
47
yalikuwa yanabubujika kama maji kwenye mfereji. Alishuka
kutoka kwenye jukwaani na kuelekea walikokuwa wameketi
wanafunzi wenzake. Huko walimkaribisha kama shujaa.
Masimulizi ya Tamara yaligusa nyoyo za wengi. Wakaguzi
walikubaliana kwa kauli moja kuwa Tamara alikariri shairi
alilokuwa ametunga kwa ajili ya tamasha hiyo.Tamara alirudi
tena jukwaani akishangiliwa na kila mtu, hata wakaguzi.
Alilikariri shairi lake kwa ujasiri mkubwa.Alitamka kila neno
kwa ufasaha. Mahadhi yake yalipendeza.
Kumbukumbu naandika, uwele nahadithia,
Miaka hadi mikaka, itasomwa historia,
Korona ililipuka, ikatingika dunia,
Makubwa yalitufika, hivi nayasimulia.
Korona ni jinamizi, janga lisilo mithili,
Halisikii mizizi, dawa na kinga ya mwili,
Huingia kama mwizi, kwa fujo bila kibali,
Kisha hukita mizizi, na kuzidisha makali.
Ilianza na uvumi, fununu na vijineno,
Watu walichonga ndimi, kueneza minong’ono,
Sikuyaamini mimi, yaliposemwa maneno,
Visa vilifika kumi, tukaonyeshwa mifano.
Walifunga mipakani, viwanja na bandarini,
Tulisalia nyumbani, hakuna kwenda shuleni,
Masomo mtandaoni, kazi ni mtandaoni,
Jirani hawaonani, hujambo hawapeani.
Tulivaa barakoa, kwa tabu tulipumua,
Ikawa kubwa hatia, kieuzi kususia,
Mikono tulisugua, sabuni tulitumia,
Virusi tuliviua, korona ilipungua.