa.
“Mwanangu, tumelia hadi tukamaliza machozi machoni. Hakuna
haja ya kulia tena. Usife moyo kwa kuchekwa na vijana wa rika
lako. Nina imani siku moja, siku moja utakuwa na utajiri kuliko
yeyote hapa kijijini, mama alimwambia.
“Kweli mama. Siku hizi silii kama zamani. Nimeshazoea kuchekwa
na kudharauliwa. Najua siku moja watatafuta wa kumcheka
wakose, Kezo alimhakikishia mama yake.
“Mwanangu, natamani uishi ukitanguliza nidhamu katika maisha
21
yako. Kila mara kumbuka kuwaheshimu wakubwa kwa wadogo
na vilevile kuusema ukweli hata kama ukweli huo utakuletea
hasara au ukutie hatarini, mama alimkumbusha.
“Nitafuata ushauri wako na wa marehemu baba kila wakati,
Kezo aliitikia.
Siku moja mfalme wa nchi hiyo aliyeitwa Daudi Mwema alitamani
kumpata kijana mwenye tabia nzuri.Aliwatuma watumishi wake
katika vijijini vingi nchini kuwachagua vijana ambao wangeshindana.
Watumishi walipofika katika kijiji cha Ngomeni, waliwachagua
vijana wanne na Kezo alikuwa mmoja wao.
“Hawa watumishi hawaelewi walifanyalo. Mbona wanamchagua
Kezo? Kezo ni kijana wa maskini na hafai hata kukanyaga kwenye
kasri, mama mmoja alisema.
“Nilikuwa na matumaini kijana wangu angechukuliwa lakini
watumishi wapumbavu hawa wameenda kumchagua mtoto wa
maskini. Huyo hata akishiriki shindano hilo, atavuta mkia,”
mama wa kwanza alisema.
“Baba yake alifariki akiwa maskini na yeye na mama yake
wataendelea kuwa maskini, mama wa pili alijibu akitikisa kichwa.
Huko kwenye kasri, yaani jumba kubwa la Mfalme Daudi Mwema,
vijana wengi walifika.Walikuwa wametoka vijiji hamsini na vitatu.
Mfalme alipendezwa na jinsi vijana hao walivyosubiri walichoitiwa
kwa hamu na ghamu.Alianza kuwahutubia.
“Basi vijana wangu, nimewaita hapa ili nipime uwezo wenu wa
ukulima. Kumbukeni kuwa nchi yetu inategemea kilimo katika
kuimarisha uchumi wake. Basi nikajisemea nitawapa mtihani
wa kujaribu iwapo mnaweza kuwa wakulima wazuri katika siku
22
zijazo, mfalme alinyamaza kidogo. Kila mvulana alikuwa ametulia
tuli kama maji ya mtungi.
“Mbele yenu nina mamia ya mbegu za mimea mbalimbali.
Mbegu hizi nimepewa na mfalme wa nchi jirani. Huko wamepanda
mbegu hizi na kufikia sasa, wamevuna mazao mengi. Nitawapa
mbegu hizi nanyi mkapande.Wale watakaopanda na ziote kuwa
miche mizuri, hakika nitawatuza kwa zawadi za thamani kubwa,
mfalme aliwaeleza.
Mfalme alisaidiwa na watumishi kuwagawia vijana hao mbegu
kwa idadi sawa pamoja na mikebe maalumu yenye mchanga
wenye rutuba. Kila kijana alipata mbegu saba.
“Nendeni mkapande mbegu hizo. Miezi mitatu itakapoisha, ndipo
mtakapokuja hapa tena tujue mshindi ni nani, Mfalme Daudi
Mwema aliwaaga kwaheri.
Kezo alifika nyumbani jioni hiyo akiwa na furaha. Mama yake
alimpokea vyema kisha akamwomba amweleze yaliyotokea.
Kezo alieleza kila kitu bila kuficha.Alimweleza mama yake jinsi
vijana wa kijiji chao walivyomwacha na kumwamuru asitembee
nao kutoka makao ya mfalme hadi hapo kijijini.
“Mjua kesho si mwanadamu, mwanangu. Nitakusaidia kuzitunza
mbegu alivyoshauri mfalme nawe bila shaka utaona ukiishinda
zawadi, mama alimtia moyo.
Siku iliyofuata, Kezo na mama yake walipanda mbegu katika
ule mkebe waliopewa akina Kezo na mfalme. Kezo alikumbuka
kunyunyizia mbegu maji kila siku. Alikuwa na subira. Baada ya
mwezi mmoja, hakuna mbegu katika mkebe wa Kezo iliyoota.
23
Kezo na mama yake walipanda mbegu kaka ule mkebe...
24
“Wewe ni kijana mwenye kisirani. Hakika hukufaa kuchaguliwa
kwenda kwa mfalme. Hizo mbegu zako hazitawahi kuota, mama
wa kijana mmoja alimwambia Kezo.
Siku hiyo, Kezo alilia sana.Alilia alipoona kuwa hakuna mwanakijiji
yeyote aliyemtakia mazuri isipokuwa mama yake. Alianza
kuvunjika moyo wale vijana wengine wa kijiji hicho walipoelezea
kwa furaha jinsi mbegu zao zilivyoota kufikia mwisho wa mwezi.
“Si vyema kukata tamaa, mwanangu.Tuwe na subira, Bi. Mpole
alimtuliza mwanawe Kezo aliyekuwa amelia kwa muda mrefu.
“Nita…nitamjibu vipi mfalme i..iwapo mbegu zangu hazi..
hazitaota?” Kezo alilia na kupenga kamasi.
Kwa muda wa miezi mitatu, mkebe wa Kezo ulibaki bila mche
wowote! Alikuwa akinyunyizia maji asubuhi na jioni lakini bidii
zake ziliambulia patupu. Ajabu ni kuwa vijana wote waliopewa
mbegu walikuwa na furaha mpwitompwito. Mbegu zao ziliota
mwishoni mwa mwezi wa kwanza. Waliisubiri siku ya kwenda
kwa mfalme kwa hamu na ghamu.
Siku hiyo, Kezo aliamshwa na mama yake alfajiri na mapema.
“Kezo! Kezo mwanangu, amka! Leo ni siku ya kwenda kwa
mfalme, mama alimkumbusha.
“Mama, nampenda mfalme kwa moyo wangu wote. Naogopa
kwenda kumkabili. Naogopa kumkasirisha. Naogopa kukuletea
aibu mama, Kezo alisema machozi yakimtiririka usoni.
“Usiogope mwanangu.Waswahili husema, ukweli ukidhihiri, uongo
hujitenga. Hakuna kosa lolote ulilotenda. Nimekuwa nawe kipindi
chote tangu mlipopewa mbegu na mikebe. Nimeshuhudia juhudi
25
zako za kuzitunza mbegu. Si makosa yako kuwa hazikuota,
mama alimwelezea.
“Lakini mama, huoni ajabu upande wangu? Iweje mbegu za wengi
nasikia zimeota. Hata hapa kijijini wale vijana nilioenda nao kwa
mfalme, nimewatembelea na kujionea kwa macho yangu miche
tofauti tofauti katika mikebe yao. Iweje mkebe wangu..wangu tu,
hauna mche hata mmoja?” Kezo aliuliza kwa huzuni.
“Kumbuka maneno ya baba yako alipokuwa hai.Alikukumbusha
kusema ukweli hata kama ukweli huo ungekutia mashakani.
Mwanangu, kama mama yako nami nitaushikilia ukweli. Nenda
kwa mfalme na uuseme ukweli nami ninakuhakikishia kuwa
hutakuwa na mzigo wowote moyoni mwako.
Vijana waliwasili katika makao ya Mfalme Daudi Mwema. Kati
ya vijana wote, ni mkebe wa Kezo ambao ulikuwa na mchanga
tu. Mikebe ya vijana wote ilikuwa na miche iliyostawi vyema.
“Jamani! Mwone huyu kijana mvivu asiyejua kumfurahisha
mfalme!” alishangaa kijana mmoja.
“Tulipewa mbegu miezi mitatu iliyopita na bado mkebe wake
ni mtupu. Ningalikuwa yeye, nisingalijichosha nikija kujiaibisha
mbele ya Mfalme Daudi Mwema, kijana huyo alisema ili kila
mtu amsikie.
Vijana wote walipotazama mkebe wa Kezo, walishangaa kwa
kuona kuwa hakuna mche wowote ulioota. Baada ya muda usio
mrefu, mfalme alitokeza na kuanza kuzungumza na vijana.
“Vijana wangu, nafurahia bidii na kujitolea kwenu. Nina furaha
ninapotupa macho kwenye mikebe yenu na kuona miche mizuri.
Nyinyi ni vijana wema na leo mtapokea zawadi nyingi mno.
26
Waswahili husema, ukiona vyaelea jua vimeundwa. Je, kuna
yeyote ambaye mkebe wake ni mtupu?” mfalme aliuliza.
Kabla Kezo ajibu, watumishi walikuwa wamemkamata na
kumfikisha mbele ya mfalme. Kezo alikuwa akitetemeka sana.
“Kijana, waitwa nani?” mfalme alimuuliza.
“Naitwa Kezo…Kezo Huzuni, alijibu kwa wasiwasi.
“Kwa nini hukutunza mbegu zangu?” mfalme aliuliza kwa sauti kali.
“Mfalme, na Mungu akujaalie uishi maisha marefu. Nilipanda
mbegu zangu na nikazitilia maji kila siku lakini hazikuota. Niliamua
nifike hapa ili kukueleza ukweli ulio moyoni mwangu, Kezo
alistaajabu akizungumza bila hofu.Woga wote ulimtoka.
Mfalme Daudi Mwema alishangazwa na Kezo.Aliamini kuwa katika
ufalme wake, bado walikuwapo vijana waaminifu. Alisimama
na kuwageukia vijana wote waliosubiri zawadi.
“Nyinyi nyote ni waongo! Waongo wakubwa mno. Nilitayarisha
mbegu za mpapai kisha nikawaamuru watumishi wangu mbegu
zote zichemshwe ili atakayezipanda zisiote. Sasa ni maajabu gani
ninayoyaona mbele yangu? Mikebe mingi hapa mbele yangu ina
mimea tofauti na mbegu nilizowapa! Mlipoona mbegu hazioti,
mlitafuta mbegu nyingine mbadala mkazipanda ili kunidanganya.
Huyu kijana hapa, Kezo Huzuni, ndiye msema kweli.Amenionesha
uaminifu wake. Hajaaibika kufika hapa mkebe wake ukiwa mtupu.
Kwa hivyo, Kezo Huzuni ndiye mshindi!” Mfalme Daudi Mwema
alitangaza.
27
...Huyu kijana hapa, Kezo Huzuni, ndiye msema kweli...
28
Kezo hakuamini aliyoyasikia.Watumishi wa mfalme walimbeba
juu juu kwa furaha kulizunguka kasri la mfalme. Kufikia mwisho
wa siku hiyo, vijana waliondoka kuelekea nyumbani kwa nyoyo
nzito. Kezo alituzwa zawadi kemkemu na mfalme.Alibebwa kwa
farasi mweupe wa mfalme hadi nyumbani kwao. Kila mwanakijiji
cha Ngomeni alitoka katika nyumba kushuhudia tukio hilo.Wote
waliomcheka na kumdharau, walijipata wakistaajabu.
“Mama, nimeshinda! Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, nimeshinda.
Mfalme ameagiza uchukuliwe akakuone, Kezo alimwambia mama
yake akimkumbatia kwa furaha.
Mfalme alikubali mama wa Kezo na Kezo kuishi katika kasri na
kupata chochote walichotamani. Mfalme alikuwa na wake wengi
lakini hakujaaliwa mwana wa kiume.Alikuwa tayari kumrithisha
Kezo ufalme pindi akiwa mtu mzima. Kezo na mama yake waliishi
katika makazi hayo ya kifalme kwa raha mustarehe.
29
Kamusi Yangu
aibu hali inayompata mtu akitenda
kitendo kibaya mbele ya watu
alimtia moyo alimpa matumaini
atavuta mkia atakuwa wa mwisho
hamu na ghamu hali ya kulisubiri jambo sana
kasri jumba analoishi mfalme
kukata tamaa kutokuwa na matumaini
machokoraa vijana wa mitaani
makuukuu yasiyo mapya, ya zamani
yasiyopendeza
mbegu kokwa zinazopandwa ardhini ili
kupata mimea
mfinyanzi anayetengeneza vyungu kwa udongo
miche miti midogo midogo
mtemakuni mtu ambaye kazi yake ni kukata kuni
na kuziuza
rutuba vitu vilivyo ardhini ambavyo hufanya
mimea kustawi vizuri
waaminifu wasio wadanganyifu
wasamaria wema wenye nyoyo za kuwasaidia wengine
wateja watu wanaomnunulia muuzaji bidhaa
zake
30
Maswali
1. Elezea kazi walizofanya wazazi wa Kezo Mzee Huzuni na Bi.
Mpole.
2. Elezea shida alizopitia Mzee Huzuni kutokana na ugonjwa
aliougua.
3. Andika mambo mabaya aliyotendewa Kezo na mama yake
na wanakijiji kutokana na hali yao ya umaskini.
4. Mfalme aliwapa Kezo na vijana wengine shughuli gani?
5. Ni jambo lipi linaloonyesha kwamba Kezo alikuwa kijana
mwenye subira?
6. Kezo alipoona mikebe ya vijana wenzake ikiwa na miche,
alifanya nini?
7. Mfalme alipomwuliza Kezo kwa nini hakutunza mbegu zake,
Kezo alimjibu vipi?
8. Elezea jinsi kusema ukweli kulivyomsaidia Kezo Huzuni
maishani.
9. Elezea mambo yote mazuri Mfalme Daudi Mwema aliyomfanyia
Kezo baada ya kumtangaza mshindi.
10. Mfalme Daudi Mwema alimwahidi Kezo kwamba pindi
akiondoka uongozini, Kezo ___________ ufalme. (angeuridhi,
angeurithi, angediriki)
31
Mama Kawira na Jitu
32
Hapo zamani za kale kando ya msitu mmoja aliishi mtu na mkewe.
Mtu huyo aliitwa Mzee Kiloba na mkewe Mama Kawira. Mzee
Kiloba alipata riziki yake kupitia kazi ya kutengeneza vitu vya
chuma. Kwa hivyo alikuwa mhunzi stadi sana.Watu wa vijiji vya
mbali na karibu walimtegemea Mzee Kiloba kuwatengenezea
vifaa vya chuma. Mzee Kiloba naye aliifanya kazi hiyo kwa moyo
wote na kila mmoja akampenda.
Siku moja Mzee Kanyi, rafiki wa Mzee Kiloba alimtembelea.
Alikuwa akifanya kazi mahali palipoitwa Utange, maeneo ya
mbali sana kutoka alipoishi Mzee Kiloba na familia yake. Mzee
Kanyi alimwelezea Mzee Kiloba kuwa watu wa huko Utange
hawakujua umuhimu wa vifaa vya chuma. Kwa hivyo, iwapo Mzee
Kiloba angehamia Utange, bila shaka angekuwa tajiri. Habari
hizo zilikuwa nzuri masikioni mwa Mzee Kiloba.
“Mke wangu, tumeishi maisha ya umaskini mkubwa. Nikubalie
niondoke na nikipata hali ni nzuri kule Utange, nirudi nikuchukue.
Nisingetamani tuendelee kuishi maisha kama haya, Mzee Kiloba
alimwelezea mkewe.
“Sina tatizo, mume wangu. Nakutakia kila la heri. Usisahau
kunitumia pesa za matumizi ya hapa nyumbani, Kawira
alimkumbusha mumewe.
Mzee Kiloba aliandamana na Mzee Kanyi safarini. Alikuwa na
matumaini makubwa ya kupata utajiri.Alikuwa akiwatengenezea
wanavijiji vifaa vya chuma lakini walimlipa pesa kidogo mno.
Ni kazi aliyoifanya usiku na mchana lakini ikampatia pesa
zisizomwezesha kuishi maisha mazuri.
33
Alikuwa akiwatengenezea wanavijiji vifaa vya chuma...
34
Mzee Kiloba alipofika Utange, aliamini maneno ya Mzee Kanyi.
Kweli watu wa Utange walikuwa nyuma kimaendeleo.Walichonga
vijiti na kuvitumia kulima mashambani. Hata mashujaa wa Utange
walienda vitani na marungu bila mikuki wala mishale.Walitumia
mawe kukatia nyama walipowinda wanyama wa mwituni au
kuchinja wale wa nyumbani. Mzee Kiloba alitengeneza vifaa vizuri
na kuanza kuvipigia debe vinunuliwe.
Waswahili husema kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza.Vifaa
vya Mzee Kiloba vilijulikana na wanavijiji wa karibu na mbali
wakafika kuvinunua. Aliuza kuanzia alfajiri hadi jioni. Aliutumia
usiku kuendelea kutengeneza vingine na hata akawa hana muda
wa kupumzika. Hata hivyo, hakusahau kumtumia mkewe pesa
za matumizi. Pesa nyingine alizopata alizitumia kuweka akiba
kwani akiba haiozi.
Kule nyumbani kwa Mzee Kiloba, Mama Kawira aliendelea
vyema.Alikuwa mjamzito na siku zake za kujifungua zilikaribia.
Siku moja wakati wa alasiri, mkunga alifika kumsaidia naye
akajaaliwa kupata mwana wa kiume aliyefanana na baba yake.
Mama Kawira alikuwa na furaha isiyo kifani kumpata mwana
huyo. Hakujua namna ya kuwasiliana na mumewe amweleze
habari hizo kwa kuwa nyakati hizo hakukuwa na simu. Watu
waliowajua walikuwa wamewadharau kwa miaka mingi kwa
sababu hawakuwa na mwana. Mama Kawira alimwita mtoto
huyo Bahati.
Usiku huo huo, mgeni wa ajabu alifika nyumbani kwa Mama
Kawira. Mama Kawira alikuwa akipika chajio wakati aliposikia
sauti kama ya upepo mwingi ulioitikisa nyumba. Sauti hiyo
ilifuatiwa na nyingine ya nyayo. Hazikuwa nyayo za kawaida
kwa kuwa kila sauti ilipotokea, nyumba ilikuwa nusura kubomoka.
Mama Kawira alishikwa na uoga sana na akaanza kumlilia mume
35
wake. Bahati naye aliogopa sana akalia ng’aa ng’aa ng’aaa.
“Usimlilie mume wako Mzee Kiloba!” Mama Kawira alisikia sauti
mbovu nje ya nyumba.
Alipoufungua mlango, alikuwa nusura kuanguka chini na kuzimia.
Hapo nje ya nyumba palikuwa na jitu. Lilitisha sana. Lilikuwa refu
kama mlingoti na jeusi kama makaa. Kwenye paji usoni lilikuwa na
macho matatu na jicho la katikati liling’aa kama tochi iliyowaka
gizani. Katikati ya kichwa palikuwa na pembe mbili ndefu kama
za mbuzi wa kiume. Jitu halikuwa na shati. Kifua chalo kilikuwa
kikubwa mno na kilijaa malaika kama msitu. Lilikuwa na miguu
mirefu kama ya twiga.
“Ha! Ha! Haaaa!” Jitu liliangua kicheko kwa dharau.
“Mimi…Miimi Masangisa nina bahati sana. Natamani sana nyama
ya mtoto mchanga. Hiyo ndiyo nyama ambayo niliahidiwa na
mganga itaniongezea nguvu maradufu. Kwa hivyo, nimekuja
huku kwako ili unipe Bahati nimle. Najua baba yake yu mbali
sana kwa hivyo sina wasiwasi hata!” Jitu lilieleza kwa furaha.
“Tafadhali, nakuomba usinidhuru wala mtoto wangu. Sina mtoto
mwingine, ni huyu Bahati, Mama Kawira alielezea akidondokwa
na machozi.
“Usijali Mama Kawira. Utawazaa wengine wengi. Nimtakaye kwa
sasa ni huyu Bahati. Kwa kuwa ndiye amezaliwa leo, nitasubiri
afikishe siku kumi. Hakikisha umemnyonyesha sawasawa ili
anenepe. Nitakuwa nikipitia hapa kuona jinsi anavyoendelea,
Jitu lilisema na kuondoka.
Mama Kawira alishindwa kulala usiku huo. Hakupata hata lepe
la usingizi. Siku iliyofuata alianza kufikiria namna ya kumwokoa
36
mwanawe kutokana na jitu.Aliwaza kupakia nguo na kutoroka
lakini hakujua alikofanyia kazi mumewe.Afanye nini? Alipokuwa
ameshika tama, ng’ombe wake wa kike alimwona.
“Mama Kawira, mbona leo huna furaha? Jambo gani limetokea?”
Ng’ombe alimuuliza.
“Ninamhitaji mume wangu kwa dharura. Hakuna yeyote
anayeweza kunisaidia. Sijui nitafanya nini, Mama Kawira alisema
baada ya kumwelezea ng’ombe yale yaliyotokea.
“Sisi wanyama hatutaweza kukusaidia. Hata hivyo, ndege
watakufaa. Sijui ni ndege yupi bora lakini ukiwachunguza, utaona
ni yupi atakayekufaa, Ng’ombe alimshauri.
Mama Kawira alifuata ushauri wa ng’ombe.Alianza kuwachunguza
ndege ili kujua ni ndege yupi angemtuma alikofanyia kazi mumewe.
Alijua ndege walikuwa na uwezo wa kipekee wa kuruka kwa
kasi na kwenda mbali.
“Mama Kawira, jina langu ni Kasuku. Nimeambiwa unanihitaji
nami nimefika, Kasuku alijitambulisha.
“Ndio. Hakika nahitaji ndege wa kuruka mbali aliko Baba Bahati
ampelekee ujumbe maalum.
“Nitume Mama Kawira. Nakuhakikishia kuwa nitaufikisha ujumbe
huo, Kasuku alijisifu.
“Je, nikikutuma na uanze kuigaiga sauti na vitu vingine njiani,
huoni unaweza kusahau kuufikisha ujumbe wangu?”
Kasuku aliposikiliza swali la Mama Kawira alijua ni kweli alipenda
kuiga chochote alichosikia. Kwa hivyo, kulikuwa na uwezekano
mkubwa asiufikishe ujumbe.
37
“Pole Mama Kawira. Kwa kweli ukinituma, huenda nikayaona
mambo mageni nikaanza kuyaiga. Napenda sana kuiga hasa
sauti za binadamu na viumbe wengine.
Hatimaye Kasuku aliondoka kwa aibu nyingi sana.
“Mama Kawira, nimesikia kwamba Kasuku alishindwa na kazi
ya kuupeleka ujumbe. Nimefika. Jina langu ni Bundi, Bundi
anayeogopwa na kuogofya. Nimefika kukusaidia.
“Mbona unapenda kujisifia hivyo Bundi? Majisifu ya nini? Nikujuavyo,
unapenda kuyaacha majukumu yako na kwenda kuwatangazia
habari za kifo wanadamu. Je, ujumbe wangu utaufikisha vyema?”
Bundi alishtuka kwamba Mama Kawira alijua siri yake.
“Ni kweli Mama Kawira. Nina tatizo kubwa. Tatizo langu ni
kuwatembelea wanadamu usiku nikiwakumbusha kuwa kifo ki
karibu. Nasikitika siweza kuupeleka ujumbe wako, Bundi alikiri
udhaifu ake.
Chiriku aliposikia kwamba Bundi alishindwa, alimcheka sana. Siku
iliyofuata alikuwa nyumbani kwa Mama Kawira.
“Jina langu ni Chiriku na halipo lolote gumu kwangu. Ukiwauliza
wenzangu watakuambia ukweli. Nipo hapa kukusaidia.
“Sioni iwapo utaweza. Nikujuavyo, una kelele nyingi sana. Huenda
ukausahau ujumbe wangu na badala yake upige kelele jinsi
ulivyozoea tangu kuzaliwa, Mama Kawira alimweleza.
Kutokana na kuwa na maneno mengi, Chiriku aliuanguka mtihani
akaondoka akiwa na huzuni nyingi.
Siku hiyo hiyo jioni,Tausi alifika nyumbani kwa Mama Kawira.
38
Alikuwa niTausi wa kiume.Tausi huyo alisimama mbele ya Mama
Kawira na kuonesha urembo wake wa shani.
“Tausi, wewe ndiwe ndege mrembo niliyepata kukutana nawe.
Hata hivyo, nina wasiwasi mwingi nawe. Je, utaufikisha ujumbe
wangu mbali anakofanyia kazi mume wangu?”
“Nitafikisha, Mama Kawira, Tausi alijibu kwa sauti thabiti.
“Nina hofu kubwaTausi. Ujumbe nikupao hautaki ndege anayeruka
akijitazama kwa kioo jinsi alivyo mrembo. Je, utaweza?”
“Hiyo ni kazi ngumu, Mama Kawira. Sitaweza. Mimi huutanguliza
urembo wangu kuliko jambo lolote duniani. Kwaheri Mama
Kawira, Tausi alisema na kuruka.
Mama Kawira alianza kuwa na hofu. Ilikuwa siku ya sita na
zilisalia siku nne, nne tu jitu lifike kumla Bahati.
“Tai, najua wewe ni ndege mwenye nguvu na uwezo wa kuruka
mbali sana. Nina ujumbe kwa mume wangu. Je, utaweza kuufikisha
salama?”
“Mbona nisiufikishe, Mama Kawira? Nipe ujumbe huo nami
nitaanza safari mara moja.
“Sioni ukiufikisha. Je, ukiiona mizoga ya wanyama waliokufa au
kuliwa na simba hutaigusa?”
“Siwezi kuiacha. Mizoga ni mitamu sana, Tai alijibu.
39
“Siwezi kuiacha. Mizoga ni mitamu sana,...
40
“Basi ni wazi nikikupa ujumbe, utaiona mizoga na kuusahau.
Umefeli mtihani wangu, Mama Kawira alisema kwa huzuni.
Haukupita muda mrefu, Kipanga alitokea.
“Mama Kawira, nasikia ndege wenzangu wakiniambia una ujumbe
wa ajabu ungetamani kumtuma ndege mwenye uwezo. Basi mie
hapa Kipanga niko tayari unitume.
Mama Kawira alimtazama Kipanga kwa muda kisha akatikisa
kichwa.
“Je, ukiibeba barua kwa kidona na uone vifaranga wa binadamu
utafanya nini?”
“Nitashuka niwale vifaranga mara moja. Nyama ya vifaranga
ni tamu sana. Siwezi kuiacha, Kipanga alisema.
“Ukiendelea kumla kifaranga, barua utakuwa umeiweka wapi?”
Kipanga alishindwa kujibu swali hilo.Aliinamisha uso na kutoweka
kwa aibu nyingi sana.
Mama Kawira alizidi kusikitika kila saa ilipopita. Alikuwa
ameanza kukata tamaa. Akiwa hapo nje ya nyumba yake,
alimwona Hondohondo akitokea. Baada ya mazungumzo marefu,
Hondohondo alishindwa kuipeleka barua kwa kuwa alikiri alipenda
kupiga kelele za ajabu msituni. Pia, kidona chake kilikuwa kikubwa
na barua ingeanguka akiwa hewani.
Alifuatia Kunguru aliyeshindwa kutokana na tabia yake ya kuruka
mahali popote penye nyama. Heroe naye alishindwa kwa kuwa
badala ya kuruka moja kwa moja, alipenda kuogelea sehemu
zenye maziwa. Hatimaye alifika Mbayuwayu. Zilisalia siku mbili
tu, siku ya kumi itimie.
41
“Mama Kawira, naitwa Mbayuwayu na ni miguuni pako
nikuhudumie. Mbayuwayu alisema taratibu.
Wamefika hapa ndege wengi na wote wameshindwa. Nikujuavyo,
huwezi kushindwa. Mwendo wako wa kasi hewani ukiwa na
ndugu yako Kipungu ni wa kustaajabiwa. Njoo nikutume maana
hakuna wakati.
“Shika barua hii iliyo katika bahasha. Mpelekee mume wangu aliye
nchi ya Utange.Akishaisoma barua, atajua namna ya kufanya,
Mama Kawira alieleza.
Mbayuwayu hakuhitaji kwenda nyumbani kujitayarisha.Alianza
safari mara moja, barua ikiwa kwenye kidona chake.Aliruka usiku
kucha na siku iliyofuata saa tano akawasili Utange. Alitua juu
ya mti mahali Mzee Kiloba alipofanyia kazi.Aliimba wimbo huu:
Mbayuwayu nimefika, nimeuleta ujumbe,
Niruhusu nishuke, mimi ni mjumbe wako,
Nimefika kwa haraka, nipokee usiogope.
Ukinitizama kidona, nimeibeba barua,
Na wala sijaichana, sijaichana kwa kuwa,
Watakwa haraka sana, mkeo kajifungua.
Kajifungua kitoto, kitoto kilichoumbika,
Ukiyatazama macho, ni kama ya malaika,
Kiloba kubali wito, jamaa inakutaka.
42
Nyumbani kuna mgeni, sio mgeni wa heri,
Ni mchukivu shetani, mwenye ujanja ayari,
Usipofika nyumbani, ashaupanga ushari.
Mzee Kiloba alimkaribisha Mbayuwayu. Aliichukua ile bahasha
na kuitoa barua. Alipoisoma, sura yake ilibadilika mara moja.
Alimwachia Mzee Kanyi vifaa vyake kisha akamkodi farasi
mwenye nguvu. Alimwendesha mbio mbio usiku kucha na siku
iliyofuata, akawasili salama salmini nyumbani.Alikaribishwa na
mkewe na baada ya kula na kupumzika, akajiandaa kwa vita.
Akiwa mfua vyuma, alikuwa na upanga mkubwa wenye makali
ya ajabu. Usiku ulipofika, alijificha katika nyumba.
Jitu Masangisa lilitimiza ahadi. Lilifika usiku na kutaka kumla
Bahati. Bahati aliposikia sauti ya jitu, alilia sana.
“Kabla hujamla mwanangu, naomba nikutilie asali ya kulainisha
tumbo lako, Mama Kawira alisema akilipokeza jitu asali.
Jitu lilikunywa kisha likasema liongezwe hadi likanywa kibuyu
kizima. Kumbe haikuwa asali ilikuwa ni pombe tamu. Lilianguka
na kulala usingizi fofofo! Mzee Kiloba alipoona hayo, alitoka
mafichoni.Alilichoma jitu kwa upanga tumboni na kabla liamke,
akalichoma tena na tena. Tumbo lilipasuka na maini ya jitu
yakatawanyika pote. Lilikufa kifo chenye uchungu mwingi.
43
Alilichoma jitu kwa upanga tumboni na kabla liamke,..
44
Mzee Kiloba aliacha kazi Utange akaishi na familia yake.Alikuwa
amepata utajiri mwingi usio kifani.Yeye, mkewe na Bahati waliishi
maisha ya raha mustarehe.
45
Kamusi Yangu
akiba pesa anazoweka mtu zimsaidie
baadaye
chajio chakula cha jioni
kuvipigia debe kuvisifia vitu vinunuliwe
malaika nywele zinazoota kifuani, mikononi na
miguuni
maradufu mara mbili kwa idadi
mhunzi mtu anayefua vyuma na kutengeneza
bidhaa mbalimbali kwa kutumia
vyuma hivyo
mkunga mtu anayesaidia kina mama kujifungua
46
Maswali
1. Ni jambo gani lililomfanya Mzee Kiloba kuhama nyumbani
kuenda Utange?
2. Ni jambo gani lililomfanya Mzee Kiloba kutopata pesa nyingi
alipokuwa akifanyia kazi nyumbani kwake?
3. Eleza ni mambo gani mawili yanayoonesha kwamba Mzee
Kiloba aliipenda familia yake hata akiwa mbali.
4. Ni mgeni wa aina gani aliyemtembelea Mama Kawira?
5. Ni mnyama yupi aliyemshauri Mama Kawira kwanza?
6. Kwa nini Kasuku asingeweza kutumwa afike alikokuwa Mzee
Kiloba?
7. Kwa nini bundi asingeweza kutumwa afike alikokuwa Mzee
Kiloba?
8. Miongoni mwa ndege waliotajwa, ni yupi hupenda kula mizoga?
9. Kwa nini Kipanga aliinamisha uso wake chini mbele ya Mama
Kawira kisha akaondoka?
10. Mama Kawira alilifanyia jitu nini hadi likaishiwa na nguvu?
47
Mungu Hamsahau Mja
Wake
48
“Taabu! Taabu! Umekuwa kiziwi siku hizi? Njoo hapa mara moja,
ilikuwa ni sauti kali ya Bi. Upanga mama yake Taabu.
“Naona siku hizi umemea pembe na leo ni siku yangu ya mwisho
kuzivumilia hizo pembe. Lazima nizikate kabisa, Bi. Upanga
alisema kwa hasira.
Taabu kijana mwenye umri wa miaka kumi na miwili alitokeza
nyuma ya mwembe uliokuwa mbali kidogo na nyumba.Alikuwa
akichanja kuni za kupikia. Jasho jingi lilikuwa likimtiririka tiriri
na uchovu kumlemea. Alianza kuzichanja kuni hizo saa nzima
iliyopita.Taabu alisimama mbele ya mama yake huku akitetemeka
kama kifaranga aliyenyeshewa.
“Mtoto usiyefaa hata chembe! Nimezikosa shilingi zangu mia
tano zilizokuwa juu ya meza katika chumba changu cha kulala. Zi
wapi pesa hizo?” Bi. Upanga alimuuliza, hasira za mkizi zikimwaka
kama moto.
Taabu alisimama mbele ya mama yake huku akichanganyikiwa.
Ni swali ambalo hakujua alijibu vipi. Mara nyingi alizosingiziwa
na mama yake huyo, hata alipomweleza ukweli, mama alimpuuza.
Ni mara nyingi alipokea kipigo cha bure na baadaye mama
akagundua kwamba Taabu hakuwa na makosa.
“Unanificha kule ambako umeziweka pesa? Leo ni leo msema
kesho ni mwongo. Leo nakwambia utakiona cha mtemakuni.
Leo nitakuchuna ngozi kama mbuzi achunwavyo akichinjwa, Bi.
Upanga aliapa.
“Haya, nakuuliza kwa mara ya mwisho, umezificha wapi pesa
zangu?”
49
Taabu alimtazama mama yake na kuona hatari ikimtawala uso
mzima. Hatimaye aliamua kuzungumza.
“Mama, jana nilipotoka shuleni, nilivua sare yangu chafu na
nikaifua. Nilikatakata kabichi na kuanza kuandaa chakula cha
jioni na kweli ulipotoka kwa mama Kasoja kusukwa, ulipata
chajio kikiwa tayari. Kaka yangu Tito ndiye nilimwona akiingia
na kutoka katika chumba hicho, Taabu alieleza.Tito alikuwa ni
kijana wa rika sawa na Taabu.
Bi. Upanga alimtazama Taabu kana kwamba alikuwa amefanya
kosa kubwa sana kulitaja jina la mwanawe Tito.
“Yaani unamsingizia mwanangu kipenzi Tito kwamba ndiye
aliyeziiba pesa zangu? Unathubutu kumwita mwanangu kipenzi
Tito mwizi?” Bi. Upanga alishindwa kustahimili.
“Titooo! Tito mwanangu njoo huku!” Bi. Upanga aliipaza sauti
yake mbovu kumwita mwanawe.
Kufumba na kufumbua,Tito, kijana mwenye mwili mnene kama
kiboko alitokeza.Alikuwa akiendesha baiskeli aliyonunuliwa na
baba yake Mzee Chozi wiki kadhaa zilizopita.
“Kwa nini wanikatizia starehe zangu mama?Yaani hutaki kunipa
muda nifurahie kuendesha baiskeli?” Tito alimuuliza mama yake
akighadhabika.
“Samahani mwanangu kipenzi Tito. Kuna pesa zangu zilizokuwa
juu ya meza katika chumba changu cha kulala. Sasa hazipo.
Uliziona?”
“Mama, usijitaabishe kuzitafuta pesa hizo. Nani mwizi katika
nyumba hii isipokuwa Taabu? Wewe Taabu, utakana kwamba
50
nilikuona jana ukiingia na kutoka katika chumba cha mama?
Utakana hilo? Mpe mama pesa zake na uombe msamaha sasa
hivi!” Tito alishikilia msimamo wake akimwelekeza Taabu kidole.
“Mama, niamini kwamba sikuingia katika chumba chako. Ni Tito
aliingia na nilimwona kwa macho yangu haya,Taabu alisimama
kidete na kujitetea.
Bi. Upanga alijivuta na kusimama. Lilikuwa jimama lenye uzito wa
tembo kutokana na kula vyakula vyenye mafuta na kutofanya
kazi nzito.
“Tito mwanangu, kaniletee kitabu changu kile kikuukuu, Bi.
Upanga alimtuma mwanawe.
“Vilevile, kaniletee ile kalamu yangu ya wino, Bi. Upanga aliagiza.
Taabu alipojua kile alichopania kufanya mama yake, alijitupa
miguuni pake na kuanza kuomba msamaha. Alilia na kumsihi
lakini kilio chake kiliangukia masikio yaliyotiwa nta. Bi. Upanga
hakutaka kumsikiliza. Kila mara Taabu alipofanya makosa, Bi.
Upanga aliagizia kitabu hicho na kuweka rekodi ya makosa
aliyofanya maskini Taabu.
Baba yake Taabu Mzee Chozi alikuwa na mazoea ya kuulizia
makosa yoyote aliyofanya mwanawe kila alipofika nyumbani.
Ajabu ni kwamba Bi. Upanga aliyarekodi makosa yaTaabu lakini
hakufanya hivyo pindi Tito alipokosea. Mara tu Mzee Chozi
alipopewa kitabu kile na kuyapitia makosa yote, kwa kila kosa
alimwadhibu mwanawe Taabu bila huruma.Alikuwa Mzee asiye
na chembe ya huruma ndio maanaTaabu alihuzunika sana wakati
mama yake alipoagizia kitabu hicho.
51
...alijitupa miguuni pake na kuanza kuomba msamaha.
52
“Tangu mwanzo uliposikia nikiuliza kuhusu pesa zangu, ungekiri
mara moja bila hofu kwamba ni wewe uliyezichukua badala ya
kumsingizia kipenzi mwanangu.Yaani, mwanaharamu wewe
unamsingizia mwananguTito wizi? Unatamani awe mwizi kama
wewe? Leo baba yako atakuonesha kilichomfanya sangara
kuchomwa moto, Bi. Upanga alimtisha Taabu.
Kitabu kikuukuu kililetwa pamoja na kalamu ya wino.Tito akiwa
kwenye kilele cha furaha alimpokeza mama yake vitu hivyo
viwili kisha akasimama kando kuona kile mama angemfanyia
kaka yake. Bi. Upanga naye alivipokea vitu hivyo huku akiwa
mwingi wa uchungu.Aliweka kitabu kwenye paja lake nene kisha
akakamata kalamu na kumtazamaTaabu aliyekuwa amelia hadi
machozi yakamkauka machoni.
“Sogea hapa mara moja!” alimwamuru Taabu naye akatii.
“Wanililia mimi umekuwa mtoto mchanga wa kunyonyeshwa?
Nilishakuonya mara nyingi kuhusu tabia zako lakini ukawa
huambiliki husemezeki. Utajuta leo, Bi. Upanga alionya.
“Kumbe! Nilikuwa nimesahau kuweka rekodi ya makosa yako
tangu mwanzo wa wiki na maadam umeniudhi kupita kiasi,
hata umenikumbusha kwamba ni jukumu langu kumpasha baba
yako kila kosa unalolifanya. Utajua maana ya methali majuto
ni mjukuu huja kinyume. Haya, sema kuanzia majuzi makosa
yote uliyoyatenda!” Bi. Upanga alipaza sauti kavu, sauti ya juu
iliyoyaumiza masikio ya Taabu.
“Haya, anza kukiri kila kosa ulilofanya! Ukithubutu kunificha kosa
hata…hata moja tu hivi, utajuta kwa nini ulizaliwa. Ni lazima
baba yako leo asikie jinsi unavyozidi kuchakaa kitabia kila uchao.
“Mama, unajua mimi si kijana mkorofi. Mimi hujaribu kadri ya
53
uwezo wangu kutenda kila kazi hapa nyumbani bila malalamishi.
Kwa makosa niliyoyafanya mama, naomba msamaha.Tafadhali
usimwambie baba asije kuniua maskini mie, Taabu aliomba
akimpigia magoti mama yake.
Bi. Upanga hakumsikiliza.Alilitumia guu lake kumsukuma Taabu
ambaye wakati huo machozi yalikuwa yakimtoka njia mbilimbili
na kamasi kumvuja puani.
“Sema makosa yako! Sina wakati wa kukusikiliza mie, Bi. Upanga
alichemka kwa hasira.
“Basi…ba.si mama, Jumapili nilisahau kuweka chai sukari
sawasawa ikakolea. Juma..Jumatatu, nilisahau kununua mikate
miwili nikanunua mmoja, Taabu alisita na kunyamaza.
“Endelea…Taja makosa yote uliyofanya ama nikufanye kengeza,
mtoto mpumbavu wewe, Bi. Upanga alizidi kumzomea Taabu.
“Ju..Jumanne nilipoteza shilingi kumi ulizonituma kununua chumvi.
Jumatano nili…nilisahau kuanua nguo zikanyeshewa. Jana Alhamisi
pesa zako zilipotea japo si mimi niliyezichukua. Hala…”
Kefle! Kama si wewe uliyezichukua basi mwizi ni nani? Unataka
niandike nani mwizi wa pesa zangu hapa kitabuni? Kiri mara moja
wewe ndiwe uliyeziiba au nikukate midomo yote miwili kwa kisu.
Sema sasa hivi!” Bi. Upanga alikuwa amefikia upeo wa ghadhabu.
“Basi Alhamisi ni…ni mimi niliiba pesa zako katika…katika chumba
cha kulala. Na leo Ijumaa nimekuwa mdanganyifu kwamba si
mimi niliyeziiba pesa zako, Taabu alishusha pumzi, akasimama
mahali pale akimtumbulia mama yake macho asijue la kufanya.
“Ukaidi wako umezidi. Kila siku ina kosa lake. Nakuapia utajutia
54
upumbavu wako huu.
“Mama, mara nilizosahau hiki au kile ulikuwa umenipa kazi
nyingi mara moja hadi nikasahau. Si mapenzi yangu kutofanya
kazi ambayo umenipa,Taabu alijipigania kwa mara ya mwisho
kusudi mama amwonee imani.
Ilikuwa furaha na fahari kubwa kwa Bi. Upanga kuona Taabu
akipata tabu. Aliandika kwenye lile buku makosa yote kisha
akamtuma mwanawe Tito kukiweka kitabu katika chumba cha
kulala.Taabu alipangusa machozi yaliyomshuka mashavuni njia
mbilimbili akijua waziwazi kwamba pindi baba yake akipewa
kitabu hicho, bila shaka angekuwa katika shida nyingi.
“Kosa la kuiba pesa zangu ndilo limenifikisha kilele cha hasira.
Isingekuwa wizi wako, ningekusamehe makosa yale mengine
madogo madogo ambayo umefanya lakini…hili la wizi…siwezi
katu kukusamehe. Lazima baba yako ajue ushakuwa jizi. Kuanzia
leo, hutawahi kuziiba pesa zangu. Utakuwa ukiziona na kuzimezea
mate tu, mama alimzomea.
Bi. Upanga alimwita mwanawe Tito na wawili hao wakaondoka
na kumwacha Taabu mahali pale, chozi kifua tele, maumivu ya
moyo na usumbufu wa akili ukizidi kumtesa.
“Mwanangu Tito, tumwache mjinga huyu hapa. Kuna kilo ya
nyama nilinunua jana. Njoo tukaipike baba yako akija alasiri
apate ikiwa tayari, Bi. Upanga alimwambia mwanawe huku
wakielekea jikoni.
Huku harufu ya nyama iliyokuwa ikikaangwa ikilitesa tumbo
la Taabu, mawazo yake yalikuwa mbali..mbali mno. Hakika
aliumia kwa njaa. Kila siku alikula makombo. Kila siku Bi.Taabu
alimzomea na kumtusi Taabu. Alimwambia waziwazi kwamba
55
asingefanikiwa maishani hata akifanya bidii za mchwa. Bi. Upanga
alikuwa na maneno makali kuliko upanga. Kila kosa lililotokea
hapo nyumbani,Taabu alisingiziwa na kuadhibiwa.Taabu akaishi
maisha ya tabu na kukosa amani, amani aliyoitafuta hata asiipate.
Taabu alikumbuka yaliyopita na machozi mengi yakazidi kumtoka.
Yalikuwa ni machozi ambayo yangejaa kikombe hadi pomoni.
Alilia hadi macho yakawa mekundu kama kaa la moto. Baba yake
mzazi Mzee Chozi alikuwa amemwoa mama yake mzazi Bi. Shida
zamani. Tito alipozaliwa, alikuta baba na mama wakiishi kwa
furaha na amani. Mzee Chozi alikuwa akifanya kazi ya udereva
katika kampuni moja iliyohusika na utengenezaji wa mafuta ya
kupikia. Mzee Chozi alifanya kazi kwa bidii na kuchukua mikopo
ya kufanya shughuli za maendeleo. Akajenga jumba zuri na
kununua mashamba.Akamfungulia mkewe Bi. Shida biashara ya
uuzaji bidhaa za elektroniki naye Bi. Shida akapata pesa nyingi.
Taabu alilelewa kwa upendo.Alikula chakula kizuri na akapelekwa
katika shule nzuri ya kibinafsi iliyoitwa Akili Pevu. Huko akasoma
kwa bidii kama mchwa na kuondokea kuongoza katika kila mtihani
waliofanya. Walimu wakampenda na wanafunzi pia kutokana
na tabia zake nzuri. Hali ilibadilika wakati Bi. Shida alipougua.
Aliugua ugonjwa wa saratani. Ni ugonjwa ambao uligunduliwa
baadaye kwani ulikuwa umemla sana. Madaktari walimtibu lakini
Bi. Shida hakuonesha dalili za kupata nafuu.
Madaktari waliposhindwa, Bi. Shida alirudishwa nyumbani.
Mumewe alimshughulikia kadri alivyoweza lakini mwishowe
Bi. Shida alizidiwa na ugonjwa akaaga dunia. Kifo cha Bi. Shida
kilimliza sana Taabu.Alimpenda mama yake na kuondokewa na
mama angali kijana mdogo kulimuuma sana. Mazishi ya Bi. Shida
yalihudhuriwa na halaiki ya watu kwa kuwa alikuwa mama
mwenye moyo mweupe kwa kila mmoja awe mdogo au mkubwa.
56
Baada ya mazishi na muda wa mwaka mmoja na nusu kupita,
Mzee Chozi alioa mke mwengine. Aliitwa Bi. Upanga. Huyo
ndiye aliyeanza kuyafanya maisha ya Taabu kuwa magumu.
Huyo ndiye aliyeyabadilisha maisha ya Taabu kabisa. Furaha
aliyokuwa nayoTaabu ikaisha. Uchangamfu aliokuwa naoTaabu
ukaisha. Mabadiliko makubwa mno yakatokea katika maisha ya
Taabu. Ilikuwa nadra mno kwa Taabu kusemekana alifanya hiki
au kile vibaya lakini mama yake huyo wa kambo akawa haishi
kumsingizia mambo kusudi baba yake amchukie. Na hakika,
alifanikiwa. Mzee Chozi alimsikiliza mkewe sana. Akaondokea
kumchukia mwanawe Taabu na kumwona kama mzigo.
Bi. Upanga alihakikisha kwamba Mzee Chozi alimhamisha
Taabu kutoka katika shule ya kibinafsi ya Akili Pevu alikosomea
hadi katika shule ya umma kwa jina Elimika iliyokuwa karibu.
Mwanawe Tito alikuwa akisomea katika shule ya umma. Tito
alikuwa ni kijana aliyelelewa kwa malezi mabovu na malezi
hayo yakamharibu. Hakuwa na tabia nzuri.Alikuwa haambiliki
hasemezeki. Kilichomkasirisha sana Bi. Upanga ni akili nyepesi
aliyojaaliwa Taabu. Kila mtihani uliofanywa, Taabu aliongoza
na kushangiliwa huku Tito akivuta mkia na kukashifiwa. Tito
alikuwa goigoi, kijana mzembe hivi kwamba hata kuandika jina
lake kulimshinda. Vijana hao walikuwa katika gredi ya tano
wakijiandaa kujiunga na gredi ya sita wafanye mtihani wa kitaifa.
“Mume wangu, sioni faida ya kuendelea kumlipia Taabu karo.
Naonelea akifanya mtihani wa mwisho wa kitaifa wa gredi ya
sita, masomo yake yafikie mwisho.Anaweza kufundishwa namna
ya kujitafutia riziki kama vile kutemakuni, kufinyanga vyungu
au kuchoma makaa, Bi. Upanga alipendekeza naye mumewe
hakulipinga pendekezo hilo.
Hayo yote aliyakumbuka Taabu akiwa mahali pale alipoachwa
57
akisimama na mama na kaka yake.
“Kweli wasemavyo wahenga, mama ni mama hata kama ni
rukwama. Mama yangu alipokuwa hai, sikupata taabu hii. Nateseka
kwa kuwa mama yangu mzazi aliondoka duniani.Alifunga safari
isiyo na marejeo. Lau mama angalikuwa na uwezo wa kuamka
kutoka pale alipolala kaburini, shida hizi zote kwangu zingekuwa
ni kama simulizi ya hadithi. Hata hivyo, Mungu si Athumani na
maisha yangu yajayo yapo mikononi mwa Mungu,Taabu alisema
kimoyomoyo kwa uchungu mwingi.
Taabu aliondoka mahali pale na kuingia katika chumba chake
cha kulala. Alianza kuzikunja nguo zake alizokuwa amezifua
alfajiri ya siku hiyo. Hazikuwa nguo nzuri kama za Tito lakini
alizikunja vizuri.Yalikuwa ni mavulia aliyopewa na Tito baada
ya baba kuchelea kumnunulia nguo mpya.Alipomaliza kuziweka
nguo zote sandukuni, alijilaza kitandani na muda mfupi baadaye
akabebwa na wimbi la usingizi.
Tito alipozinduka, ulikuwa ni wakati wa alasiri.Alizinduka akitokwa
na jasho jingi na mwili kumtetema. Alidhani alikuwa na homa
kali ya malaria.Alizinduliwa na sauti mbovu ya baba yake.Tangu
mkewe wa kwanza Bi. Shida kuaga dunia, Mzee Chozi alianza tabia
ya kulewa chakari.Alikuwa akilewa kila siku na majukumu mengi
ya familia akampokeza mkewe. Bi. Upanga alipoona akipokezwa
majukumu hayo, alihakikisha kwamba mumewe alizidi kumchukia
mwanawe Taabu.
“Yu wapi huyo ninayesikia amekataa kumtii mama yake?Yu wapi
huyo Taabu anayefanya nipigiwe simu nikiwa kazini ati ameota
pembe za ukaidi? Mzee Chozi aliuliza kwa sauti kali kama ya radi.
Taabu alitetemeka zaidi.Alijua baba yake alipokasirika, aligeuka
58
kuwa mkali kama simba.Taabu angalikuwa na uwezo, angalitoka
chumbani na kutoweka ghafla.Angalikuwa na mbawa angaliruka
asionekane tena.
“Nasikia siku hizi unamkosea mama yako heshima! Ni kweli?”
Mzee Chozi alinguruma.
“Baba, mimi ni kijana mwema na katu sijawahi kumkosea heshima
mama yangu Bi. Upanga. Niamini baba,Taabu alimsihi baba yake.
“Kwa hivyo, unataka kusema mama yako ni mwongo? Unataka
niamini kuwa mama yako ananidanganya? Kwa nini unaiba pesa
zake? Ni chakula hupati hapa nyumbani? Kwa nini umekuwa
kijana kaidi kama punda?” Mzee Chozi alizidisha maswali.
Taabu alishindwa kuyajibu maswali hayo. Alinyamaza kama
bubu. Ni mara nyingi alizojaribu kujitetea lakini baba yake
asingemwamini. Kwa hivyo aliona kwamba juhudi zake za kuusema
ukweli zisingemfaa kwa lolote au chochote.
“Kutokana na ukaidi wako, lazima nikuadhibu kama njia mwafaka
ya kuzikata pembe kali ambazo zimeota. Kuanzia leo, utakuwa
ukiamka saa kumi alfajiri badala ya saa kumi na moja. Zipo kazi
nyingi za kufanya wakati huo kama kufua nguo, kuzianika, kupiga
deki pamoja na kuandaa kiamshakinywa kwa watu wote wa
familia. Hutaandamana nasi katika safari ya kuzuru nchi jirani
ya Tanzania tuliyoipangia mwanzoni mwa mwezi ujao.Vilevile,
zawadi ya baiskeli niliyokuwa nimekuahidi hutaipata ijapokuwa
ulikuwa nambari ya kwanza darasani. Ujuavyo, kila mwezi mimi
huwapa pesa kiasi fulani ukiwa na kaka yako Tito kusudi muweke
akiba. Kuanzia mwisho wa mwezi huu, sikupi pesa hizo hadi nione
tabia zako zimebadilika. Haya, ondoka mbele yangu mara moja!”
Mzee Chozi alisema kwa sauti kali.
59
“Zipo kazi nyingi za kufanya waka huo kama kufua nguo, kuzianika,...
60
Huo ndio uliokuwa mwanzo mwingine wa matatizo mengi
katika maisha ya Taabu. Licha ya shida hizo, alijikaza kisabuni.
Alivyoahidi baba yake,Taabu hakuandamana nao katika safari za
kuzuri kwingi kuzuri.Aghalabu aliamka alfajiri kuu kufanya kazi
mbalimbali kabla ya kujiandaa kwenda shuleni. Kupigiwa kelele
na kutukanwa kukawa jambo la kawaida ambalo halikumkaa
moyoni. Alipofanya mtihani wa mwisho katika gredi ya sita,
alikuwa amefuzu kwelikweli. Kila mmoja alimmiminia sifa na
shule ya msingi ya Elimika ikanawiri na sifa zake kusikika mbali.
Kufuzu kwa Taabu hakukufurahiwa na kila mmoja. Bi. Upanga
aliumia ndani kwa ndani kwa kuwa mwanawe Tito alikuwa
miongoni mwa wanafunzi wachache ambao walianguka mtihani
huo na kuvuta mkia.Alikuwa tayari kumshauri mumewe asimlipie
karo Taabu.
“Iwapo mwanangu Tito hakufaulu, vipi nimlipie karo chokoraa
huyu nimwitaye mwanangu? Nitahakikisha kwamba hatauona
mlango wa elimu ya sekondari, Bi. Upanga alisema huku akiuma
mdomo wa chini.
Taabu alikonda kutokana na fikra nyingi alipotangaziwa ghafla
kwamba asingepelekwa katika shule ya upili. Taarifa hizo
zilimvunja moyo hasa alipowaona vijana wengi aliowashinda
darasani wakibeba masanduku walimopakia nguo na vitabu
wakienda kujiunga na shule za upili. Kila siku,Taabu aliamshwa
alfajiri kuu na mama yake kuenda kutemakuni na kuziuza. Kile
alicholipwa kiliingia mikononi mwa mama yake na hakufaidika
kwa senti hata moja. Zaidi ya changamoto zote hizo, Taabu
alizidi kumwomba Mwenyezi Mungu kwa matumaini na imani
akiamini kuwa mvumilivu hula mbivu. Siku moja, aliporejea jioni
akiwa mchovu, ilisadifu kwamba wageni wasiotarajiwa walifika
nyumbani kwao.Wageni hao walijitambulisha naye Mzee Chozi na
61
mkewe wakawakaribisha kwa moyo mkunjufu. Baada ya kunywa
kahawa na kuzungumza mengi, ndipo mmoja wao alielezea hasa
sababu kuu ya kuitembelea familia ya akina Taabu.
“Mzee Chozi na Bi. Upanga, tumefika huku tukiwa na haja ya
kumchukua Taabu.Tulivyosema awali, sisi hulifanyia kazi shirika
lisilo la kiserikali liitwalo Mageuzi. Ni shirika linalohusu kutoa
msaada kwa wale watoto ambao hawajabahatika maishani. Iwapo
mtatukubalia, tuna mpango wa kumsaidia Taabu. Tutampeleka
katika makao yetu maalum ambako ataweza kufanikisha ndoto
yake ya kuwa daktari maishani, mwakilishi huyo wa shirika la
Mageuzi alisema akimpokeza Mzee Chozi karatasi fulani asome
na kuzitia sahihi.
Taarifa hizo zilimtia furaha tele Mzee Chozi na mkewe Bi.
Upanga. Kwao Taabu alikuwa mzigo na walionelea bora aondoke
wapate starehe walizotamani.Taabu alichukuliwa na shirika hilo
na kujiunga na shule ya upili iliyoitwa Faulu.Alisoma kwa bidii
akiwa na lengo la kuwa daktari, ilivyokuwa ndoto yake angali
mdogo.Aliwashangaza walimu na wanafunzi kwa kupita mitihani
yote bila kusahau kuonesha kipawa chake cha uchezaji soka.
Miaka minne baadaye, alifanikiwa kujiunga na chuo kikuu. Huko
hakulegeza juhudi zake. Muda ulipita naye Taabu akajipata akiwa
katika mwaka wake wa mwisho chuo kikuu. Alifua dafu katika
kozi ya udaktari. Shirika lilo hilo la Mageuzi nalo likamsaidia
kuenda kusomea nchini Marekani.
Taabu aliishi nchini Marekani kwa muda mrefu.Alimaliza masomo
yake na kuwa daktari maarufu.Aliajiriwa huko na kufanya kazi
akiendelea kupata ujuzi hadi akawa daktari mwenye ujuzi wa
kutosha.Alipokuwa na hakika alishapata alichotamani maishani,
aliandika barua ya kuomba uhamisho naye akaruhusiwa kurejea
nyumbani. Serikali nayo ilimpa cheo cha kusimamia hospitali kuu.
62
Taabu alijaaliwa kuoa mke ambaye alifanya kazi ya uuguzi na
wakabarikiwa kupata wana wawili, mmoja wa kike na mwengine
wa kiume. Huku hayo yakiendelea, kuna jambo lililokuwa
likimsumbua sana Taabu. Alitamani kuwasiliana na baba yake
mzazi lakini hakuwa na nambari yake ya simu.Alikuwa ameenda
mara kadhaa mahali walipoishi zamani yaani kule alikokulia
lakini hakuwapata. Aliwapata majirani wapya waliomwambia
hawakumjua mtu aliyemwulizia kwa jina Mzee Chozi. Taabu
akaanza safari ndefu ya kuitafuta familia yake asijue ilikokuwa.
Siku moja, wakati alipokuwa akitoka katika afisi yake humo
hospitalini, aliona mwanamume mzee akisukuma kijigari
kilichokaliwa na mgonjwa. Alimtazama yule mzee kwa muda
kisha mgojwa aliyekuwa amezidiwa na maradhi na kukonda sana.
Aliwaonea huruma na machozi yakamdondoka. Mbona machozi
yalimdondoka? Ni wagonjwa wangapi aliokuwa ameshuhudia
wakiaga dunia na hakuingiwa na hisia za kulia? Mbona hao wawili
mzee na mkewe wakamchochea kutamani kulia? Hao walikuwa
ni kina nani? Aliagiza waingie katika afisi yake.
Taabu alitambua kwamba mzee huyo alikuwa ni baba yake
mzazi, Mzee Chozi. Pia aligundua kwamba bikizee aliyekalia
kiti cha magurudumu akizidiwa na ugonjwa alikuwa ni mama
yake wa kambo, Bi. Upanga.Wote watatu waliangua vilio mle
afisini mara tu Taabu alipojitambulisha. Taabu alilia kwa yote
yaliyopita kwa kuwa alikuwa amewasamehe.Wazazi hao nao
walilia walipokumbuka mabaya waliyomtendea mwanaoTaabu.
“Baba na mama, husemwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.
Mimi nilikwishawasamehe kitambo. Nanyi msiwe na ugumu
mioyoni mwenu. Naomba tuanze mwanzo mpya familia yetu iwe
na furaha na msingi wa amani, Taabu aliwaomba.
63
“Baba na mama, husemwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo...
64
“Twashukuru, mwanangu. Mama yako hapa ndiye kaugua miaka
kadhaa iliyopita nami nikazidiwa na gharama za hapa hospitalini,
Mzee Chozi alisema.
Taabu alipata kujua mama yake wa kambo Bi. Upanga alikuwa
ameugua kansa lakini haikuwa imesambaa mno mwilini.Alimtuliza
moyo baba yake kwa ahadi kwamba angesimamia bili za matibabu
ya Bi. Upanga. Bi. Upanga alipelekwa nchini India na miezi
kadhaa baadaye akarejeshwa akiwa tayari kapata nafuu kabisa.
Tito aliyekuwa nusra kuingiwa na wendawazimu kutokana na
matumizi ya dawa za kulevya, alifanyiwa mpango na nduguye
Taabu akapelekwa katika kituo cha urekebishaji tabia. Miezi sita
alitoka naye Taabu akampeleka kozi ya useremala alikofuzu
vyema na akamwanzishia karakana kubwa ya utengenezaji
wa samani.
Furaha ya awali kabla ya kufariki kwa Bi. Shida ilirejea katika
familia ya Mzee Chozi. Ilikuwa ni furaha baada ya kusameheana
baina ya Taabu na jamaa zake.Waliishi wakikumbuka kwamba
kumcha Mungu lilikuwa jambo la maana sana maishani mwao.
65
Kamusi Yangu
akichanja akipasua kitu kama kuni kwa shoka
akighadhabika akikasirika
alimzomea alimtolea maneno makali
alisimama kidete alisimama imara kutetea alilosema
buku aina ya kitabu kikubwa
chokoraa mtoto asiye na makao ambaye huishi
mitaani
karakana mahali ambapo seremala au mafundi
mbalimbali hutengenezea bidhaa zao
kefle neno linalotumiwa kumnyamazisha
mtu
kengeza mtu mwenye macho ambayo mboni
zinatazama upande
kupiga deki kusafisha sakafu kwa kutumia
tambara, maji na sabuni
makombo chakula kinachobaki baada ya watu
kula
mavulia nguo ambazo zimeshavaliwa na mtu
husaidiwa na mwingine kuendelea
kuzivaa
mwanaharamu mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa
samani vitu vinavyotengenezwa kwa mbao;
fenicha
sangara aina ya samaki
saratani aina ya ugonjwa; kansa
yakamdondoka yakamtoka tone baada ya jingine
66
Maswali
1. Kwa nini Bi. Upanga alikuwa akimwita Taabu kwa sauti kali?
2. Taabu alipoitwa na mama yake alikuwa akifanya nini?
3. Kwa nini Taabu alimwangukia mama yake miguuni alipoagizia
kitabu kikuukuu?
4. Bi. Upanga alimsingizia mwanawe Taabu nini?
5. Ni adhabu gani Mzee Chozi aliyompa mwanawe Taabu
alipofika nyumbani?
6. Ni jambo lipi lililomfika mama wa Taabu wa kumzaa?
7. Wazazi wa Taabu walipokataa kumwelimisha, alibahatika
vipi?
8. Ndoto ya Taabu tangu udogoni ilikuwa gani?
9. Taabu alikuwa mzuri masomoni na vilevile alikuwa na kipawa.
Elezea kipawa hicho.
10. Ni funzo gani unalopata katika hadithi hii?
67
Nuru Mlemavu
68
Hapo zamani za kale, paliondokea msichana aliyeitwa Fatuma.
Fatuma alilelewa na wazazi maskini.Alikuwa msichana mrembo
sana kijijini. Kijiji chao kiliitwa kijiji cha Songole. Kilikuwa ni
kijiji kikubwa mno. Katika nchi nzima ya Miale, Songole ndicho
kilichokuwa kijiji kikubwa na chenye idadi kubwa ya watu. Hata
hivyo, wakazi wa kijiji cha Songole walikuwa maskini kupindukia.
Wengi wa wakazi walikuwa na mashamba madogo. Wengine
walikuwa wavuvi, watemakuni na wafinyanzi.
Baba wa Fatuma aliitwa Mzee Tonje.Alikuwa ni mvuvi. Mama wa
Fatuma Bi. Zuhura naye alifanya kazi ya kutema kuni. Mzee Tonje
alivua usiku baharini na kurejea nyumbani asubuhi. Bi. Zuhura
naye alitema kuni na kuzipeleka sokoni kila siku. Kuna nyakati
MzeeTonje hakujaaliwa samaki na upo wakati Bi. Zuhura alikosa
mtu wa kununua kuni zake.
Fatuma alikuwa na wakati mgumu kuwaelewa wazazi wake.
Alikua akitamani laiti angalikuwa amezaliwa katika familia tajiri.
Aliichukia hali ya umaskini ya wazazi wake. Alitamani kuishi
maisha ya kifahari ambayo wazazi wake wasingemudu.
Fatuma alikuwa na ndoto nyingi za kufanikiwa maishani. Mojawapo
ya ndoto hiyo ilikuwa ni kuolewa kwa mwana wa Mfalme
aliyeitwa Mwangaza. Mfalme wa nchi hiyo aliitwa Mfalme Fikirini.
Mwangaza ndiye alitarajiwa kupokezwa mamlaka pindi baba
yake akifariki. Kuna nyakati fulani Fatuma alikumbuka Mwangaza
alipokitembelea kijiji chao akimwendesha farasi mzuri mwenye
nguvu. Kila mwanakijiji alijitokeza siku hiyo kumwona mwana
wa Mfalme.Walikuwapo watoto, vijana, kina mama, kina baba
na hata wazee hawakubaki nyuma. Mwangaza alikuwa amevalia
kanzu iliyotiwa nakshi za dhahabu na viatu vizuri. Alijifunga
kichwani kwa kilemba kizuri.Alipendeza sana.
69
Fatuma alikuwa na ndoto nyingi za kufanikiwa maishani.
70
Mwangaza aliwasalimu watu kwa kuwapungia mkono wake.
Wakazi wa Songole walimshangilia kama mwanasiasa. Alipita
polepole kijijini kisha akaondoka kwa kasi. Wakazi hawakujua
kile kilichomleta Mwangaza kijijini.
“Siku moja ningetamani kuolewa kwa Mwangaza niwe mke
wake, Fatuma alijisemea moyoni. Hakutaka kumweleza yeyote
wa rika lake ndoto yake.
Baada ya miaka michache, kulingana na utamaduni wa jamii,
Fatuma na wasichana wa rika lake walifikia umri wa kuolewa.
Ngoma zilipigwa usiku kucha. Maandalizi yalifanywa. Jambo hilo
lilimkasirisha Fatuma sana.Alitamani kutoroka nyumbani lakini
angetorokea wapi? Ilikuwa ni lazima aolewe na wazazi wake
kuletewa mahari. Basi alijitokeza mwanamume mmoja aliyeitwa
Kala. Kala alikuwa akifanya kazi ya kusuka mikeka na kufuma
vikapu. Huyo ndiye aliyetoa mahari kwa wazazi wa Fatuma.
Fatuma aliolewa shingo upande.
Mwaka mmoja baadaye, Fatuma alijaaliwa ujauzito. Hata hivyo,
licha ya kuolewa na Kala, bado ndoto yake ya kuwa mke
wa Mwangaza mwana wa mfalme haikumtoka akilini. Siku ya
kujifungua ilipofika, alijaaliwa mwana wa kiume aliyemwita Nuru.
Lo! Mambo hayakuwa mazuri. Nuru alikuwa na ulemavu wa
miguu. Mtoto alinyonyeshwa lakini ulipofika wakati wa kujifunza
kutambaa, asingeweza. Miguu yote miwili haikuwa na nguvu.
Wanakijiji wengi walimcheka sana Fatuma na mumewe Kala. Hii
ni kwa sababu iliaminiwa wazazi waliojaaliwa mtoto mlemavu,
walikuwa na kasoro fulani. Pia iliaminiwa mtoto huyo angewaletea
kisirani. Kwa hivyo, mtoto huyo alistahili kuuawa. Fatuma
alihuzunika sana. Dharau aliyooneshwa na hata marafiki zake
ilimuuma sana moyoni.Aliondokea kumchukia mwanawe Nuru.
71
Alianza kumlaumu Mungu kwa nini alimjaalia mtoto mlemavu
ambaye hakupendwa kijijini.
Fatuma na mumewe waliishi maisha ya upweke na ufukara.
Licha ya Kala kujibidiisha kusuka mikeka na kufuma vikapu,
hakuna mwanakijiji aliyetamani kuwanunulia bidhaa zao. Ilimbidi
Kala kusafiri maeneo ya mbali kuuza bidhaa zake. Walikosa
wageni kabisa na waliishi kana kwamba hawakuwa na majirani.
Hata wazazi wa Fatuma na mumewe Kala hawakuthubutu
kuwatembelea.
“Mume wangu, tunaishi maisha ya dhiki kwa sababu ya Nuru.
Nimechoka kutukanwa na wenzangu kwa sababu ya mtoto
huyu. Mbona tusimuue jinsi tulivyoshauriwa na wazee wa kijiji?”
Fatuma alimuuliza mumewe.
“Si vyema kumuua Nuru. Nuru ni mwanangu. Hata kama ana
ulemavu, ni mwanangu na nampenda sana. Nisingefurahi kuona
tukimtesa. Kumbuka Mwenyezi Mungu ndiye mwenye uwezo wa
kutoa na kutwaa.Yeye ndiye aliyetupatia Nuru na alikuwa na
sababu maalum ya kufanya hivyo, Kala alimjibu mkewe.
Baada ya muda usiokuwa mrefu, Kala aliugua ugonjwa wa ajabu.
Alilalamika kuumwa kichwa na tumbo. Ugonjwa huo ulimkondesha
na hakuweza kufanya kazi tena. Hatimaye Kala aliaga dunia.
Wanakijiji walisema mengi baada ya kifo cha Kala. Baraza la
wazee lilikutana na kujadiliana mambo mengi. Fatuma aliitwa
mbele ya baraza hilo la wazee.
“Tuliwaonya wewe na mume wako Kala kuhusu mtoto wenu
lakini mkakosa kutusikiliza. Sasa tazama, tumeshamzika mumeo
Kala umebaki mjane kwa sababu ya kutotii ushauri wetu. Iwapo
unatamani kuendelea kuishi hapa kijijini, ni lazima ukubali ushauri
72
wetu. Mwanao Nuru ni lazima afe.Ameshindwa kusimama licha
ya kufikisha umri wa miaka minne.Anaweza tu kuburuta miguu
yake na kutambaa chini ijapokuwa anajua kuzungumza. Baada ya
siku tatu, mchukue uende ukamwache kwenye msitu mkubwa,
wazee walishauri kisha wakatawanyika.
Fatuma alifurahia uamuzi wa wazee. Muda wote huo tangu
alipojifungua Nuru, alitamani kumuua lakini mumewe akamzuia
kwa sababu alimpenda Nuru sana. Kala alishazikwa na asingemzuia
kulitenda lile lililowapendeza wazee wa kijiji.
Siku tatu baadaye, Fatuma alitayarisha chakula kitamu sana
kisha akakitia katika mkebe.Alimwogesha mwanawe na kumvika
nguo maridadi.
“Mama, sijawahi kuona ukitamani kuniogesha niwe safi. Leo kuna
nini? Pia sijawahi kuona ukinivika nguo mpya. Je, kuna sherehe
leo hapa nyumbani?” Nuru aliuliza.
“La mwanangu. Leo tuna safari ndefu sana mbele yetu. Nataka
tutoke hapa kijijini twende safari kisha turudi kabla ya jioni,
Fatuma alimjibu mwanawe.
Alichukua leso kisha akaitumia kumfunga na kumbeba mgongoni.
Nuru alifurahia sana. Tangu azaliwe, hakuwahi kutoka kijijini.
Alifurahia kuona miti na milima. Alifurahia kuona maua na
wanyama kama sungura na kulungu.
“Mama, msitu huu unapendeza sana. Ningetamani sana kuishi
mahali ninapowaona wanyama kila siku, Nuru alimweleza mama
yake ambaye naye alishangazwa na jibu la mwanawe.
Baada ya safari ya muda mrefu, kufikia adhuhuri, waliwasili
kwenye msitu huo mkubwa. Fatuma alifuata njia kubwa iliyoingia
73
msituni hadi akajipata katikati ya msitu. Hakukuwa na watu.
Kote kulikuwa na ukimya wa kutisha. Fatuma alionekana kuwa
na hofu na wasiwasi.
“Mama, mbona unaonekana kuwa na wasiwasi? Tungehama
kijijini na kuja kuishi mahali kama hapa pasipo na watu wenye
wivu na kiburi, ningefurahi sana, Nuru alisema.
“Mwanangu, unapapenda mahali hapa? Mimi pananiogofya sana,
Fatuma alijibu.
“Naam, napapenda sana mama. Mimi sitaki kurejea kijijini. Najua
wewe unauogopa msitu lakini mimi ninaupenda. Ukiniacha hapa,
nitafurahia sana, Nuru alimshangaza Fatuma.
“Mwanangu, ikiwa hivi ndivyo unavyopenda, basi nitakuacha.
Nasikitika kukuacha hapa na kurejea kijijini lakini mwenyewe
umesema unatamani kuishi mahali kama hapa, Fatuma alisema
akitokwa na machozi.
“Ndio mama. Napenda kuishi mahali kama hapa penye utulivu.
Tangu nilipozaliwa, kitu gani kizuri nimeona kule kijijini Songole?
Wanakijiji wananichukia. Wanakijiji wananidharau. Wanakijiji
waliamua kutowatembelea wewe na marehemu baba kwa sababu
yangu.Wazee wa kijiji nao wananichukia kutokana na hali yangu
hii ya ulemavu. Hata wewe mama, najua katika moyo wangu
hunipendi.Aliyekuwa akinipenda kwa moyo wake wote alikuwa
ni baba naye ameshafariki. Ondoka mama. Ondoka urejee kijijini.
Usije ukanisikitikia. Mimi nikiwa hapa, niko nyumbani salama u
salmini, Nuru alizidi kumpumbaza mama yake kwa maneno yake.
Yalikuwa ni maneno mazito ambayo hayakutarajiwa kusemwa
na mtoto mdogo kama Nuru.
74
Baada ya kulia kwingi, hamaye Fatuma aliondoka.
75
Baada ya kulia kwingi, hatimaye Fatuma aliondoka. Aliondoka
machozi mengi yakiufunika uso wake baada ya kumwacha
mwanawe humo msituni. Ijapokuwa alimchukia, kitendo cha
kumwacha mwanawe humo peke yake kilimhuzunisha sana.
Alijua kwamba Nuru angefariki kutokana na njaa, baridi au
angevamiwa na mnyama hatari na kuliwa.Alihisi uchungu kwa
sababu mwanawe asingeweza kusimama na hata kutembea
kujitafutia njia ya kujitoa mle msituni.
Wakati Fatuma alipofika kijijini, alipata akisubiriwa na mamia ya
watu. Alishangiliwa sana na wanakijiji. Wazazi wake walikuwa
mstari wa mbele kumpokea na kumshangilia kwa vifijo na
nderemo.
“Mwanangu, hatimaye umesikiliza ushauri wa wazee wa kijiji.
Umejiondolea laana iliyokuwa ikikufuata. Umefanya jambo la
busara mwanangu. Mwache huyo marehemu mumeo ambaye
badala ya kusikiliza ushauri wa wazee, aliupuuza nayo laana
hatimaye ikamuua angali mdogo, Mzee Tonje alimwambia
mwanawe.
“Mwanangu, sijawahi kuwa na furaha kwa miaka mingi kama
leo. Hatimaye huyo shetani umemtupa msituni. Utaona jinsi
maisha yako yatakavyokuwa mazuri kuanzia leo, Bi. Zuhura
naye alimwambia mwanawe kwa furaha.
Fatuma alianza kuheshimiwa kijijini. Bado ule umaridadi wake
haukuisha na kulikuwa na wanaume zaidi ya kumi waliokuwa
wakitamani kumwoa lakini akawakataa. Bado ndoto ya kuolewa
na mwana wa mfalme ilikuwapo kichwani ikimsumbua kila
mchana na usiku. Ni siri ambayo hakutaka kumweleza yeyote
hata wazazi wake.
76
Siku saba baada ya Nuru kuachwa msituni, jambo fulani lilitokea.
Ulikuwa ni wakati wa usiku. Fatuma alikuwa amelala usingizi
mzito. Alikoroma sana kama chura. Ghafla alizinduka. Alisikia
sauti kwenye dirisha la chumba chake cha kulala. Dirisha lilikuwa
likigotwagotwa. Fatuma alisikia wimbo ufuatao.
Kijana Nuru karudi, mama naomba fungua,
Nimeileta zawadi, nguo hariri chukua,
Nje kunayo baridi, mama yangu naumia.
Fatuma aliamka haraka, akawasha taa, akatoka na kuufungua
mlango. Alishangaa kumwona mwanawe Nuru akiingia katika
nyumba, akijiburura chini kwa kuwa asingeweza kusimama.
Alikuwa amebeba kifurushi fulani mgongoni. Kifurushi hicho
kilikuwa kimefungwa vizuri jinsi zawadi inavyofungwa.
“Mama, usishangae. Nimerudi hapa nyumbani lakini wasemavyo
wa kale, mkono mtupu haurambwi. Nimekuletea zawadi kwa
kuwa nakupenda. Ichukue zawadi yako na uifungue. Tazama
kilicho ndani kisha utaniambia iwapo umeipenda zawadi au la,
Nuru alisema.
Fatuma aliifungua zawadi na kupata nguo iliyokuwa maridadi
sana. Nguo hiyo ilikuwa imetiwa nakshi za dhahabu na ilikuwa
imeshonwa kwa mtindo wa kipekee. Hiyo ilikuwa ni nguo kama
zile zilizovaliwa katika kasri la mfalme. Fatuma alitokwa na
machozi ya furaha. Hakuamini kuwa alikuwa ameletewa na
mwanawe vazi la hariri.
“Mwanangu, sikuelewi. Hili vazi umelitoa wapi? Nani kakupatia
vazi hili? Uliliiba?”
“Mama, uliponiacha msituni, nilibaki nikimwomba Mungu.
Nilimwomba Mungu anijibu kwa nini nilikuwa nikiutamani msitu,
77
mahali pa upweke. Mungu alinijibu kwa kuniletea zawadi hii, kisha
akaniagiza nikuletee wewe mama yangu, Nuru alijibu.
Fatuma alipolivalia vazi hilo, hakuamini. Alipojitazama kwenye
kioo, alikuwa akipendeza kama malkia.Alimrukia mwanawe na
kumkumbatia kwa furaha huku machozi mengi yakimtiririka
tiriri usoni pake.
“Mwanangu, sitaki kukuachilia tena.Tutaishi hapa nyumbani kwa
furaha na amani. Ijapokuwa umeniletea zawadi kutoka msituni,
naomba usirudi kule tena, Fatuma alisema.
“La hasha mama. Ngoja wazee wa kijiji wanione hapo kesho.
Watakushauri tena ushauri wa kunitupa. Nawajua wazee
hao. Wanawafanya wanakijiji wazidi kunichukia. Usijali mama.
Chochote watakachokushauri unifanyie, usiogope. Tii ushauri
wao, Nuru alimjibu akamwomba mama ampandishe kitandani
alale.
Wazee wa kijiji walipogundua baadaye Nuru hakufa, walikasirika
sana.
“Hatutakuamini tena. Ulitudanganya. Bado unampenda mwanao.
Hukumpeleka msituni kama ulivyodai. Mbona amerudi akiwa
mzima na buheri wa afya?” waliuliza.
“Hatutakuamini tena. Mara hii ya pili utaandamana na baadhi
ya wazee kwenda kumtupa mwanao mbali mno na hapa kijijini,
walimwambia.
Siku iliyofuata, walifika wazee watano nyumbani kwa Fatuma.
Ilivyokuwa desturi, Fatuma alimfungia mwanawe mgongoni kwa
ubeleko kisha safari ikaanza. Hawakuenda msituni.Walivuka mito,
maziwa na mabonde hadi wakafika eneo lililoitwa Milima Miwili.
78
Lilikuwa ni eneo lenye baridi sana hata wakawa wakitetemeka.
Fatuma, akitokwa na machozi, alimweka mwanawe chini kisha
akiwa na wazee hao wakaanza kuondoka. Fatuma alisimama
kumtazama mwanawe.
“Mama, usijali. Ondoka nao mimi ni salama, Nuru alisema kwa
sauti iliyojaa furaha.
“Twende! Safari hii, huyu mtoto wa laana lazima atakufa.
Msahau na umfute moyoni na akilini mwako, mmoja wa wazee
alimwambia.
Walimwacha na kuelekea nyumbani. Huko walipokelewa na
shangwe na nderemo kuliko mara ya kwanza. Kulikuwa na kikundi
cha vijana wa kike na kiume kilichopigiwa ngoma na kucheza.
Wazee nao hawakuachwa nyuma, kila mmoja akifurahi kwa
kuwa laana ilikuwa imeondolewa kijijini.
“Nina hakika wakati huu, huyo shetani mmemwacha mahali
ambapo hata akasafiri kwa miaka kadhaa, hawezi kufika hapa
kijijini, kiongozi wa wazee aliuliza.
“Ni kweli. Tumemwacha mbali kwenye Milima Miwili isifiwayo
kwa baridi. Hamtaweza kusikia jina Nuru tena hapa kijijini,
walijibu kwa uhakika.
Siku saba baadaye wakati wa usiku, Fatuma aliamshwa na sauti
kwenye dirisha lake. Ilikuwa ni sauti kama ile ya kwanza, dirisha
likigotwagotwa. Ghafla alisikia sauti ya mwanawe Nuru.
Aliyeachwa kwenye milima, milima yenye baridi,
Amesharudi mzima, hakuuliwa na radi,
Amemletea mama, zawadi atakayopenda.
79
Fatuma alimfungulia mwanawe ambaye aliingia katika nyumba,
akijiburura polepole. Kama ilivyokuwa mara ya kwanza, alimbebea
zawadi kwa mgongo, ikifungwa kama kifurushi.
“Mama, chukua zawadi yako halafu naomba unipakulie chakula,
nina njaa, Nuru aliomba.
Fatuma alimpakulia mwanawe wali akaujaza sahani nzima.
Alipozifungua zile zawadi, alishtuka sana. Mlikuwa na mkufu wa
dhahabu, herini, mafuta ya nywele, mafuta ya kujipaka mwili,
manukato, taji la dhahabu, bangili na viatu vya dhahabu.
“Mama, oga sasa halafu uvalie nguo niliyokuletea pamoja na
mapambo hayo, Nuru alishauri.
Mama alimtii mwanawe. Usiku huo huo alioga kisha akaivalia ile
nguo. Nakuambia Fatuma alipojitazama kiooni, chozi la furaha
lilimtoka. Alikuwa msichana mrembo hata kushinda malkia wa
nchi ile.Alibaki kujitazama pale kiooni kwa muda mrefu.
“Mama, umekuwa maridadi jinsi nilivyopenda. Wazee wa kijiji
wakitambua niko hapa, watanirejesha sehemu nyingine mbaya
kuliko ile ya baridi. Usiogope.Watii mama kwa sababu hii itakuwa
ndiyo mara ya mwisho kwenda kunitupa. Mama, nafanya yote
haya kwa sababu najua ndoto yako. Ulizawidiwa na Mwenyezi
Mungu kunizaa mimi ili ndoto yako itimie kwa hivyo usiwe na
wasiwasi, Nuru alimshangaza mama.
Siku iliyofuata, wanakijiji wote walikusanyika huku wakiomboleza.
Laana ilikuwa imerejea kijijini. Wazee walimchinja fahali na
kuitolea miungu dhabihu. Siku tatu baadaye, wazee wote
pamoja na Fatuma walifunga safari. Ilikuwa safari ndefu ya siku
nne. Walifika kwenye ukingo wa bahari. Walikuwa na kidau.
Walimweka Nuru ndani ya kidau kisha wakakiachilia kikaelea
80
baharini. Maji ya bahari yalikipeleka kidau kwa kasi hadi baada
ya nusu saa, kikapotea machoni pao.
“Mara hii, usimtarajie mwanao.Tumeshatoa dhabihu na kumtupa
baharini.Ataliwa na papa na nyangumi na kijiji chetu kiwe na
amani, kiongozi wa wazee aliwaeleza kisha wote wakaanza
safari ya kurudi nyumbani.
Siku saba baadaye mambo yale yale ya kawaida yalijirudia tena.
Nuru alirejea nyumbani usiku na kumwamsha mama yake kwa
wimbo huu.
Mama yangu mama yangu, amka usingizini,
Nishatoka kwa uvungu, kwenye kina baharini,
Ninazo zawadi chungu, nimebeba mgongoni.
Fatuma aliamka kustaajabishwa na zawadi zilizoletwa. Zilikuwa
ni zawadi zilizokuwa katika kikapu maridadi sana. Kulikuwa na
zawadi za dhahabu za kifalme, zawadi ambazo zisingepatikana
katika nchi hiyo kwa urahisi.
“Mama, weka zawadi hizi vizuri. Hivi karibuni utazihitaji. Naomba
chakula, nina njaa nyingi, Nuru alisema naye mama akampakulia
chakula, akala akashiba kisha wakalala.
Siku iliyofuata, ilijulikana kote kwamba Nuru alikuwa amerudi.
Hakuna mwanakijiji aliyetaka kuikaribia nyumba ya Fatuma.
Wazee na kila mmoja walitambua kwamba Nuru hakuwa
mwanadamu wa kawaida na juhudi za kutaka kumuua zisingefaulu.
Waliachana naye.
Mwezi mmoja baadaye, ilitangazwa kwamba, mwana wa mfalme
alikuwa akimtafuta mchumba wa kuoa. Mwana wa mfalme
alitarajiwa kuzuru vijiji vingi akijionea wasichana warembo
81
kisha angemchagua aliyempendeza. Zamu ya kijiji cha Songole
ilipofikiwa, wasichana wengi walijitokeza. Fatuma naye, alioga
siku hiyo akawa safi kisha akavalia nguo yake ya hariri yenye
nakshi za dhahabu. Alipaka nywele zake mafuta, akayaremba
macho yake, midomo yake na kuvalia herini, bangili na kila aina
ya urembo.Alijipulizia marashi yaliyonukia kama ruhani kisha
mkononi akashika kile kikapu chenye zawadi. Kila mwanakijiji
aliyemwona Fatuma, alipigwa na bumbuazi.
“Katoa wapi vazi lile la kifalme? Katoa wapi viatu na mapambo
yale ya kifalme? Katoa wapi kile kikapu maridadi?” wanakijiji
cha Songole walijiuliza.
“Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni. Labda hicho kishetani
chake ndicho kimemletea, mmoja wa wasichana aliyekuwa
amefika kubahatisha kuchaguliwa na Mwangaza aliwaambia
wenzake.
Mwangaza alipokelewa kijijini Songole kwa shangwe, vifijo,
hoihoi na vigelegele vingi. Aliwakagua wasichana ila macho
yake yakanaswa na Fatuma. Alishuka kutoka kwenye farasi,
akamkumbatia na kumbusu.
82
Alishuka kutoka kwenye farasi, akamkumbaa na kumbusu.
83
“Huyo si mwanamwali! Alikuwa ameolewa na akajifungua
mlemavu! Atakuletea laana kubwa sana, baadhi ya wasichana
walimwonya mwana wa mfalme lakini hakuwasikiliza.
Ghafla wakati huo huo, Nuru alitokea. Yalikuwa ni maajabu.
Alikuwa mvulana mkubwa na alikuwa akitembea kwa miguu
yote miwili.Wanakijiji walipomwona walitaka kutoroka.
“Msiniogope mimi. Mwogopeni Mwenyezi Mungu aliye na nguvu na
mamlaka. Nilizaliwa nikiwa mlemavu na wengi mkadhani kwamba
nilikuwa mkosi, kisirani na laana kwa kijiji hiki. Hamkujua kwamba
nilizaliwa kwa lengo moja, kutimiza ndoto ya mpenzi mama yangu.
Tangu ujanani, mama alitamani kuolewa na mwana wa mfalme,
jambo ambalo hakumweleza yeyote yule.Aliliweka siri moyoni.
Nami nilitumiwa na Mwenyezi Mungu kumtimizia ndoto yake.
Kila nilipodhulumiwa kwa kutupwa msituni, nilimletea zawadi.
Nilipopelekwa eneo lenye baridi, nilirudi na kumletea zawadi.
Nilipotupwa baharini, nilizamia hadi penye kilindi na kumletea
mpenzi mama zawadi. Nilitamani ndoto yake ya kukutana na
Mwangaza itimie na leo bila shaka kwa uwezo wa Mwenyezi
Mungu, ndoto imetimia, Nuru alisema na watu wote wakajipata
wakipiga makofi.
Siku hiyo, Nuru na mama yake walieleka kwenye kasri ya
Mfalme Fikirini. Siku saba baadaye iliandaliwa arusi kubwa ya
kukata na shoka ambayo haikuwahi kufanyika katika nchi ile.
Fatuma aliolewa kwa mwana wa mfalme, Mwangaza, naye Nuru
akachukuliwa kuishi katika kasri. Fatuma, Nuru na Mwangaza
waliishi maisha ya raha mustarehe hadi siku zao za mwisho
duniani.
84
Kamusi Yangu
adhuhuri wakati baina ya saa sita na saa tisa
mchana
dhabihu kitu kinachotolewa kwa Mwenyezi
Mungu
dhiki shida
kanzu aina ya vazi refu linalovaliwa na
wanaume
kidau chombo kidogo cha majini
kifurushi kitu kilichofungwa vizuri kwa karatasi
kilemba aina ya kitambaa
kinachofungwa kichwani
kilindi mahali majini palipo na kina kirefu
kuburuta sawa na kuvuta kitu kwa nguvu
kutwaa kuchukua
likigotwagotwa likigongwagongwa
nyangumi mnyama mkubwa sana wa baharini
papa aina ya samaki wa baharini
ruhani aina ya jini anayesadikiwa kuwa na
harufu nzuri
shingo upande bila hiari; yaani bila kupenda
ubeleko kipande cha nguo au shuka cha
kubebea mtoto
ufukara umaskini
upweke hali ya kuwa peke yako bila mtu
mwengine
vazi la hariri vazi la kitambaa laini zuri na maridadi
watemakuni watu wanaokata kuni na kuziuza
wafinyanzi watu wanaotengeneza vyungu kwa
udongo
wakatawanyika wakaenda kila upande; wakafumukana
85
Maswali
1. Kwa nini Fatuma asingeweza kutembelea maeneo mazuri na
marafiki zake?
2. Elezea jinsi Mwangaza mwana wa Mfalme alivyovalia.
3. Fatuma alipendekeza kwa mumewe Kala wamfanyie nini
mwanao Nuru?
4. Baada ya mazishi ya Kala, Fatuma alimfanyia nini mwanawe
Nuru?
5. Fatuma alipoondoka msituni alienda akilia. Kwa nini alikuwa
akilia?
6. Ni zawadi ipi ya kwanza ambayo Fatuma aliletewa na
mwanawe Nuru kutoka msituni?
7. Ziandike zawadi kadhaa ambazo Nuru alimletea mama yake
kutoka Milima Miwili.
8. Elezea jinsi Fatuma alivyovalia ile siku Mwangaza alipofika
kijijini kujitafutia mke.
9. Kwa nini wanakijiji walitoroka Nuru alipotokea?
10. Hadithi hii ina funzo gani?